Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Neno La Wiki

Neno la Wiki: "Kuogopa" na "Kuongopa"

Mchambuzi wako leo ni Nuhu Bakari kutoka CHAKITA, Kenya na anasema "Kuongopea" maana yake ni kudangaya, ndio maana halisi, na anasema mtanzania akikuambia unaniongopea maanake ni unanidanganya, lakini Kenya mtu akikuambia unaniongopea inaweza kuwa na maana nyingine ambayo ni unamuogopa na anasema halitumiki mno kwa sababu ya uoga huo , na katika lugha ya Kiswahili hamna neno kama kuogopea. Kwa hivyo Ongopea maana yake ni "danganya" na Ogopea "tia hofu".

Neno la wiki- Vaji

Katika Neno la Wiki hii  Ijumaa Julai 22 tunaangazia neno vaji na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, huko nchini Tanzania.

Onni Sigalla anazungumzia maana ya neno vaji ambapo anasema, vaji ni nguo rasmi, nguo maalum, nguo ambayo inayotayarishwa na ndugua, marafiki au jamaa ambazo nguo hizo ni za kumuoshea mtu aliyekufa au maiti.

Neno la wiki-Elfu mia moja au Laki moja?

Mchambuzi wetu leo ni Nuhu Zuberi Bakari, Naibu mwenyekiti wa maswala ya mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya CHAKITA. na anaagazia maneno elfu mia  moja na laki moja ambapo anasema matumizi ya neno laki moja linatumika sana nchini Tanzania huku akisema ni kwa sababu ya wepesi wa matamshi lakini neno elfu mia moja linatumika sana nchini Kenya. Kwa upande wake maneo yote yanaelezea  kitu kile kile.

Neno la Wiki-Mbashara

Katika Neno la Wiki hii  Ijumaa Juni 10 tunaangazia neno mbashara na mchambuzi wetu ni Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi, Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA, huko nchini Tanzania.

Onni Sigalla anazungumzia maana ya neno mbashara ambapo anasema, ni kipindi kinachorushwa hewani moja kwa moja na kusikika au kuonwa kwa wakati huo huo aghalabu kupitia matangazo ya redio na televisheni matumizi yake unaweza kusema, Kipindi mbashara cha televisheni kitarushwa saa moja usiku.

Neno la wiki-Afueni au Ahueni?

Katika neno la wiki tunachambua maneno afueni na ahueni, mchambuzi wetu leo ni, Nuhu Zuberi Bakari ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Maswala ya Mawasiliano kwenye Chama cha  Kiswahili cha Taifa nchini Kenya, CHAKITA. Maneno haya yote yako kwenye kiswahili lakini ni lipi sahihi kutumia?.