Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mitandao ya kijamii yahatarisha chaguo la kile mtoto wa kike anataka kufanya maishani- UNESCO

Wasichana wakiwa shuleni Yaoundé mji mkuu wa Cameroon wakisoma kutumia teknolojia ya kidijitali.
© UNICEF/Frank Dejongh
Wasichana wakiwa shuleni Yaoundé mji mkuu wa Cameroon wakisoma kutumia teknolojia ya kidijitali.

Mitandao ya kijamii yahatarisha chaguo la kile mtoto wa kike anataka kufanya maishani- UNESCO

Utamaduni na Elimu

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo inaonya kuwa licha ya kwamba teknolojia za kidijitali zinachochea ufundishaji na kujifunza, teknolojia hizo hizo zinaambatana na hatari kubwa kwa mtumiaji kama vile kuingilia faragha yake, kumtumbukiza kwenye uonevu wa kimtandao na vile vile kumuondoa kwenye mwelekeo sahihi.

 

Ikiwa imeandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni, UNESCO ripoti hiyo ya Jinsia iliyotolewa leo siku ya kimataifa ya mtoto wa kike kwenye TEHAMA, inaangazia ni kwa vipi mitandao ya kijamii inasongesha fikra potofu kuhusu jinsia, huku madhara makubwa yakiwa ni kwemye ustawi wa watoto wa kike, kujifunza kwao na jinsi ya kuchagua kile wanachotaka kufanya maishani.

Watoto wa kike wanaona maumbo ya miili yasiyo ya uhalisia

Teknolojia kwa mtazamo wake, ndio jina la ripoti hiyo ambayo inaonya kwamba maudhui na picha zinazopatiwa kipaumbele kwa kuzingatia takwimu hasa kwenye mitandao ya kijamii, vinawakutanisha watoto wa kike na video na mambo yanayochochea tabia zisizo nzuri kiafya au viwango vya maumbo ya miili visivyo vya kihalisia.

“Kukutana na mambo haya hasa kwa watoto wa kike na wasichana kunaweza kuwa na madhara kwenye kujiamini kwa msichana na pia vile anavyojiona kuhusu umbo la mwili wake,” imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa hatma yake ni mtoto wa kike kuathiriwa kwenye afya ya akili na ustawi wake, mambo ambayo ni muhimu kwa mafanikio yake kitaaluma.

Watoto wa kike wachukia maumbo ya miili yao

Mathalani UNESCO imetaja utafiti uliofanywa na mtandao wa Facebook uliobaini kuwa asilimia 32 ya wasichana barubaru walisema walipojihisi vibaya kuhusu maumbo ya miili yao, mtandao wa Instagram uliwafanya wajisikie vibaya zaidi.

Ripoti inataja pia muundo wa TikTok ulivyo na uraibu kutokana na mfumo wa video zake ulio mfupi na kumfanya mtumiaji kujikuta analazimika kushiriki. “Kufurahia huku kwa papo kwa papo kunaweza kuwa na madhara kwa muda wa mtu anaotumia kujifunza au kuzingatia kitu, na hivyo kusababisha umakini kwenye majukumu ya elimu na kujiendeleza kuwa na changamoto kubwa.

Unyanyasaji mtandaoni unaweza kusababisha wasiwasi, msongo wa mawazo na hata kujiua kwa watoto.
© UNICEF/Karel Prinsloo
Unyanyasaji mtandaoni unaweza kusababisha wasiwasi, msongo wa mawazo na hata kujiua kwa watoto.

Maudhui ya aina hiyo pia yameoneshwa kuwaondoa watoto wa kike na wasichana kwenye mstari wa kujifunza masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM.

Watoto wanatumbukia kwenye maadili yasiyo sahihi

“Maisha ya kijamii ya watoto yanazidi kuendelezwa kwenye mitandao ya kijamii. Lakini mara nyingi majukwaa haya yanayosongeshwa kwa kutumia takwimu yanatumbukiza watoto kwenye maadili ya jinsia yasiyo sahihi,” ameesma Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, alipotoa maoni yake kuhusu ripoti hiyo.

Anachosisitiza ni kwamba maadili yanapaswa kuzingatiwa pindi majukwaa haya ya mitandao ya kijamii yanapoundwa na kwamba “mitandao ya kijamii haipaswi kuwafungia wanawake na wasichana kwenye majukumu ambayo yanawekea ukomo matarajio yao kielimu na kiajira.”

Wasichana ndio wanaumizwa zaidi kuliko wavulana

Ripoti pia imetanabaisha kuwa uonevu mtandaoni unakumba wasichana zaidi kuliko wavulana, mathalani katika nchi za Ulaya, taswira za maumbo ya miili ya wasichana zilizotengenzwa kwa Akili Mnemba au AI, zinasambazwa mitandaoni na madarasani. Wanafunzi wa kike waliohojiwa kwenye ripoti hii walinukuliwa wakisema waliona picha au video ambazo hawakutaka kuziona.

Hii inadhihirisha umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye elimu, ikiwemo elimu ya masuala ya habari na taarifa, halikadhalika kanuni kwenye majukwaa ya kidijitali kwa mujibu wa Miongozo ya UNESCO ya usimamizi wa majukwaa ya kidijitali iliyozinduliwa mwezi Novemba mwaka jana.

Soma ripoti nzima hapa.