Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 90 ya wanawake na wasichana barubaru hawatumii intaneti katika nchi masikini: UNICEF

Wasichana barubaru wajifunza teknolojia ya kompyuta katika shule moja ya msingi chini India
© UNICEF/Srikanth Kolari
Wasichana barubaru wajifunza teknolojia ya kompyuta katika shule moja ya msingi chini India

Asilimia 90 ya wanawake na wasichana barubaru hawatumii intaneti katika nchi masikini: UNICEF

Wanawake

Hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya wasichana katika TEHAMA, uchambuzi uliotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF unasema asilimia 90 ya wasichana vijana na barubaru hawatumii mtandao wa intaneti hasa katika nchi za kipato cha chini wakati wenzao wa kiume wana fursa karibu mara mbili ya kuwa mtandaoni.

Maudhui ya mwaka huu ya siku hii ni “Ujuzi wa kidijitali kwa Maisha” lengo likiwa ni kuchagiza wasichana na wanawake kushamiri katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati au STEM.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa elimu wa UNICEF Robert Jenkins “Kuziba pengo la kidijitali baina ya wasichana na wavulana ni zaidi ya kuwa na fursa ya intaneti na teknolojia. Ni kuhusu kuwawezesha wasichana kuwa wabunifu, waundaji na viongozi. Endapo tunataka kukabiliana na pengo la kijinsia katika soko la ajira hususan katika masuala ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati STEM, ni lazima tuanze sasa kwa kuwasaidia vijana hasa wasichana kupata ujuzi wa kidijitali.”

Kuna tofauti katika fursa za kidijitali

Tathimini ya ripoti hiyo “Kupunguza mgawanyiko wa kidijitali: Changamoto na wito wa haraka wa hatua za usawa kwa maendeleo ya ustadi wa kidijitali” inaangalia kwa karibu mgawanyiko wa kijinsia wa kijdijitali kati ya vijana wenye umri wa miaka 15-24 kwa kuchanganua takwimu zinazopatikana kuhusu matumizi ya mtandao, umiliki wa simu za mkononi au za rununu, na ujuzi wa kidijitali katika nchi nyingi zenye uchumi wa chini, chini-kati, na baadhi ya uchumi wa kipato cha kati.

Ingawa takwimu zaidi za kijinsia zinahitajika ili kufuatilia vyema, kuelewa na kufanyia kazi ujumuishaji wa kidijitali, ripoti hiyo imegundua kuwa wasichana wanaachwa nyuma katika ulimwengu unaozidi kuwa wa kidijitali na kushikamana.

Ingawa kuendeleza fursa za ufikiaji wa mtandao ni muhimu, bado haitoshi kwa mafunzo ya ujuzi wa kidijitali.

Kwa mfano, katika nchi nyingi zilizochanganuliwa, sehemu ya vijana walio na fursa za ufikiaji wa mtandao nyumbani ni kubwa zaidi kuliko ile ya vijana walio na ujuzi wa kidijitali.

Kulingana na ripoti hiyo wasichana ndio wana uwezekano mdogo wa kupata fursa za kukuza ujuzi unaohitajika kwa ajili ya kujifunza na kuajiriwa katika karne ya 21.

Kwa wastani katika nchi na maeneo 32, wasichana wana uwezekano mdogo wa kuwa na ujuzi wa kidijitali kwa asilimia 35 kuliko wenzao wa kiume, ikiwa ni pamoja na shughuli rahisi kama vile kunakili au kubandika mafaili, kutuma barua pepe au kuhamisha mafaili.

Siku ya kimataifa ya wasichana kwenye TEHAMA, Addis Ababa, Ethiopia, 2019. (Maktaba)
© ITU/M. Jacobson – Gonzalez
Siku ya kimataifa ya wasichana kwenye TEHAMA, Addis Ababa, Ethiopia, 2019. (Maktaba)

Changamoto ni nyingi

Ripoti imefafanua kwamba miziiz ya vizuizi ni mirefu na imeenda mbali zaidi ya ukosefu wa fursa za ufikiaji wa mtandao.

Matokeo ya utafiti huo yanapendekeza kuwa mazingira ya kielimu na kifamilia yana jukumu muhimu katika mgawanyiko wa kijinsia wa kidijitali.

Kwa mfano, hata ndani ya nyumba moja, wasichana wana uwezekano mdogo sana kuliko wavulana kufikia na kuwa na uwezo wa kutumia kikamilifu mtandao na teknolojia za kidijitali.

Miongoni mwa nchi na maeneo 41 yaliyojumuishwa katika uchanganuzi huu, kaya zina uwezekano mkubwa wa kutoa simu za rununu kwa wavulana kuliko wasichana.

Vizuizi vya kupata fursa za masomo ya juu na soko la ajira, kanuni na itikadi potofu za kibaguzi za kijinsia, na wasiwasi juu ya usalama wa mtandaoni vinaweza kuzuia zaidi ujumuishaji wa kidijitali wa wasichana na ukuzaji ujuzi.

Uwezo wa wasichana hautafsiriwi kuwa ujuzi

Ripoti hiyo pia inasema kwamba hata wakati wasichana wana uwezo sawa wa kupata ujuzi wa kimsingi wa kusoma, kuhesabu na kufanya kazi kwa usawa au bora zaidi kuliko wenzao wa kiume haitafsiriwi kuwa ujuzi wa kidijitali kila mara. Ili kuondokana na vizuizi vinavyowarudisha nyuma wasichana, wanahitaji kubainiwa mapema na kupata teknolojia, mafunzo ya kidijitali na stadi za maisha, na juhudi zinazoshughulikia dhana potofu za kijinsia, hasa katika familia, na unyanyasaji mtandaoni.

UNICEF inatoa wito kwa serikali na washirika kuziba pengo la mgawanyiko wa kijinsia na kuhakikisha kuwa wasichana wanapata fursa za kufanikiwa katika ulimwengu wa kidijitali.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni pamoja na:

- Fundisha ujuzi wa kidijitali kwa usawa kwa wasichana na wavulana walio ndani na nje ya shule, ukijumuisha programu za jamii.

- Kulinda usalama wa wasichana mtandaoni kupitia fursa pepe salama, será, sheria na elimu.

- Kuza fursa za ufikiaji rika wa wasichana katika kujifunza, ushauri, uanagenzi, mafunzo na mafunzoya ya vitendo kazini katika ulimwengu wa kidijitali/STEM.