Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la mihadarati mtandaoni INCB yaja na suluhu

Dawa za kulevya za aina ya Cocaine zanaswa katika Bandari ya Kingston, Jamaika, mnamo Machi 2023.
© UNODC
Dawa za kulevya za aina ya Cocaine zanaswa katika Bandari ya Kingston, Jamaika, mnamo Machi 2023.

Ongezeko la mihadarati mtandaoni INCB yaja na suluhu

Afya

Walanguzi wa mihadarati wanaendelea kutumia teknolojia za kidijitali, mitandao ya kijamii na taarifa potofu kuuza biashara zao haramu na kuchochea matumizi ya mihadarati au dawa za kulevya duniani imesema ripoti mpya iliyozinduliwa leo ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo ya utafiti wa Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti dawa za Kulevya INCB inapendekeza kutumia mbinu sawa ili kuendesha kampeni za kukabiliana na dawa za kulevya zinazotoa ushauri ambao unaweza kuaminiwa kwenye mifumo maarufu ya mtandaoni.

"Tunaweza kuona kwamba ulanguzi wa dawa za kulevya haufanywi tu kwenye mitandao haramu. Majukwaa halali ya biashara ya mtandaoni yanatumiwa na wahalifu pia,” amesema Jallal Toufiq, Rais wa INCB.

Ripoti imesema magenge ya wahalifu hutumia fursa hiyo kufikia hadhira kubwa ya kimataifa kwenye chaneli za mitandao ya kijamii kwa kuzigeuza kuwa soko na kuchapisha maudhui yasiyofaa, yanayopotosha na yanayolenga na kanuni za algoriti ambayo yanapatikana kwa wingi kwa watoto na vijana barubaru.

Kilimo cha afyuni

Waandishi wa ripoti hiyo wamebaini kupungua kwa kiasi kikubwa kwa kilimo cha kasumba au afyuni na uzalishaji wa heroini nchini Afghanistan, kufuatia Taliban kupiga marufuku dawa za kulevya. 

Lakini kuongezeka kwa biashara ya methamphetamine Asia Kusini kunahusishwa na utengenezaji wake nchini Afghanistan na maduka huko Ulaya na Oceania.

Nchini Colombia na Peru, ripoti imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la kilimo haramu cha koka, na kupanda kwa asilimia 13hadi asilimia 18 mwaka 2022.

Ukamataji wa Cocaine pia ulifikia kiwango cha rekodi mpya mwaka 2021 Afrika Magharibi na Kati, ambalo ni eneo kubwa la usafirishaji.

Na mataifa ya visiwa vya Pasifiki yamebadilika kutoka kuwa kitovu pekee cha kupitisha kwenye njia za ulanguzi wa dawa za kulevya hadi kuwa masoko ya dawa za bandia au syntetisk.

Huko Amerika Kaskazini, mzozo wa opioid unaendelea, na idadi ya vifo vinavyohusishwa na opioids za bandia isipokuwa methadone ilipita 70,000 mwaka wa 2021. 

Barani Ulaya, nchi kadhaa zinatafuta soko la bangi kwa madhumuni yasiyo ya matibabu, ambayo, wataalam wa INCB wanaamini inaweza kuwa haiendani na udhibiti wa dawa za kulevya.

Hatari kubwa mtandaoni

Mitindo mingine inayohusishwa na uuzaji wa dawa za kulevya leo ni pamoja na utumiaji wa mbinu za siri katika mawasiliano na miamala na kuvinjari bila majina kwenye mtandao wa kujificha, pamoja na malipo katika njia za siri ambazo ni ngumu kufuatilia, ambayo huongeza changamoto kwa waendesha mashtaka.

Ripoti ya INCB pia imeangazia jinsi wahalifu huhamisha shughuli zao hadi katika maeneo yenye utekelezaji wa sheria usio na masharti magumu au vikwazo vyepesi, mara nyingi wakichagua nchi ambapo uhamishaji unaweza kuepukwa.

Takwimu za hivi karibuni pia zinasisitiza ongezeko la hatari ya utumiaji wa dawa hatari kupita kiasi unaohusishwa na upatikanaji mtandaoni wa dawa za fentanyl mara nyingi zaidi ambao ni uraibu kuliko wa heroini na afyuni bandia au sintetiki.

Sehemu nyingine inayotia wasiwasi ni telemedicine na maduka ya dawa mtandaoni. 

Ingawa huduma kama hizo zina uwezo wa kuimarisha ufikiaji wa huduma ya afya na kurahisisha maagizo na utoaji wa dawa za kuokoa maisha, maduka haramu ya mtandao ambayo huuza dawa bila agizo la daktari moja kwa moja kwa watumiaji ni hatari kubwa kiafya.

Biashara ya kimataifa ya dawa haramu inakadiriwa kuwa dola bilioni 4.4.

Mara nyingi, haiwezekani kwa watumiaji kujua kama dawa wanazonunua ni ghushi, zimepigwa marufuku au ni haramu.

Ili kukabiliana na tishio la mtandaoni, waandishi wa ripoti hiyo wanasisitiza kwamba majukwaa ya mtandao yanapaswa kutumiwa kuongeza ufahamu kuhusu uraibu wa dawa za kulevya katika kuunga mkono kampeni za afya ya umma, hasa zinazolenga vijana.

Na kwa kuzingatia hali ya kimataifa ya changamoto hiyo, nchi zinapaswa kushirikiana kutambua na kukabiliana na vitisho vipya, ilisema INCB, ambayo wanachama wake 13 wamechaguliwa na Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC).