Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW68: Mkutano waanza leo New York Marekani kumalizika 22 Machi

Jinsi inavyokuwa kwenye mkutano wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW. Huu ulikuwa mkutano wa mwaka 2019. (Maktaba)
UN Women/Ryan Brown
Jinsi inavyokuwa kwenye mkutano wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW. Huu ulikuwa mkutano wa mwaka 2019. (Maktaba)

CSW68: Mkutano waanza leo New York Marekani kumalizika 22 Machi

Wanawake

Hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani unaanza mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68, kusanyiko kubwa zaidi la kila mwaka la Umoja wa Mataifa linalomulika usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women kupitia wavuti wake linasema maudhui yanayopatiwa kipaumbele kwenye mkutano huo unaoanza leo hadi tarehe 22 mwezi huu wa “Chagiza mafanikio ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake wote na wasichana kwa kuondoa umaskini na kuimarisha taasisi na ufadhili kwa kuzingatia jinsia.”

Katika mkutano huu wa CSW68, wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia, wataalamu, wanaharakati kutoka kona mbalimbali za dunia watakutana kujadili na kukubaliana juu ya hatua na uwekezaji ambao unaweza kumaliza umaskini miongoni mwa wanawake na hatimaye kusongesha usawa wa kijinsia

Dunia iko njiapanda usawa wa jinsia

UN Women inasema  dunia hivi sasa iko katika njiapanda kuelekea usawa wa jiinsia, kwani duniani kote asilimia 10.3 ya wanawake wanaishi kwenye umaskini wa kupindukia na ni maskini kuliko wanaume.

“Maendeleo kuelekea kutokomeza umaskini yanahitaji kasi ya mara 26 zaidi ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030,” inasema UN Women.

Hata hivyo UN Women inasema kuchagiza kasi ya kufanikisha SDGs kunahitaji uwekezaji.

Takwimu kutoka nchi 48 zenye uchumi unaoendelea zinaonesha kuwa nyongeza ya dola bilioni 48 inahitajika kila mwaka kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake katika malengo yote ya msingi ikiwemo kutokomeza umaskini na njaa.

Mwanamke akiandaa chakula jikoni kwake katika moja ya vijiji nchini Chad
© WFP/Evelyn Fey
Mwanamke akiandaa chakula jikoni kwake katika moja ya vijiji nchini Chad

Tumia uchaguzi kuamua kuongeza uwekezaji

UN Women inasema pia mwaka huu watu bilioni 2.6 watapiga kura kwenye chaguzi za rais, wabunge, magavana na madiwani, hivyo wana uwezo wa kudai uwekezaji zaidi kwenye usawa wa jinsia.

Majawabu ya kumaliza umaskini miongoni mwa wanawake yanatambulika kwa kiasi kikubwa, inasema UN Women, ikitaja majawabu hayo kuwa ni pamoja na kuwekeza kwenye sera na miradi inayoshughulikia ukosefu wa usawa wa jinsia na kuimarisha mashirika ya wanawake, halikadhalika wanawake viongozi.

Uwekezaji huo una faida kubwa kwani zaidi ya wanawake na wasichan milioni 100 wanaweza kuondoka katika lindi la umaskiniiwapo serikali zitapatia kipaumbele elimu, uzazi wa mpango, ujira sahihi na wa usawa, kupanua huduma ya hifadhi ya jamii.

Halikadhalika takribain ajira milioni 300 zinaweza kuanzishwa ifikapo mwaka 2035 kupitia uwekezaji kwenye huduma ya malezi na uangalizi.

Kuziba pengo la jinsia kwenye ajira kunaweza pato la ndani la taifa kwa asilimia 20 kwenye maeneo yote duniani, inasema UN Women.

Jiongezee uelewa kuhusu CSW

Bofya hapa kupata ratiba nzima hapa.

Bofya hapa kufahamu kwa kina kuhusu CSW 

Bofya hapa kutazama Habari kwa Picha kuhusu wanawake.