Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msuya: mambo matatu ya kufanya kusaidia wanawake walioko kwenye mizozo

Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura OCHA Bi. Joyce Msuya. (Maktaba)
COP28/Mahmoud Khaled
Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura OCHA Bi. Joyce Msuya. (Maktaba)

Msuya: mambo matatu ya kufanya kusaidia wanawake walioko kwenye mizozo

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68, ukiendelea hapa jijini New York Marekani hii leo kuna mikutano kadhaa inaendelea ya kujadili mambo mbalimbali ikiwemo hali ya wanawake nchini Afghanistan, kuziba pengo la kujinsia kwenye elimu, athari za umaskini na uhalifu katika huduma ya utoaji mimba pamoja na mkutano wa kuangalia jinsi mabunge yanayozingatia jinsia katika kuendeleza usawa wa kijinsia ili kumaliza umaskini. 

Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura OCHA Bi. Joyce Msuya amehuduria mkutano ulioandaliwa na serikali ya Uturuki unaongalia athari Mbaya za Migogoro kwa Wanawake na Wasichana. 

Katika hotuba yake Bi.Msuya ambaye hivi karibuni alikuwa ziarani nchini Somalia alikokwenda kuungana na wanawake wa nchi hiyo kuadhimisha siku ya wanawake duniani, alieleza yale aliyojionea ikiwemo juhudi mbalimbali za wanawake pamoja na kushauri mambo makuu matatu ya kufanya ili kuwasaidia wanawake walio katika maeneo yenye mizozo ili si tu kuwalinda bali pia kuwawezesha ili waweze kujipangia wenyewe mstakabali bora wa maisha yao ya baadae.

Mosi, kuhakikisha sauti zao zinasikika. 

Bi. Msuya ameeleza kuwa hii si tu kupaza sauti zao na kuhakikisha zinasikika kwa watunga sera, vyombo vya habari na umma ila ni kuhakikisha kila mtu anazungumza kupinga ukimwaji wanaokutana nao pamoja na mateso wanayopitia. 

“Ni kutambua kuwa kusaka amani na usalama kwa kweli kwenye mizozo ni kuhakikisha wanawake wanahusishwa kushiriki kwenye kufanya maamuzi kikamilifu. Kwa usawa na kwa maana katika ngazi zote ndani ya jamii.” 

Ili hilo liwezekane amesema wanawape wanapaswa kupewa nafasi kwenye ngazi za juu za uongozi katika kila aina ya uongozi unaofanya kazi ya kumaliza migogoro, kutafuta suluhu au shughuli za kibinadamu. Na kwa kuongezea amesisitiza ufadhili wa mashirika yanayoongozwa na wanawake. 

kuongea dhidi ya ukiukwaji mkubwa wanaoteseka - ingawa zote mbili ni za msaada.

Pili, kuwapatiwa ulinzi wa haraka ili kuepuka athari mbaya za mzozo

Inafahamika wazi kuwa inapotokea mizozo wanawake na wasichana ndio huadhirika zaidi. Vitendo kama ukatili wa kijinsia vinatumika kama silaha wakati wa vita, mifumo ya afya inashindwa kufanya kazi, Kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia, ndoa za utotoni, biashara haramu ya binadamu, ombaomba, na utumikishwaji wa watoto huongezeka, afya ya akili na kimwili inashuka.

Naibu Mkuu huyo wa OCHA amesema wadau wa masuaka ya kibinadamu, wafadhili na washirika wao wanapaswa haraka kuongeza ufadhili ili kwenda kushughulikia changamoto zinazowakumba wanawake na wasichana. 

“Hii inamaanisha kuelekeza fedha kwenda kusaidia mashirika yanayoongozwa na wanawake wanaofanya kazi e mstari wa mbele. Inamaanisha kutekeleza ulinzi wa hospitali chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ikijumuisha huduma za kabla na baada ya kujifungua na vifaa vya kujifungulia.”

Tatu, Kukomesha unyanyasaji badala ya kushughulikia matokeo mabaya ya ukatili dhidi yao

Akifafanua suala hili la mwisho katika hotuba yake Bi. Msuya amesema mara tu mzozo au vita inapotokea basi watekelezaji wa sheria, wanajeshi na walinda amani wamefunzwa kikamilifu jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.

“Kutengeneza maeneo salama ambapo wanawake na wasichana wanaweza kusaka hifadhi na usaidizi. Inahusu kupinga kanuni hatari za kijamii, kukuza usawa na kuongeza ufahamu kuhusu dhuluma ambayo wanawake wanateseka, na kufanya hivyo katika kila ngazi ya jamii na katika kila shirika.” 

Bi Msuya amesisitiza kuwa ili kwenda kuleta maendeleo ya kweli nakuondoa ukosefu wa usawa ndani ya jamii lazima kushughulikia chanzo kikuu cha ukosefu wa uaswa

Ikiwa tutafanya maendeleo ya kweli, basi hatuwezi tu kujibu matokeo ya ukosefu wa usawa. Badala yake, lazima tushughulikie chanzo kikuu cha ukosefu wa usawa, mila na kanuni potofu na za kibaguzi kijinsia, mitazamo na tabia za mtu binafsi, na miundo ya mamlaka inayoendeleza vurugu.

Iwapo hayo yote yakishughulikiwa na wanawake wakiwezeshwa itasaidia kuwa ruhusu kusimamia na kuongoza mustakabali wa pamoja kuelekea ulimwengu ambao ni bora kwa sababu ya ushiriki wao na uongozi.