Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Hofu yatanda mzozo kuenea ukanda mzima Mashariki ya Kati

Baraza la Usalama la UN lakutana kujadili Mashariki ya Kati
UN
Baraza la Usalama la UN lakutana kujadili Mashariki ya Kati

Gaza: Hofu yatanda mzozo kuenea ukanda mzima Mashariki ya Kati

Amani na Usalama

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili hali ya Mashariki ya Kati hususan suala la Palestina wakati huu ambapo mapigano yanaendelea huko Ukanda wa Gaza, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya mzozo huo kusambaa kwenye ukanda huo.

 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa ikisema kuwa “kadri uhasama unavyozidi huko Gaza kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, Hamas pamoja na vikundi vingine vilivyojhami, Katibu Mkuu ana wasiwasi mkubwa juu ya kusambaa zaidi kwa mzozo huo, hali ambayo inaweza kuleta madhara makubwa kwenye ukanda mzima.

Taarifa hiyo kutoka kwa Stéphane Dujarric, inasema kuna hatari kubwa ya ukanda mzima kutumbukia kwenye mzozo kwa kuzingatia hatari ya kuendelea na kutokuzingatiwa kwa masuala mbali mbali.

Halikadhalika taarifa hiyo imeelezea kuongezeka kwa ghasia kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordani ikiwemo kushamiri kwa operesheni za kijeshi za jeshi la Israel, idadi kubwa ya vifo, na mashambulizi yanayofanywa na wapalestina dhidi ya walowezi wa kiisraeli, taarifa ikisema “vyote hivyo vinatia hofu kubwa.”

Utulivu wa kikanda umeathiriwa vibaya

“Mapigano ya kila wakati kwenye eneo lisilotakiwa kuwa na shughuli za kijeshi kati ya Lebanon na Israel yanaathiri utulivu wa ukanda huo,” imesema taarifa hiyo ikieleza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anazidi kuwa na hofu ya kusambaa kwa mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami huko Iraq na Syria, halikadhalika mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami vya wahouthi huko Yemen dhidi ya vyombo vya majini kwenye bahari ya Shamu, matukio ambayo yameshamiri siku za karibuni.

“Bwana Guterres amesihi pande zote kujizuia na zichukue hatua za dharura kumaliza mvutano kwenye eneo hilo,” imesema taarifa hiyo.

Zaidi ya yote, Katibu Mkuu amesihi jamii ya kimataifa ifanye kila iwezalo kutumia ushawishi wao kwa  pande husika kwenye mzozo ili kuzuia kusambaa zaidi kwa mzozo huko Mashariki ya Kati.

“Katibu Mkuu anasisitiza wito wake wa sitisho la mapigano hivi sasa huko Gaza kwa misingi ya kiutu na kuachiliwa huru mateka wote bila masharti yoyote,” imetamatisha taarifa hiyo.

Baraza la Usalama nalo lajadili Mashariki ya Kati

Mapema asubuhi Baraza la Usalama lilipokutana saa tano na dakika tano asubuhi kwa saa za New York, Marekani,  Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Mashariki ya Kati Khaled Khiari alijulisha wajumbe kuwa hali ya MAshariki ya Kati inatisha na inaendelea kudhoofika kila uchao, ikiwemo kuweko kwa matukio ya mzozo yanayoungana.

Amesema operesheni nzito za kijeshi za ardhini kati ya jeshi la Israel na kikundi cha Hamas na vinginevyo kwenye maeneo mengi ya Gaza, wakati ambapo Hamas nao wanaendelea kurusha maroketi kutoka Gaza kuelekea Israel.

“Raia pande zote, hususan Gaza hivi sasa wanaendelea kubeba mzigo wa madhara ya mapigano haya,” amesema afisa huyo wa UN.

Mashambulizi yaripotiwa Syria, Iraq na Bahari ya Shamu

Amerejelea wito wa Katibu Mkuu wa sitisho la haraka la mapigano kwa misingi ya kiutu huko Gaza huku akionya kuwa mzozo huo unaweza kuwa na madhara kwenye ukanda mzima.

Bwana Khiari amegusia pia mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani huko Iraq na Syria, huku Marekani ikifanya mashambulizi ya anga dhidi ya makundi yanayoshukiwa kufanya vitendo hivyo huko Iraq na Syria.

Aidha ametaja ripoti za mashambulizi ya anga ya Israel nchini Syria pamoja na mivutano huko bahari ya Sham.

Palestina: Kinachotokea dhidi ya wapalestina kimepangwa mapema

Akihutubia Baraza la Usalama, Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Majed Bamya amesema “mauaji ya raia wa kipalestina si matokeo ya kisichotarajiwa cha vita inayoendelea, bali ni matokeo ya mashambulizi ya Israel yenye lengo kuua raia kwa kiwango kikubwa. Janga la kibindamu Gaza si matokeo ya vita. Ni mbinu inayotumiwa na Israel kushinikiza  watu waondoke. Baa la njaa linalonyemelea ni jambo lililopangwa kwenye vita hii.”

Balozi Bamya amesema njaa ni mbinu mojawapo ya vita. Halikadhalika kudhoofika kwa mifumo ya afya. “Ni matokeo ya mashambulizi yaliyopangwa mapema dhidi ya hospitali na wahudumu wa afya,” amesema Mwakilishi huyo wa Palestina.

Ameelezea pia kuwa mauaji ya jumla, kukamatwa watu kiholela na kuwapiga video wapalestina, halikadhalika kutoweshwa na kuuawa kinyume cha sheria, vyote vinalenga kuwajengea hofu wapalestina.

Israel: Hamas yaendelea kurusha maroketi Israel

Balozi Gilad Erdan ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa alimulika mashambulizi ya maroketi kutoka Hamas akisema, “jana asubuhi tu, maroketi yalirushwa kutoka Lebanon na kupiga maeneo ya kati yenye watu wengi kwenye miji ya kaskazini mwa Israel ya Haifa na Akko. Siku mbili zilizopita, maroketi yalirushwa kwenye mji wa kaskazini wa Israel wa Kiryat Shmona.”

Halikdhalika amesema siku tatu zilizopita, wanamgambo wa Hezbollah walirusha kombora kwenye kanisa la Mt. Maria huko Galilaya magharibi na kujeruhi watu 11.

“Lakini mashambulizi haya dhidi ya raia, miji na majiji pamoja na maeneo matakatifu hayaonekani kuchochea kikao cha dharura cha Baraza la Usalama. Je mashambulizi haya hayaonekani kuwa ndio kusambaa kwenyewe kwa mzozo? Je mashambulizi haya yanafanyika kimazingara?” alihoji Balozi Erdan.