Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: UN yataka misaada zaidi iingie wakati watu wengi wakikimbilia Rafah

Watu wanaokimbia mapigano huko Gaza wanaendelea kutafuta maeneo salama ya kujihifadhi katika eneo hilo.
© UNICEF/Eyad El Baba
Watu wanaokimbia mapigano huko Gaza wanaendelea kutafuta maeneo salama ya kujihifadhi katika eneo hilo.

Gaza: UN yataka misaada zaidi iingie wakati watu wengi wakikimbilia Rafah

Amani na Usalama

Huko Ukanda wa Gaza, Mashariki  ya Kati, takribani watu 100,000 waliofurushwa makwao hivi karibuni kutokana na mashambulizi yanayoendelea kutoka Israel wamemiminika Rafah, umesema Umoja wa Mataifa hii leo, na hivyo kufanya hali kuwa mbaya zaidi ya kibinadamu kwenye sehemu hiyo ya eneo hilo la kusini zaidi lililozingirwa na Israel.

 

“Watu wana kiwewe na wamechoka na sasa wanalazimika kulundikana kwenye eneo lenye usalama linalozidi kuwa dogo kila uchao,” amesema Martin Griffiths, Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, kupitia ukurasa wake wa X.

Hata hivyo vikwazo bado vinazidi kuibuka dhidi ya wale wanaotaka kupeleka misaada zaidi kutokana na mashambulizi makali yanayofanywa na Israel kutokea angani na ardhini.

OCHA inataja ripoti kutoka mamlaka za afya Gaza zinazosema kuwa nusu ya wajawazito waliosaka usalama kwenye makazi ya muda Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na kiu, utapiamlo na ukosefu wa huduma za afya. Hakuna chanjo kwa watoto wachanga na mtoto mmoja kati ya watoto wawili wakimbizi anakabiliwa na ukosefu wa maji mwilini, utapiamlo na magonjwa.

Takribani wakazi milioni 1.9 wa Gaza au asilimia 85 ya wakazi wote kwenye eneo hilo lililozingirwa na Israel, wamefurushwa makwao tangu Israel ilipoanza kulipiza kisasi cha mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba mwaka huu.

Mlundikano usio wa kawaida

Kwa mujibu wa OCHA, wimbi jipya la watu kukimbia makaziyao limechochewa na ongezeko la mashambulizi kwenye mji wa kusini wa Khan Younis na eneo la kati mwa Gaza la Deir al Balah, pamoja na amri za kuondoka zinazotolewa na jeshi la Israel.

Takribani siku 10 zilizopita, mji wa Rafah tayari ulikadiriwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu ukanda wa Gaza, ikizidi watu 12,000 katika kila kilometa moja ya mraba, imesema OCHA, idadi ambayo ni zaidi ya jiji la New York, Marekani kwenye ukubwa kama huo.

Ufikishaji misaada una vikwazo

Licha ya azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kuimarishwa kwa kasi ya kupeleka misaada kwenye eneo hilo lililozingirwa, bado ufikiaji wa watu unakumbwa na mkwamo mkubwa.

Ni malori 76 yenye shehena za misaada ndio yameingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah upande wa Misri jana Alhamisi, “idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na malori 500 kila siku kabla ya kuanza kwa mashambulizi Oktoba 7,” imesema OCHA.

“Unadhani kuingiza misaada Gaza ni rahisi? Hebu fikiria tena,” amesema Bwana Griffiths kupitia mtandao wa X leo Ijumaa. Ametaja vikwazo lukuki vinavyokabiliwa watoa misaada ya kibinadamu huko Ukanda wa Gaza, ikiwemo “ngazi tatu za ukaguzi kabla hata ya gari kuingia”, uhaba wa maeneo ya kuingilia, “mashambulizi ya mara kwa mara na barabara mbovu.

“Hii ni hali isiyowezekana kwa watu wa Gaza na wale wanaojaribu kuwasaidia. Mapigano lazima yakome,” amesisitiza Bwana Griffiths.

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema kuwa “operesheni fanisi ya kufikisha misaada Gaza inahitaji usalama; wafanyakazi wa kufanya kazi zao kwa usalama; uwezo wa kivifaa na kurejea kwa shughuli za kibiashara.”

“Kwa sasa mambo haya manne hayako,” alisema Guterres.