Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kura za Baraza la Usalama zapitisha Azimio zito kuhusu Gaza

Mwonekano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wanachama wanapiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio kuhusu hali ya Mashariki ya Kati tarehe 22 Desemba 2023.
UN Photo/Loey Felipe
Mwonekano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati wanachama wanapiga kura kuunga mkono rasimu ya azimio kuhusu hali ya Mashariki ya Kati tarehe 22 Desemba 2023.

Kura za Baraza la Usalama zapitisha Azimio zito kuhusu Gaza

Amani na Usalama

Mchana huu wa Ijumaa 22 Novemba saa za New York, Marekani, Baraza la Usalama limeidhinisha azimio linalozitaka pande zinazohusika katika mzozo wa Gaza kuruhusu usambazaji wa haraka wa msaada wa kibinadamu kwa raia wa Palestina katika Ukanda wote wa Gaza. Nyaraka hiyo pia inataka hatua za haraka zichukuliwe ili kuunda mazingira ambayo yanasababisha usitishaji endelevu wa uhasama. Maandishi hayo yameidhinishwa kwa kura 13 za ndiyo, huku Marekani na Urusi zikijiepusha kupiga kura. 

 

Matokeo ya kura ni kama ifuatavyo: 

Ndiyo: Kura 13 (China, Uingereza, Ufaransa, Japan, Gabon, Albania, Ecuador, Ghana, Malta, Uswizi, Msumbiji, Brazil, Falme za Kiarabu) 

Hapana: Kura 0 

Hawakupiga kura: Kura 2 (Marekani, Urusi) 

Mratibu wa kufuatilia utoaji wa misaada ya kibinadamu

Azimio lililopitishwa pia linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kumteua Mratibu Mwandamizi wa Masuala ya Kibinadamu na Ujenzi, ili awajibike kuwezesha, kuratibu, kufuatilia na kuthibitisha huko Gaza, "hali ya kibinadamu ya shehena zote za misaada ya kibinadamu zinazopelekwa Gaza zinazotumwa na Mataifa ambayo sio sehemu ya mzozo. Lengo ni kuharakisha utoaji wa misaada ya kibinadamu.

Azimio hilo linazitaka pande zinazohusika katika mzozo huo kushirikiana na mratibu, ambaye atapewa mamlaka ya kuripoti kwa Baraza la Usalama kuhusu kazi yake ndani ya siku 20 kwa mara ya kwanza, na kila siku 90 baada ya hapo.

Mchakato haukuwa rahisi

Baada ya mazungumzo makali ya faragha kwa wiki nzima katika Baraza la Usalama lenye wanachama 15 (watano wa kudumu), mabalozi wamepiga kura asubuhi hii ya saa za New York Marekani kuhusu rasimu ya azimio lililoandikwa na Umoja wa Falme za Kiarabu ambalo limeripotiwa kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili kuruhusu utoaji wa misaada kwa usalama na bila vikwazo kwa raia walioathirika katika Ukanda wa Gaza.

Jana Alhamisi, wajumbe wa Baraza waliendelea na mashauriano yao ya faragha hadi jioni. 

Balozi wa Marekani na Mwakilishi wa Kudumu wan chi hiyo katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield alijitokeza kwenye mkutano huo wa jana, na kuwaambia waandishi wa habari kwamba baada ya kufanya kazi kwa bidii katika wiki iliyopita, nchi yake ilikuwa tayari kuipiga kura  rasimu ya azimio, ikiwa maafikiano yaliyofanywa yatabaki katika rasimu mpya. 

Rasimu ya mwisho kupigiwa kura ilipigiwa kura ya turufu na Marekani tarehe 8 Desemba, ambayo ilifuatiwa haraka na hatua ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku nne baadaye, wakati Nchi Wanachama zilipiga kura kwa wingi wa kura kuunga mkono usitishwaji wa mapigano wa haraka wa kibinadamu ingawa azimio hilo halina nguvu kisheria.  

Kuepuka kura nyingine ya turufu 

Baraza limekuwa likijadiliana kwa wiki nzima kutafuta lugha ambayo itaepusha kura ya turufu nyingine kutoka kwa Marekani, baada ya kwanza kuwasilisha rasimu iliyotaka "kusitishwa kwa uhasama", ambayo sasa inataka "kusitishwa" kwa mapigano, ili kuongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa msaada wa kuokoa maisha. 

Marekani ilisema siku ya Jumanne na katika vikao vya awali vilivyokuwa na mkwamo kwamba azimio lolote linapaswa kulaani ‘mashambulizi ya kigaidi ya kundi la Hamas ya tarehe 7 Oktoba’ ambayo yalisababisha ongezeko kubwa la mzozo kati ya Palestina na Israel na kusababisha vifo vya watu 1,200 kusini mwa Israel na kukamatwa kwa zaidi ya mateka 200, kadhaa kati yao wanasalia kuwa mateka huko Gaza. 

Baadhi ya nchi zinazokosoa hujuma ya Israel zimedai kujibu kwamba azimio lolote la kulaani Hamas, lazima pia lilaani uvamizi wa Israel na maelfu ya vifo vya raia vilivyotokana na hatua ya kijeshi ya Israel tangu tarehe 7 Oktoba.