Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Janga linavyozidi kushamiri, sitisho la mapigano ni jambo la dharura

Watu waliofurushwa makwao kutokana na mapigano Gaza wakiteka maji kwenye kambi ya wakimbizi iliyoko katika mji wa Khan Younis.
© WHO
Watu waliofurushwa makwao kutokana na mapigano Gaza wakiteka maji kwenye kambi ya wakimbizi iliyoko katika mji wa Khan Younis.

GAZA: Janga linavyozidi kushamiri, sitisho la mapigano ni jambo la dharura

Amani na Usalama
  • Udharura wa sitisho la mapigano unazidi kudhihirika kadri mapigano yanavyoshamiri Gaza
  • Idadi ya wanahabari na watumishi wa misaada wa UN waliouawa imevunja rekodi 
  • Mateka wanaoshikiliwa waachiliwe huru bila masharti na raia walindwe

Mapigano yanavyozidi kushamiri Ukanda huku kukiwa na hatari ya mapigano hayo kuenea Mashariki ya Kati, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa usaidizi wa dola bilioni 1.2 kusaidia takribani watu milioni tatu kwenye eneo hilo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel.

“Jinamizi lililoko Gaza ni zaidi ya janga la kibinadamu. Ni janga la kiutu,” amesema Katibu Mkuu Jumatatu akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani.

Ameelezea pia hofu yake juu ya ongezeko la mapigano na kupanuka kwa mapigano kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Kipalestina, Hamas, akitaja kuwa “Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel ikiwemo mji wa Yerusalem Mashariki ni eneo ambalo linatokota.”

‘Eneo la makaburi ya watoto’

Bwana Guterres amegusia jinsi “janga linavyozidi kushamiri huko Gaza na kudhihirisha  umuhimu wa sitisho la mapigano kwa misingi ya kiutu kila saa inayokatika,” akisisitiza pia ulinzi wa raia ni muhimu kupita kiasi.

Gaza inakuwa eneo la makaburi kwa watoto. Mamia ya watoto wa kike na wa kiume wanaripotiwa kuuawa au kuachwa na ulemavu kila siku,” amesema Katibu Mkuu.

“Waandishi wa habari wengi zaidi wameripotiwa kuuawa katika kipindi cha zaidi ya wiki nne zilizopita, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko kwenye mzozo wowote katika kipindi kisichozidi miongo mitatu. Wafanyakazi wengi zaidi wa Umoja wa MAtaifa wanaohusika na kutoa misaada wameuawa kuliko katika kipindi chochote kile cha historia ya shirika letu.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres akizungumza na waandishi wa habari 06 Novemba 2023 kuhusu kinachoendelea kutokana na mapigano huko Ukanda wa Gaza kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, Hamas.
UN /Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari 06 Novemba 2023 kuhusu kinachoendelea kutokana na mapigano huko Ukanda wa Gaza kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, Hamas.

Ombi la usaidizi kwa Gaza Mahitaji lukuki

Ombi la usaidizi wa kiutu lililozinduliwa leo na Umoja wa Mataifa na wadau wake linalenga idadi  ya wakazi wote wa Ukanda wa Gaza na wapalestina 500,000 walioko Ukingo wa Magharibi, ikiwemo mji wa Yerusalem Mashariki.

Bwana Guterres amesema ijapokuwa baadhi ya misaada inaingia Gaza kupitia Misri, kiwango cha msaada ni sawa na tone la maji baharini, kwani mahitaji ni lukuki.

Katika wiki mbili zilizopita, jumla ya malori 400 yameingia Gaza ikilinganishwa na malori 500 yaliyokuwa yakiingia eneo hilo kila siku kabla ya kuanza kwa mzozo, na misaada hiyo haijahusisha nishati ya mafuta inayohitajika.

“Bila nishati ya mafuta, watoto wachanga walioko kwenye vifaa vya kuwapatia joto pamoja na wagonjwa waliowekewa mashine za kupumulia, hawataweza kuishi, watakufa,” ameonya Katibu Mkuu.

Maji vila vile hayawezi kusukumwa ili kufikia wahitaji, bila kusahau pia hayawezi kutakatishwa na kuondolewa chumvi kwani mitambo inahitaji nishati ya mafuta.

Changamoto nyingine majitaka kutoka vyooni punde yataanza kutiririka kwenye mitaa na kusambaza magonjwa kwani mitambo ya kuchakata haina mafuta au  imeharibiwa.

Sitisho la mapigano kwa misingi ya kiutu sasa

Mwelekeo sasa ni dhahiri kwamba narejelea wito wangu wa sitisho la mara moja kwa ajili ya huduma za kiutu, na pande zote ziheshimu sheria ya kimataifa.

Amesisitiza pia wito wake wa kuachiliwa huru bila masharti yoyote waisraeli wanaoshikiliwa mateka na Hamas huko Gaza na kwa ulinzi wa raia, hospitali, maenoe ya Umoja wa Mataifa, makazi na shule.

“Chakula zaidi, maji zaidi, dawa zaidi na bila shaka nishati ya mafuta – viingie Gaza kwa usalama na haraka, na kwa kiwango kinachohitajika. Sasa! Njia ya kuingia Gaza bila vikwazo sasa. Sasa, kukoma kutumika kwa raia kama ngao. Sasa.” Amesema Katib uMkuu

Tweet URL

Mgogoro unapanuka, chuki yaongezeka

Akizungumzia madhara mapana  ya mzozo huo, Guterres amesema kuna hatari ukasaa kutoka Lebanon na Syria, Iraq na Yemen. Ametoa wito kwa juhudi za kidiplmasia kushika kasi.

Kauli za chuki na vitendo vya chuki navyo ametaka vikome, akisema anachukizwa mno na ongezeko la chuki dhidi ya wayahudi halikadhalika chuki dhidi ya waislamu akisema kuwa jamii zote za wayahudi na waislamu katika kona mbali mbali za dunia zimekaa chonjo zikihofia usalama wao binafsi.

Kuomboleza vifo vya watumishi wa UNRWA

Katibu Mkuu ameungana pia na familia za wafanyakazi 89 wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA ambao wameuawa Gaza tangu kuanza kwa mapigano.

Idadi kubwa ya wafanyakazi hao – wakiwemo walimu, wakuu wa shule za msingi, madaktari , wahandisi, walinzi na wafanyakazi wa usaidizi waliuawa wao na familia zao.

Miongoni mwao ni kijana wa kike Mai, ambaye hakukubali ulemavu wake au kutumia kwake kitimwendo kumzuie kutimiza ndoto zake ya kuwa mwanafunzi bora na hatimaye kufanya kazi ya teknolojia ya habari UNRWA.

Akitamatisha hotuba yake, Katibu Mkuu ametoa wito kwa hatua za kimataifa ili kuondokana na ukatili na uharibifu pamoja na kusaka suluhu ya kuwa na mataifa mawili, Israel na PAlestina yakiishi pamoja.