Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimesikitishwa sana na athari za mafuriko Afrika Mashariki: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres
UN Photo/Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres

Nimesikitishwa sana na athari za mafuriko Afrika Mashariki: Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amesikitishwa sana kusikia mamia ya watu wameopoteza maisha na wengine wengi kuathiriwa na mafuriko makubwa katika nchi za Burundi, Kenya, Somalia na Tanzania na maeneo mengine ya Afrika Mashariki.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake jijini New York Marekani Guterres ametoa pole kwa Serikali na watu wa nchi zilizoathirika, hasa familia za waliofariki au kujeruhiwa katika maafa haya makubwa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Umoja wa Mataifa na washirika wake wanafanya kazi kwa karibu na mamlaka za kitaifa kushughulikia mahitaji ya kibinadamu. Katibu Mkuu anasisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kutoa msaada wa ziada katika kipindi hiki kigumu.

Pia Guterres amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya athari za hali mbaya ya hewa iliyosababishwa na El Niño, ambayo inahatarisha zaidi uharibifu wa jamii na kudhoofisha uwezo wa watu kuweza kuishi.