Heko Nkurunzinza kwa kutangaza kung’atuka 2020-UN

9 Agosti 2018

 Umoja wa Mataifa umekaribisha tangazo lililotolewa hii leo na Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi ya kwamba kipindi chake cha kuongoza nchi hiyo kitamalizika mwaka 2020 na kwamba atamuunga mkono mrithi wake.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Burundi Michel Kafando amesema hayo leo akihutubia Baraza la Usalama la umoja huo jijini New York, Marekani

Bwana Kafando amesema tangazo la katiba mpya ya Burundi na tangazo la Rais Nkurunzinza kuwa atakamilisha awamu yake mwaka 2020 ni mambo muhimu katika jitihada za kumaliza mzozo unaoendelea kwenye nchi hiyo ya Maziwa Makuu.

Amesema “katika jitihada zetu za kusaidia nchi hii ili hatimaye imalize mgogoro wake, hizi ni hatua mbili kubwa muhimu ambazo tunapaswa kuziangazia. Zinatupatia pia fursa ya kusonga mbele katika kuhitimisha hoja ya Burundi.”

Mjumbe huyo pia amesema hali ya usalama Burundi imekuwa tulivu na kwamba wakimbizi walioko nchi jirani wameendelea kurejea kwa hiari.

Wakimbiz wa Burundi katika kituo cha muda cha UN Makamba wakielekezwa kwa ajili ya warejea nyumbani. Picha: UNHCR (maktaba)
Wakimbiz wa Burundi katika kituo cha muda cha UN Makamba wakielekezwa kwa ajili ya warejea nyumbani. Picha: UNHCR (maktaba)

Halikadhalika viongozi waandamizi wa mashirika ya kimataifa wamekuwa wakitembelea nchi hiyo akisema ni ishara ya kwamba Burundi iko tayari kuboresha uhusiano wake na jamii ya kimataifa.

Bwana Kafando akazungumzia pia suala la ofisi ya  haki za binadamu ya kimataifa akisema kuwa “Natoa wito kwa serikali ya Burundi ikamilishe mjadala wa makubaliano ya maelewano na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo na hatimaye watie saini ili kuruhusu ofisi yangu mjiin Bujumbura iweze kufanya kazi katika mazingira bora zaidi.”

Burundi imekuwa kwenye mzozo tangu Rais Nkurunzinza aongeze muda wake wa uongozi kwa awamu ya tatu mwezi Aprili mwaka 2015.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter