Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wapatao 43 wauawa Sudan katika mapigano kati ya jeshi la serikali na RSF

Mvuana akitembea katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salaam Darfur Kaskazini
© WFP/Leni Kinzli
Mvuana akitembea katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salaam Darfur Kaskazini

Watu wapatao 43 wauawa Sudan katika mapigano kati ya jeshi la serikali na RSF

Haki za binadamu

Huko nchini Sudan jimboni Darfur Kaskazini, hususan mjini El-Fasher na viunga vyake mapigano kati ya jeshi la serikali SAF na wanamgambo wa RSF yanazidi kuwa na madhara kwa rai ana kumtia hofu kubwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kutokea Nairobi, Kenya, msemaji wa ofisi ya Kamishna wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Seif Magango amesema hali inazidi kuwa mbaya kwani katika kipindi cha wiki mbili zilizopita watu wapatao 43 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa kutokana na mapigano kati ya pande mbili hizo kinzani.

Makombora  yanarushwa kiholela

Yaripotiwa kuwa pande zote zinarusha makombora kwenye maeneo ya raia, wengine wakitumia ndege za kivita kwenye makazi ya watu mjini El- Fasher na viunga vyake.

“Mji wa El Fasher jimboni Darfur Kaskazini ndio mji pekee ambao bado unadhibitiwa na jeshi la Sudan,” amesema Bwana Magango akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa akiongeza kuwa “wasiwasi wa Kamishna Türk  ni kwamba mapigano haya yasipositishwa basi tunaweza kushuhudia kile kilichotendeka kwenye miji kama Geneina huko jimboni Darfur Kusini mwaka jana.”

Soundcloud

Bwana Magango amesema raia wamenasa mjini El-Fasher kwa hofu ya kuuawa iwapo watajaribu kukimbia. “Hali hii mbaya inaambatana na uhaba wa huduma za msingi kwani ufikishaji wa bidhaa za kuuza halikadhalika bidhaa za usaidizi wa kiugu unakwamisha na mapigano yanayoendelea na malori yenye shehena za misaada hayawezi kupitia kwenye maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa RSF.”

Mashambulizi yanalenga raia wenye asili ya kiafrika

Hofu zaidi ya Kamishna Türk ni suala kwamba wapiganaji wa RSF wanalenga vijiji vilivyoko magharibi mwa El-Fasher ambako wanaishi raia wa kiafria wa kabila la Zaghawa.

“Wapiganaji hao wameteketeza kwa moto vijiji vya Durma, Umoshosh, Sarafaya, na Ozbani. Mashambulizi ya aina hii yanaibua wigo  wa uwezekano wa ghasia zenye misingi ya kikabila huko Darfur ikiwemo mauaji ya watu wengi.” Amesema Bwana Magango.

Amekumbusha kuwa mapigano ya mwaka jana na mashambulizi kati ya kabila la Rizegait na Masalit wenye asili ya kiafrika huko jimboni Darfur Magharibi yalisababisha vifo vya mamia ya raia na wengine walijeruhiwa, huku maelfu walikimbia makazi yao.

Mapigano yakome, wahusika wafikishwe mbele ya sheria

Idhaa ya Umoja wa Mataifa ikamuuliza Bwana Magango sasa ni nini ambacho Kamishna Türk angelipenda kuona kinafanyika wakati huu licha ya kwamba yeye Türk mwenyewe na viongozi wengine wengi wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine wamekuwa wakitoa wito zaidi yam waka sasa kukomesha mapigano hayo, na ndipo akasema “kile ambacho tunafanya ni kuendelea kuelezea msimamo wetu kuwa mapigano haya yakiendelea hali inaweza kuwa mbaya zaidi.”

Amesema “anachotaka Kamishna Türk ni mapigano yakome na uchunguzi na zaidi ya yote haki itendeke kwa wale walioathiriwa na mapigano hayo na kwa washukiwa wa kutekeleza mauaji au vitendo hivyo wafikishwe mbele ya sheria ili ichukue mkondo wake.”

Mapigano nchini Sudan yalianza tarehe 15 mwezi Aprili mwaka 2023 kati ya jeshi la serikali, SAF na wanamgambo wa RSF kwenye mji mkuu, Khartoum.

RSF ni jeshi huru nchini Sudan, ambalo limechipuka kutoka wanamgambo wa Janjaweed waliokuwa zamani wameshika hatamu kwenye jimbo la Darfur nchini humo.