Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan: Baraza la Usalama la UN latiwa hofu na hali inayoendelea El Fasher

Watoto wakitembea kuelekea kituo cha wakimbizi wa ndani huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)
© UNICEF/Shehzad Noorani
Watoto wakitembea kuelekea kituo cha wakimbizi wa ndani huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan (Maktaba)

Sudan: Baraza la Usalama la UN latiwa hofu na hali inayoendelea El Fasher

Amani na Usalama

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao mkubwa kufuatia mvutano mkubwa na operesheni za kijeshi zinazoendelea huko El-Fasher jimboni Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Taarifa ya wajumbe hao iliyotolewa jumamosi jijini New York, Marekani inasema wasiwasi  huo mkubwa unatokana na mashambulizi ya dhahiri yanayofanywa huko El-Fasher na wapiganaji wa Rapid Support Forces au RSF na washirika wao dhidi ya mji huo ambao ni hifadhi ya mamia ya maelfu ya raia waliokimbia mashambulizi kwingineko.

Wanatoa wito kwa jeshi la serikali nchini Sudan, SAF na RSF kuacha kuimarisha vikosi vyao na badala yake wachukue hatua kupunguza mapigano na kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kiutu.

Wajumbe hao wa Baraza wamerejelea wito wao wa kutaka sitisho la chuki, hatua ambayo itafanikisha sitisho endelevu la mapigano katika mji huo ambao ndio uliosalia kuwa chini ya udhibiti wa jeshi la serikali ya Sudan.

“Wajumbe wamesihi nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa ziache aina yoyote ya kuingilia mgogoro huo ili kuepuka kuuchochea zaidi na badala yake ziunge mkono juhudi za kusaka amani ya kudumu,” imesema taarifa hiyo.

Wajumbe pia wamekumbusha pande zote kwenye mzozo zizingatie mikakati ya vikwazo vya silaha kama ilivyoelezwa kwenye azimio namba 1556  la mwaka 2004 lililopatiwa msisitizo na azimio namba 2676 la mwaka 2023.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, OHCHR iliripoti Ijumaa ya kwamba huko jimboni Darfur Kaskazini, hususan mjini El-Fasher na viunga vyake mapigano kati ya jeshi la serikali SAF na wanamgambo wa RSF yanazidi kuwa na madhara kwa raia na kumtia hofu kubwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk. 

OHCHR imesema hali inazidi kuwa mbaya kwani katika kipindi cha wiki mbili zilizopita watu wapatao 43 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa kutokana na mapigano kati ya pande mbili hizo kinzani.