Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HABARI KWA UFUPI: Miaka miwili ya Taliban-Afghanistan na miezi minne ya vita Sudan

Maisha ya wanawake na wasichana yamepinduliwa tangu kurejeshwa kwa vuguvugu la Taliban madarakani katika msimu wa kiangazi  uliopita mwaka 2021
Sayed Habib Bidel/UNWomen
Maisha ya wanawake na wasichana yamepinduliwa tangu kurejeshwa kwa vuguvugu la Taliban madarakani katika msimu wa kiangazi uliopita mwaka 2021

HABARI KWA UFUPI: Miaka miwili ya Taliban-Afghanistan na miezi minne ya vita Sudan

Haki za binadamu

Ikiwa leo tarehe 15 Agosti ni miaka miwili tangu kundi la Taliban lilipotwaa mamlaka kimabavu nchini Afghanistan, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amewakumbusha Talibani kwamba Afghanistan, kama Taifa, ina wajibu chini ya sheria za kimataifa kuheshimu, kudumisha na kukuza haki za watu wote bila ubaguzi. Naye Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake (UN Women) Sima Bahous amesema hali ya unyanyasaji wa wanawake nchini Afghanistan haikubaliki na inapaswa kukoma.  

#AfghanGirlsVoices - ECW 

Wasichana wadogo wanasoma katika shule inayofadhiliwa na UNICEF katika Mkoa wa Paktika, Afghanistan.
© UNICEF/Sayed Bidel

Mfuko wa kimatifa wa Umoja wa Mataifa wa elimu haiwezi kusubiri (ECW) kwa ajili ya elimu katika dharura na migogoro ya muda mrefu umezindua kampeni ya #AfghanGirlsVoices yaani sauti za wasichana wa Afghanistan ili kuinua hadi hatua ya kimataifa sauti za wasichana wadogo wa Afghanistan walionyimwa haki yao ya msingi ya elimu na kujifunza. Kampeni ya #AfghanGirlsVoices ina mkusanyiko wa nukuu za wasichana wa Afghanistan na vielelezo asili vya sanaa. ECW inawaalika wadau na umma kwa ujumla kusimama katika mshikamano na wasichana wa Afghanistan kwa kusambaza sauti za wasichana hawa kwenye mitandao ya kijamii kila siku - kuanzia leo tarehe 15 Agosti, tarehe ambayo Taliban iliingia madarakani mwaka 2021, hadi tarehe 18 Septemba, ambapo miaka miwili iliyopita Talban watangaza rasmi marufuku kwa wasichana balehe kuhudhuria shule nchini humo. 

SUDAN 

Wakimbizi kutoka Sudan wakiwasili katika kambi ya muda nchini Chad.
© UNHCR/Jutta Seidel

Na baada ya miezi minne ya vita nchini Sudan, viongozi wa takribani mashirika 12 (OCHA, FAO, IOM, OHCHR, UNDP, UNFPA, UNHCR, UN-Habitat, UNICEF, UN Women, WFP,  WHO) ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na wadau wao wanaohudumu nchini Sudan wametoa wito wa pamoja kukomeshwa mara moja kwa uhasama. Viongozi hao wamesema watu wa Sudan wanahitaji amani na upatikanaji wa usawa wa misaada ya kibinadamu. Na jumuiya ya kimataifa lazima ijitokeze leo, ishiriki katika ngazi zote, na kuchukua hatua ya kuirejesha Sudan kwenye mstari na kumaliza vita.