Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya #AfghanGirlsVoices yazinduliwa kupaza sauti za wasichana wa Afghanistan

Wasichana wadogo wakisoma katika shule huko Mazar-i-Sharīf, Mkoa wa Balkh, Afghanistan.
© UNICEF/Mark Naftalin
Wasichana wadogo wakisoma katika shule huko Mazar-i-Sharīf, Mkoa wa Balkh, Afghanistan.

Kampeni ya #AfghanGirlsVoices yazinduliwa kupaza sauti za wasichana wa Afghanistan

Utamaduni na Elimu

Mfuko wa kimatifa wa Umoja wa Mataifa wa elimu haiwezi kusubiri (ECW) kwa ajili ya elimu katika dharura na migogoro ya muda mrefu umezindua kampeni ya #AfghanGirlsVoices yaani sauti za wasichana wa Afghanistan ili kuinua hadi hatua ya kimataifa sauti za wasichana wadogo wa Afghanistan walionyimwa haki yao ya msingi ya elimu na kujifunza.  

Kampeni hiyo imetayarishwa kwa ushirikiano na Bingwa wa ECW Somaya Faruqi, Kapteni wa zamani wa Timu ya Roboti ya Wasichana ya Afghanistan, na picha za kusisimua za msanii mdogo wa kike wa Afghanistan. Inaangazia mfululizo wa ushuhuda wenye msukumo sawa, wenye kuumiza moyo na uliodhamiriwa kutoka kwa wasichana wa Afghanistan ambao maisha yao yamepunguzwa ghafla na marufuku inayowazuia kufuata elimu na ndoto zao. Maneno yao yenye nguvu yanawasilishwa pamoja na vielelezo vya kuvutia vinavyoonesha hali ya kukata tamaa sana waliyopata wasichana hawa na wanawake wachanga wa Afghanistan pamoja na uthabiti wao wa ajabu na nguvu zao mbele ya marufuku hii isiyokubalika ya elimu yao. 

"Ujasiri wa wasichana hawa nchini Afghanistan hunipa nguvu ya kutumia sauti yangu kama Bingwa wa Kimataifa wa ECW ili kukuza sauti zao kwa ulimwengu. Pia inanitia moyo katika masomo yangu ya uhandisi kwa sababu najua thamani ya fursa ya elimu niliyonayo, ambayo wananyimwa,” anasema Somaya Faruqi na kuongeza kwamba, "Hali hiyo inaathiri sana afya ya akili ya wasichana na viwango vya kujiua kwa wasichana vimepanda katika miaka miwili iliyopita. Ni jambo la dharura zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuchukua hatua sasa, na ninatumai kwamba mwaka ujao, tutasherehekea uhuru wao badala ya kuashiria ukandamizaji wao. Mengi yanaweza kubadilika na kuwa bora katika mwaka mmoja ikiwa tutachukua hatua pamoja sasa, kwa mshikamano na kila msichana wa Afghanistan.”  

Hali ya wanawake na wasichana nchini Afghanistan ndiyo ‘mbaya zaidi duniani’, kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa. Vikwazo vya utaratibu wa haki za binadamu za wasichana na wanawake, na ubaguzi mkali wanaoupata chini ya utawala wa kweli wa mamlaka ya Taliban inaweza kuwa "ubaguzi wa kijinsia" na "unyanyasaji wa kijinsia", inasema ripoti hiyo. 

"Jumuiya ya kimataifa lazima isikie wito huu wa kuhuzunisha kutoka moyoni kutoka kwa wasichana na wanawake vijana wa Afghanistan na kuhamasishwa kwa wingi na kwa nguvu mpya ya makusudi kulaani ukiukwaji wa haki zao," aanasema Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Elimu Duniani na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la ECW - Kikundi cha Uendeshaji cha Ngazi ya Juu, Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Gordon Brown.  

Brown anaongeza akisema, "Mifumo inayotumika ya kisheria ya kimataifa inapaswa kutumika kutafuta hatua za kisheria na kuwawajibisha wale waliohusika na kutengwa huku kwa wanawake na wasichana kutoka elimu ya sekondari na ya juu. Aidha, jumuiya ya kimataifa inapaswa kupanua mara moja msaada kwa kozi za mtandaoni na redio, pamoja na kuongeza rasilimali za fedha kwa ajili ya Elimu ya Cannot Wait na washirika wake nchini Afghanistan ili kuongeza utoaji wao wa fursa za elimu kwa wasichana wa Afghanistan ndani na nje ya nchi, hasa nchini Afghanistan. Pakistan ambako familia nyingi za Afghanistan zimekaa.”  

Kampeni ya #AfghanGirlsVoices ina mkusanyiko wa nukuu za wasichana wa Afghanistan na vielelezo asili vya sanaa. ECW inawaalika wadau na umma kwa ujumla kusimama katika mshikamano na wasichana wa Afghanistan kwa kusambaza sauti za wasichana hawa kwenye mitandao ya kijamii kila siku - kuanzia leo tarehe 15 Agosti, tarehe ambayo Taliban iliingia madarakani mwaka 2021, hadi tarehe 18 Septemba, ambapo miaka miwili iliyopita Talban watangaza rasmi marufuku kwa wasichana balehe kuhudhuria shule nchini humo. 

Ujio wa kampeni hii wakati huu utainua sauti za wasichana wa Afghanistan katika jukwaa la kimataifa wakati viongozi wa dunia watakapokutana kwenye Mkutano wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) tarehe 18-19 Septemba katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York. Mkutano huo unalenga kuashiria mwanzo wa awamu mpya ya maendeleo ya kasi kuelekea SDGs yenye mwongozo wa hali ya juu wa kisiasa kuhusu hatua za kuleta mabadiliko na za kasi kuelekea 2030 - maendeleo ambayo hayawezi kufikiwa na wasichana wa Afghanistan walioachwa nyuma. 

"Wakati dunia inaadhimisha nusu ya mwisho iliyowekwa ya kufikia Ajenda ya 2030 na SDGs, lazima tusiwasahau wale ambao wameachwa nyuma zaidi. Ni vigumu kufikiria mtu yeyote aliyeachwa nyuma zaidi kuliko wasichana nchini Afghanistan ambao wananyimwa haki zao za kimsingi za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na haki yao ya kupata elimu, kwa kuzingatia jinsia zao pekee,” Mkurugenzi Mtendaji wa ECW Yasmine Sherif amesema akiongeza, "ECW imejitolea kwa dhati kuinua na kuwezesha sauti za wasichana wa Afghanistan. Tutaendelea kutetea kwa uthabiti kurejeshwa kikamilifu kwa haki yao ya elimu nchini Afghanistan, na kufanya kazi na washirika wetu kutoa fursa muhimu za kujifunza kwa watoto wa Afghanistan kupitia programu za elimu za kijamii tunazounga mkono." Sherif anasema. 

Bonyeza hapa ili kufikia vipeperushi zaidi vya kampeni hii #AfghanGirlsVoices kwa ajili ya mitandao ya kijamii.