Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya Afrika katika UN yaanza leo New York, Elimu kumulikwa

Msaidizi wa Katibu Mkuu na MShauri Maalum kuhusu Afrika, Cristina Duarte, akizungumza na waandishi wa habari jijini New York kuhusu Mazungumzo kuhusu Afrika au ADS2024
UN Photo/Manuel Elías
Msaidizi wa Katibu Mkuu na MShauri Maalum kuhusu Afrika, Cristina Duarte, akizungumza na waandishi wa habari jijini New York kuhusu Mazungumzo kuhusu Afrika au ADS2024

Mazungumzo ya Afrika katika UN yaanza leo New York, Elimu kumulikwa

Utamaduni na Elimu

Hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani vimeanza vikao vya wiki tatu kuhusu Mazungumzo kuhusu Afrika au ADS2024 maudhui yakiwa Elimu kupitia Sayansi, Teknolojia na Ugunduzi kuelekea Afrika Tuitakayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Msaidizi wa Katibu Mkuu na MShauri Maalum kuhusu Afrika, Cristina Duarte amesema mwaka huu vikao hivyo vinalenga kuhamasisha hatua na kuchochea majawabu yakitumia sayansi, teknolojia na ugunduzi ili hatimae Afrika iwe na elimu bora.

Nchi za Afrika zipatie kipaumbele elimu

“Huu kimsingi ni wito wa dhati wa kuchukua hatua,” amesema Balozi Fatima Kyari Mohammed, Mwakilishi wa Muungano wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa wakati akizungumza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.

Amesema  wito ni kwa nchi za Afrika kwenye Umoja wa Mataifa kupatia kipaumbele elimu kama msingi wa kusonga mbele na maendeleo. “Mpango huu unasisitiza umuhimu wa kujenga mifumo ya elimu inayoleta mabadiliko na yenye mnepo ambayo sio tu inaweza kufikiwa na watoto bali pia ni jumuishi, bora na inaendana na nyakati za sasa.”

Akiwasilisha Mada ya kwanza ya ADS204 ikipatiwa jina Elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM kwa ajili ya mapinduzi ya Nne ya Viwanda, 4IR, Afrika,  ikijikita katika Kuchochea ajira zenye hadhi kwa vijana wa Afrika, Bi. Duarte amesema changamoto kubwa ni kuunda ajira zenye hadi Afrika.

“Asilimia 95 ya idadi ya watu Afrika ni vijana – hawana ajira za hadhi, ikimaanisha kwamba wakati mwingine kuwa na ajira barani Afrika si mbinu ya kukuwezesha kuondokana na umaskini,” amesema Bi. Duarte.

Balozi Fatima Kyari Mohammed, Mwakilishi wa Muungano wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa wakati akizungumza kwenye mkutano  na waandishi wa habari kuhusu mazungumzo ya Afrika kwenye UN .
UN /Manuel Elias

Teknolojia na ugunduzi ni muarobaini wa elimu Afrika

Kuhusu ufadhili kwenye ugunduzi ili kuleta mabadiliko kwenye elimu, Mkuu huyo wa OSAA amesema “tuna zaidi ya watoto milioni 100 wasio shuleni. Tunaweza kukuhakikishai kwamba mfumo wa zamani wa ufadhili hauwezi kutatua shida hii.”

Amesema watu milioni 100 wasio shuleni na bila fursa ya kupata fedha. “Kwa hiyo elimu inataka ufadhili bunifu ukipatia TEHAMA kipaumbele ili kushughulikia sual hili.”

Kuhusu elimu na kujifunza kwenye maeneo yenye majanga, Bi. Duarte amesema “ukosefu wa utulivu unaendelea kuongezeka, , mizozo halikadhalika, na tunahitaji katika utungaji sera na mfumo wa msimamo wa Umoja wa Mataifa , kujadili jinsi ya kutatua ukosefu wa utulivu kwenye mizozo bila kusitisha elimu, ikimaanisha bila kufunga shule.”

ADS 2024 iliyoanza leo Mei, 6, tafunga pazia tarehe 30 Mei 2024.