Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usalama Ukanda wa Sahel wafurusha watoto; Shule zilizofungwa zaongezeka maradufu

Zaidi ya watu 35,000 wakiwa kwenye makazi yasiyo rasmi ya wakibizi huko Cameroon, baada ya kukimbia ghasia za Boko Haram. Ghasia hizi zinasababisha watoto washindwe kwenda shuleni.
UN/Eskinder Debebe
Zaidi ya watu 35,000 wakiwa kwenye makazi yasiyo rasmi ya wakibizi huko Cameroon, baada ya kukimbia ghasia za Boko Haram. Ghasia hizi zinasababisha watoto washindwe kwenda shuleni.

Ukosefu wa usalama Ukanda wa Sahel wafurusha watoto; Shule zilizofungwa zaongezeka maradufu

Utamaduni na Elimu

Kuendelea kwa ukosefu wa usalama kwenye ukanda wa Sahel kumesababisha takribani shule 2000 huko Burkina Faso, Mali na  Niger kufungwa kabisa au kushindwa kutoa elimu kwa wanafunzi mwaka 2018.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema hayo kupitia taarifa yake iliyotlewa Dakar Senegal na New York, Marekani ikitanabaisha kuwa idadi hiyo ya shule zilizofungwa ni ongezeko maradufu ikilinganishwa na mwaka 2017.

UNICEF inasema kufungwa kwa shule hizo kumesababisha watoto zaidi ya 400,000 washindwe kwenda shule, walimu zaidi ya 10,000 washindwe kufanya kazi, na inatokana na vitisho dhidi ya walimu, mashambulizi dhidi ya shule na wakati mwingine shule kutumiwa kwa shughuli za kijeshi, vitendo ambavyo UNICEF imesema ni ukiukwaji mkubwa wa haki za mtoto.

Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema pindi watoto wanaposhindwa kwenda shuleni hususan wakati wa mzozo, siyo tu wanashindwa kupata stadi mpya wanazohitaji kwa ajili ya ujenzi wa jamii zao, bali pia wanakuwa hatarini kutumikishwa kwenye vikundi vilivyojihami na pia kunyanyaswa kingono.

Bi. Fore amesema  wakati huu ambapo ukanda wa Sahel unakabiliwa na vitisho zaidi vya ghasia “hatupaswi kusahau kuwa elimu ni haki yam toto na chombo thabiti cha amani.”

Umoja wa Mataifa unataka mataifa hayo matatu kuzingatia azimio ambalo wametia saini la mazingira salama shuleni ambapo nchi hizo tatu Burkina Faso, Mali na Niger zilishatia saini zikiahidi kulinda na kuhakikisha elimu inaendelea hata kwenya meneo ya mzozo.

Mathalani Burkina Faso imeridhia mkakati mpya wa ulinzi na elimu kwenye maeneo ya mzozo ambapo inaandaa mtaala wa kusaidia watoto wasio shuleni kuweza kwenda sambamba na wenzao walio shuleni.

Halikadhalika kuimarisha usalama shuleni na ukarabati au  ujenzi mpya wa shule zilizoharibiwa.

UNICEF kwa upande wake imesema imeazimia kushirikiana na mamlaka za shule na jamii kusaidia mbinu mbadala za mafunzo kwa watoto ikiwemo elimu kwa njia ya redio na pia kwenye maeneo ya mafunzo ya dini ili watoto wasikose elimu.