Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na AU wazingatie vipaumbele ili kufikia malengo tuliyojiwekea- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mjadala wa ubia kati ya Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani
UN /Loey Felipe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza katika mjadala wa ubia kati ya Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani

UN na AU wazingatie vipaumbele ili kufikia malengo tuliyojiwekea- Guterres

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa umesema bado una imani na uongozi wa Afrika katika kutatua matatizo ya bara hilo na kwamba Umoja wa Mataifa una nia ya dhati kutumia fursa zilizopo sasa kufanya kazi kwa karibu zaidi na Muungano wa Afrika, AU.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema hay oleo wakati akihutubia kikao cha ufunguzi wa msururu wa mijadala ya Afrika ulioanza leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Mjadala huo una lengo la kuimarisha ubia kati ya pande mbili hizo ambapo  Guterres amesema, sera na mikakati ya AU na ile ya UN hivi sasa vinalandana zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Amegusia ajenda ya 2030 ya UN na ile ya 2063 ya AU akisema vinaendana na hivyo kila nchi ya Afrika inapaswa kufikia ahadi ambapo vyombo hivyo viwili viliwekeana wakati wa mkutano uliofanyika Addis Ababa.

Guterres pia amesema uchumi wa kiafrika unaonesha uimara na ukuaji na kwamba kiwango cha ukuaji kinaakisi hali ya utulivu mkubwa na jitihada za kuboresha utawala.

Akigusia mageuzi Guterres amesema, "wakati Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wakifanya mageuzi, ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote kuhakikisha kwamba tunazingatia vipaumbele vyetu, kukubaliana juu ya maeneo yetu ya wajibu, na kuimarisha ushirikiano wetu."

Naye Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa María Fernanda Espinosa amebainisha mchango muhimu wa wanawake na vijana kwa maendeleo ya bara la Afrika akisema kuwa “uwekezaji na kuongeza fursa za kupata elimu na kazi nzuri ni muhimu. Kupunguza kutokuwepo kwa usawa na ni muhimu kuijenga jamii imara na yenye amani. Tunatakiwa kuwekeza kwa vijana”

 Mkutano huu umeandaliwa na Ofisi ya mshauri  wa masuala ya Afrika kwenye Umoja wa  Mataifa, OSAA na utamalizika tarehe 18 mwezi huu wa Oktoba.