Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Mashambulizi Goma yaua raia 12, UN yalaani

Watu waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro wanaishi katika kambi ya muda karibu na Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© WFP/Benjamin Anguandia
Watu waliokimbia makazi yao kutokana na migogoro wanaishi katika kambi ya muda karibu na Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

DRC: Mashambulizi Goma yaua raia 12, UN yalaani

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Bintou Keita amelaani vikali shambulio la leo la mabomu dhidi ya makazi mawili ya kuhifadhi wakimbizi wa ndani huko Lac-Vert na Mugunga takribani kilometa 13 hadi 15 kutoka Goma mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Taarifa iliyotolewa leo Kinshasa, mji mkuu wa DRC na ofisi ya Bintou Keita ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO imesema mashambulio hayo yaliyofanywa na waasi wa M23 yamesababisha vifo vya watu 12 wakiwemo watoto 6 huku na watu wengine 31 wamejeruhiwa.

Bi. Keita ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Mkuu huyo wa MONUSCO pia amelaani kuendelea kuimarika kwa mashambulizi dhidi ya raia huko jimboni Kivu Kaskazini na kukukumbusha pande zote husika kuzingatia wajibu wao kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, na wakati huo huo walinde raia katika mazingira yoyote.

Hali ya usalama imekuwa tete Goma

Msemaji wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo amesema kuwa katika wiki kadhaa zilizopita, hali ya usalama kwenye mji wa Goma, imekuwa tete na kwamba mwezi Februari na Machi, wahudumu wa kiutu wameripoti matukio 10 ya milipuko iliyosababisha vifo vya wtu 14 na wengine 28 walijeruhiwa. Na mwezi uliopita wa Aprili, mlipuko karibu na makazi ya wakimbizi wa ndani ulisababisha vifo vya watu 5.

Mvulana akiwa ameketi katika moja ya makazi ya wakimbizi wa ndani Goma jimbo la Kivu Kaskazini
© UNICEF/Jospin Benekire
Mvulana akiwa ameketi katika moja ya makazi ya wakimbizi wa ndani Goma jimbo la Kivu Kaskazini

Bi. Keita ametaka mamlaka za DRC zichukue hatua zote zinazowezekana kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wote wa mashambulizi haya ambayo yanakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu na za kibinadamu, vitendo ambavyo vinaweza kuwa uhalifu wa kivita.

“Ametaka pia pande zote kwenye mzozo mashariki mwa DRC ziwapatie raia waliofurushwa makwao hakikisho la usalama na vile vile misaada ya kibinadamu iweze kuwafikia,” amenukuliwa Bi. Keita kwenye taarifa hiyo.

Makundi yaliyojihami yajisalimishe

Halikadhalika amerejelea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutaka vikundi vyote vilivyojihami Mashariki mwa DRC kuweka silaha zao chini mara moja na kuungana na mradi unaotekelezwa na serikali na MONUSCO wa vikundi hivyo kusalimisha silaha, kuvunja makundi na kujiunga kwenye jamii na kuweka utulivu, au (P-DDRCS).

Amesisitiza azma ya dhati na isiyotetereka ya MONUSCO ya kusaidia juhudi zote za kujenga amani, usalama na utulivu DRC, “na natoa wito kwa pande husika zifanye kazi kwa dhati kumaliza ghasia na kufanikisha kupatikana kwa suluhu la kudumu la mzozo nchini humo.”