Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano mapya yameibuka jana kati ya M23 na FARDC

Makamanda wa vikosi vya jeshi la Congo, FARDC katika Ziara ya Kiutendaji Kainama, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
UN Photo/Michael Ali
Makamanda wa vikosi vya jeshi la Congo, FARDC katika Ziara ya Kiutendaji Kainama, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Mapigano mapya yameibuka jana kati ya M23 na FARDC

Amani na Usalama

Baada ya utulivu wa muda mfupi wa ghasia, jana kumetokea mapigano mapya na makali kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa DRC, magharibi mwa mji wa Sake huko Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi, umeeleza Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza na waandishi wa Habari jijini New York leo kueleza taarifa alizozipata kutoka MONUSCO, ameeleza kwamba wakati wa mapigano, roketi mbili zilitua karibu na kituo cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Kimoka - kama kilomita 4 kaskazini magharibi mwa Sake. Hakuna majeruhi katika upande wa Umoja wa Mataifa walioripotiwa.

MONUSCO ina wasiwasi mkubwa kutokana na uhasama mashariki mwa Congo na inasisitiza wito wake kwa M23 kuacha mashambulizi yake na kuheshimu makubaliano ya Luanda, Angola.

Msemaji huyo wa Katibu Mkuu ameeleza, “MONUSCO licha ya kutuhumiwa na kulengwa mara kwa mara inaendelea na juhudi zake za ulinzi katika jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na kudumisha misimamo ya kutetea raia huko Sake na Goma.”