Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Napenda mambo yanayonipa changamoto: Sintyashi mnufaika wa mafunzo ya MONUSCO

Sintyashi Kyaula, mnufaika wa mradi wa MONUSCO wa kupunguza ghasia kwenye jamii huko Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
UN News
Sintyashi Kyaula, mnufaika wa mradi wa MONUSCO wa kupunguza ghasia kwenye jamii huko Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Napenda mambo yanayonipa changamoto: Sintyashi mnufaika wa mafunzo ya MONUSCO

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Umoja wa Mataifa kupitia ujumbe wake wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO unaendelea kutekeleza jukumu lake la kuimarisha amani kwa kupatia vijana stadi za kuwawezesha kujiinua kiuchumi kupitia mradi wa kupungua ghasia kwenye jamii, CVR.

Mathalani hivi karibuni MONUSCO kupitia CVR, ilipatia mafunzo vijana 40 wa kike na wa kiume, wakiwemo ambao wako hatarini kutumikishwa vitani, waliotumikishwa vitani au wanaohitaji stadi zaidi ili kujikwamua kiuchumi.

Mafunzo  ya miezi Sita yamwezesha kutengeneza simu janja

Miongoni mwao ni msichana Sintyashi Kyaula, mkazi wa mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini ambaye ni mhitimu wa masomo ya elektroniki.

Sintyashi akizungumza na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa akiwa kwenye kioski chake cha kutengeneza simu janja na za kawaida, anasema anafurahia kazi yake kwa kuwa anapenda sana masuala ya elektroniki.

Aliulizwa ni kwa vipi anapenda masomo hayo ikiwemo hisabati ilhali watoto wa kike hawapendi masomo hayo, wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia watoto duniani, UNICEF linasema ukosefu wa fursa ndio chanzo, Sintyashi anasema, “mimi napenda kitu ambacho kinanipatia changamoto kubwa. Najikisia kujivunia sana nikifanya kitu kama hicho.”

Baada ya mafunzo walipatiwa vifaa na uwezo wa kufungua kioski

MONUSCO ilitoa mafunzo hayo kwa miezi sita mjini Goma, ambapo baada ya mafunzo, Sintyashi na wanufaika wengine walipatiwa vifaa kama vile paneli ya sola, mashine za kubaini hitilafu kwenye simu janja, vifaa vya kufungulia simu na fedha kidogo za kuwezesha kufungua kioski.

“Mafunzo haya yamenisaidia sana kwa sababu nimefungua hiki kioski na wateja wanaleta simu zao. Wateja wanafurahia sana huduma yangu,” anafafanua Sintyashi huku akiwa anatengeneza moja ya simu iliyoletwa na mteja wake.

Katika kioski chake, Sintyashi anaonekana akiwa anafungua simu moja janja tayari kutumia kifaa maalum cha kubaini tatizo liko wapi. Misumari inaonekana imesambaa lakini alipoulizwa anakumbuka vipi ili aweze kufunga vizuri, Sintyashi anasema, “hapa nimeipanga na nafahamu upi uende wapi.”

Sasa najihudumia tofauti na awali

Alipoulizwa anaona tofauti yoyote kabla na baaada ya mafunzo? Sintyashi anasema, “kabisa! Kuna tofauti kubwa. Hivi sasa naweza kujihudumia mwenyewe tofauti na zamani.”

Ujumbe kwa vijana, na shukrani kwa  MONUSCO na UN

Na vipi kuhusu vijana wengine ambao bado wanarandaranda mitaani bila kazi ya kufanya? Sintyashi ana ujumbe gani?

“Nawaambia waache kufanya hivyo, wasikate tu, wajiunge nasi wafanye kazi za mikono kwa kuwa zina faida sana.”

Sintyashi hakuwa mnyimi wa shukrani kwa MONUSCO akisema, “asante sana, ikiwezekana watusaidie tena kwa kuwa bado kuna changamoto nyingi. Nashukuru pia Umoja wa Mataifa, nawashukuru sana. Nafurahi sana kwa ujio wenu, nafurahi sana walitupatia mafunzo, sote tuko vizuri na hakuna anayeteseka tena.”

Mradi wa MONUSCO CVR

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, miradi ya CVR ilianzishwa na MONUSCO mwaka 2017 ikilenga kusaidia kusongesha amani kupitia miradi kama vile kupatia jamii mbinu za kujipatia kipato, ujenzi wa miundombinu, stadi za kiufundi, kuzuia ukatili wa kijinsia, ulinzi wa watoto, waliotumikisha vitani na vijana walio hatarini