Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakati watu milioni 783 wakilala njaa, moja ya tano ya chakula chote kinaishia jalalani: UNEP

Moja ya tano ya chakula chote kinaishia jalalani
FAO/Giulio Napolitano
Moja ya tano ya chakula chote kinaishia jalalani

Wakati watu milioni 783 wakilala njaa, moja ya tano ya chakula chote kinaishia jalalani: UNEP

Tabianchi na mazingira

Wakati theluthi moja ya wanadamu wanakabiliwa na uhaba  mkubwa wa chakula, duniani sawa na milo bilioni moja inapotea kila siku, imesema leo ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP  ni moja ya tano ya chakula hutupwa na kuishia jalalani.

Ripoti ya UNEP ambayo ni ya “Kielelezo cha Taka za Chakula 2024” inaangazia takwimu za hivi karibuni kuanzia mwaka 2022 ambazo zinaonyesha kuwa tani bilioni 1.05 za chakula zilipotea.

Asilimia 19 ya chakula ambacho kipo kwa ajili ya watumiaji kilipotea kwa jumla katika maduka ya rejareja, sekta ya huduma ya chakula na viwango vya kaya.

Hiyo ni pamoja na karibu asilimia 13 ya chakula kilichopotea katika mnyororo wa usambazaji, kama inavyokadiriwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, kuanzia tu baada ya mavuno hadi katika hatua ya kuuzwa.

Janga la kimataifa 

“Upotevu wa chakula ni janga la kimataifa. Mamilioni ya watu watakuwa na njaa leo huku chakula kikiharibika kote duniani,” amesema Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, akieleza kuwa suala hili linaloendelea sio tu linaathiri uchumi wa dunia lakini pia linazidisha mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa bayoanuwai na uchafuzi wa mazingira.

Ripoti hiyo ya UNEP inasema takataka nyingi za chakula duniani zinatokana na kaya, jumla ya tani milioni 631 au hadi asilimia 60 ya jumla ya chakula kilichotuwa. Sekta ya huduma ya chakula na biashara ya rejareja iliwajibika kwa tani milioni 290 na milioni 131 milioni.

Kwa mujibu wa waandishi wa ripoti kwa wastani, kila mtu hupoteza kilo 79 za chakula kila mwaka. Hii ni sawa na milo 1.3 kila siku kwa kila mtu ulimwenguni aliyeathiriwa na njaa.

Sio tatizo la nchi tajiri pekee

Tatizo haliko katika mataifa tajiri pekee. Kufuatia kuongezeka maradufu kwa matumizi ya takwimu tangu Ripoti iliyochapishwa ya Fahirisi ya Taka za Chakula ya 2021 kumekuwa na ongezeko la muunganiko kati ya matajiri na maskini.

Nchi za kipato cha juu, kipato cha juu-kati, na nchi za kipato cha chini hutofautiana katika viwango vya wastani vya taka za chakula cha kaya kwa kilo saba tu kwa kila mtu kwa mwaka.

Mgawanyiko mkubwa unakuja katika tofauti kati ya wakazi wa mijini na vijijini. Ripoti inasema katika nchi za kipato cha kati, kwa mfano, maeneo ya vijijini kwa ujumla yanapoteza kidogo. 

Ufafanuzi mmoja unaowezekana ni katika kuchakata tena mabaki ya chakula cha wanyama, chakula cha mifugo, na kutengeneza mboji nyumbani katika maeneo ya vijijini.

Ripoti inapendekeza kuangazia juhudi madhubuti katika kuimarisha upunguzaji wa taka za chakula na kutengeneza mboji mijini.

Utupaji chakula na mabadiliko ya tabianchi 

Ripoti inasema kuna uwiano wa moja kwa moja kati ya viwango vya joto vya wastani na viwango vya taka za chakula.

Nchi zenye joto zaidi zinaonekana kuwa na taka nyingi zaidi za chakula kwa kila mtu katika kaya, kutokana na uwezekano wa kuwa na  ongezeko la matumizi ya vyakula vilivyo na sehemu chache za kuliwa na ukosefu wa majokofu na suluhu za kuhifadhi chakula hicho.

Hali ya juu ya msimu wa joto, matukio ya joto kali na ukame hufanya iwe vigumu zaidi kuhifadhi, kuchakata, kusafirisha na kuuza chakula kwa usalama, na mara nyingi husababisha kiasi kikubwa cha chakula kuharibika au kupotea.

Mtaalamu wa UNEPanasema anaamini kuwa “Kwa kuwa upotevu wa chakula na taka huzalisha hadi asilimia 10 ya uzalishaji wa gesi chafuzi duniani karibu mara tano ya jumla ya uzalishaji ikilinganishwa na sekta ya anga kupunguza uzalishaji wa uchafuzi wa chakula ni muhimu.” 

Chakula kwa ajili ya matumaini

Kuna nafasi ya matumaini, ripoti inapendekeza kuwepo ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi ili kupunguza upotevu wa chakula na athari kwa mabadiliko ya tabianchi na shinikizo la maji na mapendekezo yanakumbatiwa na idadi inayoongezeka ya serikali za ngazi zote.

Mifano ni pamoja na Japan na Uingereza ambao wana punguzo la asilimia 18 na asilimia 31 zikionyesha kuwa mabadiliko katika viwango vya utupaji chakula yanawezekana, ikiwa chakula kitagawiwa ipasavyo.

Ripoti hiyo iliyochapishwa kabla ya Siku ya Kimataifa ya kutotupa taka inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 30 Machi mwaka huu ikibeba kichwa  Ripoti “Tathimini ya uchafuzi wa taka za Chakula”, imeandaliwa kwa ushirikiano na WRAP, NGO ya Uingereza inayoshughulikia masuala ya tabianchi.

Ripoti inatoa makadirio sahihi zaidi ya kimataifa kuhusu upotevu wa chakula katika viwango vya reja reja na kwa walajii, huku ikitoa mwongozo kwa nchi kuhusu kuboresha ukusanyaji wa data na mbinu bora, kulingana na Lengo la Maendeleo Endelevu la 12.3 la kupunguza nusu ya upotevu wa chakula ifikapo mwaka 2030.