Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwawezesha vijana kwa elimu, mafunzo na ujuzi ni muhimu kwa mustakbali wetu:Guterres

Viki Bokanda, ingawa ni mvulana mwenye umri wa miaka 15 anajifunza  ushoni kwenye kituo cha mafunzo stadi kwa wasichana  huko Kisangani, Kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
© UNICEF/UN0507530/Frank Dejongh
Viki Bokanda, ingawa ni mvulana mwenye umri wa miaka 15 anajifunza ushoni kwenye kituo cha mafunzo stadi kwa wasichana huko Kisangani, Kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Kuwawezesha vijana kwa elimu, mafunzo na ujuzi ni muhimu kwa mustakbali wetu:Guterres

Utamaduni na Elimu

Leo ni siku ujuzi kwa vijana duniani kaulimbiu mwaka huu ikiwa “Kuwapa ujuzi waalimu, wakufunzi na vijana kwa ajili ya mustakbali wenye mabadiliko”.

Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika kila kona ya dunia, vijana wanakabiliwa na kimbunga cha mabadiliko kuanzia maendeleo ya kiteknolojia, soko la ajira linalobadilika haraka, mabadiliko ya idadi ya watu, changamoto za tabianchi, na hasara za kujifunza kutokana na janga la coronavirus">COVID-19.

Hivyo amesisitiza “Kuwapa vijana elimu bora, mafunzo na ujuzi ni muhimu. Siku hii ya ujuzi wa vijana duniani inatukumbusha kwamba walimu wako mstari wa mbele katika juhudi hizi kubwa za kimataifa.”

Wasichana wakihudhuria mafunzo ya uandaaji wa harusi Mexico
© UNESCO-UNEVOC/Teresa de Jesus Caballero Melchor
Wasichana wakihudhuria mafunzo ya uandaaji wa harusi Mexico

Waalimu lazima wapate ujuzi unaohitajika

Ameendelea kusema kwamba “Ni lazima tuhakikishe walimu wanapata elimu na fursa za kujiendeleza kitaaluma wanazohitaji huku wakiwasaidia vijana kufanya mabadiliko kutoka shuleni kwenda kazini.”

Ameongeza kuwa hivi majuzi alizindua jopo la ngazi ya juu la Taaluma ya Ualimu ili kutoa mapendekezo ya kusaidia kufanikisha suala hili.

“Na tunahitaji kuongeza kwa kiasi kikubwa uwekezaji katika mifumo ya elimu, mafunzo na teknolojia duniani kote ili walimu waweze kutoa fursa za kujifunza kwa pamoja na zinazonyumbulika kwa vijana bila kujali wanaishi wapi.” Amesema Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Guterres ameikumbusha dunia kwamba “Mustakabali wa ubinadamu unategemea nguvu zisizo na mipaka, mawazo na michango ya vijana. Katika siku hii, na kila siku, hebu tusimame na walimu wanaposaidia vijana kupata elimu na ujuzi unaohitajika ili kutengeneza mustakabali bora na endelevu kwa ajili yetu sote.”

Debora Mtambalika ni mmoja wa wanafunzi katika chuo cha Afrika cha mafunzo ya kutengeneza ndege zisizo na rubani, ADDA nchini Malawi.
© UNICEF/UNI280220
Debora Mtambalika ni mmoja wa wanafunzi katika chuo cha Afrika cha mafunzo ya kutengeneza ndege zisizo na rubani, ADDA nchini Malawi.

Ajira milioni 600 zahitajika kwa ajili ya vijana

Makadirio ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa yanaonyesha kuwa nafasi za kazi milioni 600 zitahitajika kuundwa katika kipindi cha miaka 15 ijayo ili kukidhi mahitaji ya ajira kwa vijana.

Jumla ya idadi ya vijana wasio na ajira duniani ilikadiriwa kufikia milioni 73 mwaka 2022, ikiwa ni uboreshaji kidogo tu kutoka mwaka 2021 ambapo ilikuwa milioni 75 lakini bado milioni sita juu ya kiwango cha kabla ya janga la 2019.

Pia makadirio hayo yanasema idadi ya vijana itaongezeka kwa zaidi ya milioni 78 kati ya 2021 na 2030. 

“Na nchi za kipato cha chini zitachangia karibu nusu ya ongezeko hilo. Mifumo ya elimu na mafunzo inahitaji kukabiliana na changamoto hii.”