Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Binadamu tunaitegemea bahari, je bahari inaweza kututegemea?: Guterres

Viti Levu, nchini Fiji.
© Unsplash/Alec Douglas
Viti Levu, nchini Fiji.

Binadamu tunaitegemea bahari, je bahari inaweza kututegemea?: Guterres

Tabianchi na mazingira

Katika siku ya bahari duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema bahari ni msingi wa maisha na binadamu wanaitegemea bahari lakini anahoji je bahari inaweza kututegemea?

Kupitia ujumbe wake wa siku hii iliyobeba mauadhui “Sayari bahari, mawimbi yanabadilika” ambayo inalenga kuongeza ufahamu wa umuhimu wa bahari na haja ya kuilinda, Guterres amesema bahari “Inatoa hewa tunayovuta na chakula tunachokula.”

Ameongeza kuwa bahari “Inasimamia hali ya hewa yetu na tabianchi. Bahari ni hifadhi kubwa zaidi ya sayari yetu ya viumbe hai, rasilimali zake hudumisha jamii, ustawi na afya ya binadamu duniani kote.”

Tunapaswa kuwa marafiki wa baharí

Katibu Mkuu ameitaka dunia kutambua kwamba “Tunapaswa kuwa marafiki wa bahari, lakini hivi sasa, binadamu ni adui wake mbaya zaidi.”

Kwani amesema mabadiliko ya tabianchi yanayochochewa na binadamu yanapasha joto sayari yetu, kuathiri mifumo ya hali ya hewa na mikondo ya bahari, na kubadilisha mifumo ya ikolojia ya baharini na viumbe wanaoishi humo.

Bayoanuwai ya baharini ameongeza kuwa inakabiliwa na uvuvi wa kupita kiasi, unyonyaji kupita kiasi na ongezeko la tindikali baharini.

Kana kwamba hiyo haitoshi amesema “zaidi ya theluthi moja ya hifadhi ya samaki inavunwa kwa viwango visivyo endelevu na binadamu wanachafua maji ya pwani kwa kemikali, plastiki na kinyesi.”

Katika Mkutano wa Mindelo Ocean Summit, Katibu Mkuu António Guterres anatia saini Ukuta wa Mbio za Bahari pamoja na José Ulisses Correia e Silva, Waziri Mkuu wa Cabo Verde.
UN Photo/Mark Garten
Katika Mkutano wa Mindelo Ocean Summit, Katibu Mkuu António Guterres anatia saini Ukuta wa Mbio za Bahari pamoja na José Ulisses Correia e Silva, Waziri Mkuu wa Cabo Verde.

Mawimbi yanabadilika

Hata hivyo amesisitiza kwamba “Siku ya bahari mwaka huu inatukumbusha kwamba mawimbi yanabadilika. Mwaka jana, tulipitisha lengo kuu la kimataifa la kuhifadhi na kusimamia asilimia 30 ya ardhi, maeneo ya bahari na pwani ifikapo 2030, pamoja na makubaliano ya kihistoria kuhusu ruzuku ya uvuvi.”

Katika mkutano wa bahari uliofanyika Lisbon Ureno dunia ilikubaliana kuhimiza hatua chanya kwa ajili ya bahari na makubaliano ya kimataifa yanayobana kisheria ya kutokomeza taka za plastiki hivi sasa yako katika majadiliano.

Guterres amesema na mwezi Machi mwaka huu , nchi zilikubaliana mkataba wa kihistoria wa Bahari Kuu kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya bayoanuwai ya baharini katika maeneo yaliyo nje ya mamlaka ya kitaifa.

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba “Kutimiza ahadi kubwa ya mipango hii kunahitaji uwajibikaji wa pamoja.” Lengo la 14 la Maendeleo Endelevu la kuhifadhi na kutumia kwa uendelevu rasilimali za bahari liko njiapanda.

Hivyo ametoa wito “Katika siku hii ya baharí duniani hepu tuendelee kusukuma uchukuaji hatua. Leo na kila siku hebu tutoe kipaumbele cha kwanza kwa baharí.”