Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mji wa Rafah umejaa pomoni, hofu juu ya mustakabali wa watoto

Kupata huduma za maji safi ni suala la uhai na kifo kwenye Ukanda wa Gaza. Kupata mkate, maji ni shida.
© UNRWA
Kupata huduma za maji safi ni suala la uhai na kifo kwenye Ukanda wa Gaza. Kupata mkate, maji ni shida.

Mji wa Rafah umejaa pomoni, hofu juu ya mustakabali wa watoto

Amani na Usalama

Maelfu ya wakazi wa Gaza wameendelea kukimbia mapigano makali huko Khan Younis kati ya jeshi la Israel na wapiganaji wa kipalestina wa Hamas, na sasa raia hao wanakimbilia mji wa kusini wa Rafah ambao watoa misaada ya kibinadamu wanasema “umejaa pomoni.”

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imetoa onyo hilo la kufurika kwa mji wa Rafah, ikiwa ni takribani miezi minne tangu Israel ianze mashambulizi ikiwa ni kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Hamas tarehe 7 mwezi Oktoba mwaka 2023 kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu 1,200 na wengine zaidi ya 250 kutekwa nyara.

“Katika siku za karibuni, maelfu ya wapalestina wamekuwa wakikimbilia Rafah, ambako tayari mji huo unahifadhi zaidi ya nusu ya wakazi wa Gaza ambao ni takribani watu milioni 2.3,” amesema Jens Laerke, msemaji wa OCHA.

100 wamekufa, wamejeruhiwa au hwajulikani waliko

Akirejelea hofu ya kwamba hakuna pahala popote Gaza ambapo ni salama kufuatia taarifa kwamba Israel ilikuwa inashambulia kwa makombora maeneo ya kando mwa Rafah, leo Ijuma, Bwana Laerke amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kuwa idadi kubwa ya wagaza wapya wanaowasili Rafah “wanaishi kwenye maeneo ya kuhamahama, mahema au maeneo ya wazi. Kwa sasa Rafah ni kimbilio lakini ni ‘bomu linaloweza kulipuka wakati wowote,’ tunasubiri kuona kitakachotokea.”

Hadi leo hii, watu 100,000 Gaza “penginepo wamekufa, wamejeruhiwa, au hawajulikani waliko au wanadhaniwa kuwa wamekufa” kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa angani na ardhini wakati wa mapigano kati ya jeshi la Israel na Hamas, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO

Asilimia 60 ya vifo 27,019 vilivyoripotiwa na mamlaka za afya kwenye eneo lililozingirwa la Gaza ni wanawake na watoot, na WHO imeripoti kuwa zaidi ya majeruhi 66,000 wanahitaij matibabu ambayo ni vigumu kuyapata.

Wapalestina wakihaha kupata mkate na maji Gaza
© UNRWA
Wapalestina wakihaha kupata mkate na maji Gaza

Watoto wana kiwewe

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF hii leo limeripoti kuwa watoto wapatao 17,000 huko Gaza wako peke yao bila wazazi wala walezi.

“Kila mmoja ana simulizi ya kupoteza mzazi na machungu” amesema Jonathan Crickx,  Mkuu wa Mawasiliano wa UNICEF kwenye eneo linalokaliwa la Palestina.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi kutokea mjini Yerusalem, Afisa huyo wa UNICEF ameelezea mazungumzo yake na vijana aliokutana nao Gaza mapema wiki hii.

Amesema mmoja wao alikuwa ni Razan mwenye umri wa miaka 11 ambaye amepoteza familia yake yote wakati wa mashambulizi ya wiki za mwanzoni za vita inayoendelea.

Mguu ulikatwa kisha kidonda kikapata maambukizi- Razan

“Mama yake, baba, kaka na dada wawili waliuawa,” amesema Bwana Crickx, akiongeza kuwa “Mguu mmoja wa Razan ulijeruhiwa na ilibidi ukatwe. Kufuatia upasuaji aliofanyiwa, kidonda chake kilipata maambukizi. Hivi sasa Razah anatunzwa na shangazi na mjomba wake ambao wote sasa imebidi wahamie Rafah.”

Kutokana na uhaba wa chakula, maji na malazi, familia zenye jamaa na ndugu zinahaha kujitunza, sembuse watoto yatima, au watoto wasiokuwa na walezi au wazazi, amesema Afisa huyo wa UNICEF.

“Nilikutana na watoto hawa Rafah. Tunahofua kuwa hali ya watoto ambao wamepoteza wazazi ni mbaya zaidi kaskazini na kati mwa Ukanda wa Gaza.”