Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Tor Wennesland akaribisha kuachiliwa kwa mateka 13 wa Israel na wafungwa 39 wa kipalestina

Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati
UN Photo/Eskinder Debebe
Tor Wennesland, Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani ya Mashariki ya Kati

GAZA: Tor Wennesland akaribisha kuachiliwa kwa mateka 13 wa Israel na wafungwa 39 wa kipalestina

Amani na Usalama

  • Hamas yaachilia huru mateka 13 wa kiisraeli
  • Israel yaachiliwa wafungwa 39 wa kipalestina
  • Tor Wennesland ataka sitisho la mapigano lifankishe amani ya kudumu

Hatimaye mateka 13 wa Israeli waliokuwa wanashikiliwa na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas wameachiliwa huru hii leo Ijumaa, halikadhalika wafugwa 39 wa kipalestina waliokuwa wanashikiliwa kwenye magereza ncihni Israel, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya sitisho la mapigano yaliyofikiwa Jumatano wiki hii kati ya Israel na Hamas huko Mashariki ya Kati. 

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mashariki ya Kati, Tor Wennesland amekaribisha hatua hiyo pamoja na kuachiliwa huru pia kwa watumishi wa kigeni waliokuwa wanashikiliwa Gaza huku akisema anasubiri kwa hamu kuachiliwa huru kwa watu wengine siku chache zijazo.

Taarifa iliyotolewa leo mjini Yerusalem, imesema sitisho hilo la mapigano kwa msingi wa kiutu, limeenda sambamba na kuweko kwa utulivu kiasi ambapo pia malori yenye shehena za misaada ya kibinadamu yameruhusiwa kuingia Gaza.

Makubaliano yawezeshe misaada kuingia zaidi

Hatua hii, kwa mujibu wa Bwana Wennesland, “Ni muhimu ili kwa hatua za kiutu ambazo tunahitaji kuzisongesha.”

Mathalani misaada zaidi na vifaa lazima viingie Ukanda wa Gaza kwa usalama na kwa uendelevu ili kuondoa machungu makubwa yanayokabili wakazi wa eneo hilo lililozingirwa na vikosi vya Israel.

Mateka wote wanaoshikiliwa na Hamas na wengineo Gaza waachiliwe huru

Mjumbe huyo maalum wa mchakato wa amani Mashariki ya Kati amererejelea wito wake wa kutaka mateka wote wanaoshikiliwa Gaza na Hamas na watu wengine waachiliwe huru.

Ametoa shukrani na kupongeza juhudi za serikali za Qatar, Misri na Marekani za kufanikisha makubaliano hayo yaliyoanza kuzaa matunda leo.

Hata hivyo ametoa wito kwa pande husika kwenye mzooz huo kuzingatia ahadi zao na kujizuia na vitendo vyovyote vinavyoweza kuchochea uhasama au vitendo vyovyote vinavyoweza kuathiri vibaya utekelezaji kamilifu wa makubaliano hayo.

Na vile vile pande husika kutumia kila juhudi zote ziwezekanavyo ili kufanikisha na kuongeza muda wa sitisho la mapigano na kuwa na mustakabali wenye amani.