Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho la mapigano Gaza: Matumaini ya kupumzika mashambulizi na kufikia wahitaji

Mtoto mwenyeumri wa miaka mitano akinywa maji ya kwenye chupa yaliyowasilishwa na UNICEF kwenye kambi ya Khan Younis, ukanda wa Gaza
© UNICEF/Eyad El Baba
Mtoto mwenyeumri wa miaka mitano akinywa maji ya kwenye chupa yaliyowasilishwa na UNICEF kwenye kambi ya Khan Younis, ukanda wa Gaza

Sitisho la mapigano Gaza: Matumaini ya kupumzika mashambulizi na kufikia wahitaji

Amani na Usalama

Malori yaliyosheheni misaada ya kiutu yameendelea kuingia Ukanda wa Gaza kutokea Misri kupitia kivuko cha Rafah hii leo baada ya kuanza kutekelezwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku nne, yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na usaidizi wa kibinadamu.

Mashirika hayo yamerejelea wito wao kwamba sitisho hili la mapigano liwezesha kufikia maeneo  yote ya Ukanda huo wa Gaza uliozingirwa na Israel ambako idadiya vifo inaelekea kufikia watu 15,000 na wengine wengi waliokimbia makazi yao wanaishi mitaani.

James Laerke ambaye ni msemaji wa OCHA, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya kiutu na dharura amewaeleza waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi kwamba matumaini kutokana na makubaliano hayo kati ya Israel na wanamgambo wa kipalestina, Hamas yaliyofikiwa mapema wiki hii ni kwamba “sitisho la mapigano linazingatiwa, linatuwezesha kufikia wale wanaotuhitaji na kwamba makubaliano hayo yataongezwa kwa muda mrefu na kuwa sitisho halisi la mapigano kwa msingi wa kiutu.”

Kando ya sitisho la mapigano kwa saa 96 kwa msingi wa kiutu, makuabaliano hayo ambayo yalifanikishwa na Misri, Qatar na Marekani, yanataka pia kuachiliwa huru kwa mateka  waliochukuliwa na Hams wakati wa shambulio lao la kigaidi tarehe 7 Oktoba 2023, halikadhalika kuachiliwa kwa wapalestina wanaoshikiliwa kwene magereza nchini Israel.

“Tunatumaini kuwa makubaliano haya yataleta pumziko kidogo kwa wakazi wa Gaza na Israel na unafuu kwa mateka na wafungwa ambao wataachiliwa huru, vile vile kwa familia zao,” amesema Bwana Laerke.

Tweet URL

Kufikia watu pale waliko

Msemaji huyo wa OCHA amegusia, “hali tete na hatarishi iliyoshuhudiwa katika saa chache baada ya kuanza kwa makubaliano hayo akisisitiza kuwa njia ya kupita kufikisha misaada ni ndefu mno na haiku chini ya udhibiti wtu na hii inahusisha pia uthibitishaji wa shehena zinazopelekwa.”

Akizungumzia uharaka wa kufikia wahitaji, “kokote pale waliko,” ameangazia umuhimu wa kufikia eneo la kaskazini mwa Gaza “ambako uharibifu na mahitaji ya kiutu ni makubwa kupindukia,” na ambako kwa muda mrefu eneo hilo limekatwa na mawasiliano na eneo la kusini mwa Gaza na halipatiwi misaada kutokana na operesheni za jeshi la Israel.

Mipango zaidi kuhamisha wagonjwa

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO limeelezea matumaini yake kuwa sitisho la mapigano litatoa fursa ya kuhamisha wagonjwa na kuwapaleka mahala salama.

Msemaji wa WHO Christian Lindmeir akizungumza Geneva, Uswisi ameangazia machungu wanayopitia wagonjwa na wahudumu wa afya walionaswa kwenye hospitali zilizoko eneo la kaskazini huko Ukanda wa Gaza uliozingirwa na Israel.

Amesema mipango inaendelea ili kuhamisha wengine kutoka hospitali za Indonesia na Al-Ahli.

Jana Jumatano, juhudi za mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya kiutu, likiwemo shirika la Hilal Nyekundu la Kipalestina, PRCS, ziliwezesha kuhamisha majeruhi na wagonjwa 151 pamoja na familia zao na wahudumu wa afya kutoka hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza.Walisafirishwa kwa gari la wagonjwa na basi kuelekea kusini.

Bwana Lindmeier amesema WHO ina hofu kubwa juu ya usalama wa wagonjwa 100 na wahudumu wa afya waliosalia kwenye hospitali hiyo.

‘Waondolewe hofu wakazi wa Gaza

Zaidi ya watu milioni 1.7 katika Ukanda wa Gaza wanakadiriwa kuwa ni wakimbizi wa ndani na takribani milioni moja kati yao hao wanaishi kwenye makazi zaidi ya 150 yanayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kiplestina, UNRWA.

Makazi kusini mwa Gaza, ambako watu wamelazimika kukimbilia ili kuepuka mashambulio kutoka jeshi la Israel, mengi yao yamezidiwa uwezo na OCHA inasema idadi kubwa ya wakimbizi wanaume na vijana wa kiume wanalala maeneo ya wazi, kwenye shuleni au mitaani.

Kupitia  taarifa aliyotoa Alhamisi, Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazarini amesisitiza kuwa watu walioko Gaza wanastahili kuishi bila kuwa na hofu ya iwapo wataiona siku mpya kesho yake.

“Hiki angalau ni kitu kidogo tu ambayo kila mtu anapaswa kuwa nacho,” amesema Lazarrini.