Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utekelezaji wa sitisho la mapigano ukikaribia Gaza UN iko tayari kutoa misaada

Wanawake wa Kipalestina wakitembea kwenye kifusi katika kitongoji cha Nasr
© UNICEF/Mohammad Ajjour
Wanawake wa Kipalestina wakitembea kwenye kifusi katika kitongoji cha Nasr

Utekelezaji wa sitisho la mapigano ukikaribia Gaza UN iko tayari kutoa misaada

Amani na Usalama

Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu yanayojiandaa kuingia Gaza leo yanaendelea kukusanya akiba ya misaada inayohitajika sana kwa eneo hilo lililokumbwa na vita huku kukiwa na ucheleweshaji wa utekelezaji wa kusitishwa kwa mapigano kwa muda na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, mazungumzo yanayoendelea kuhusu makubaliano ya Israel na Hamas juu ya kusitishwa vita kwa siku nne kwa ajili ya masuala ya kibinadamu na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na kundi la wapiganaji wa Palestina la Hamas tangu mashambulizi yake ya kigaidi ya Oktoba 7 yanaonyesha kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo hauwezekani kuanza kabla ya Ijumaa.

Wakati changamoto ya njaa ikiongezeka Gaza mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP Cindy McCain amesema shirika hilo "linahamasisha kwa haraka kuongeza msaada ndani ya Gaza mara tu ufikiaji salama utakaporuhusiwa.”

Maoni yake yanafuatia taarifa ya mkuu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya dharura Martin Griffiths juu ya utayari wa shirika hilo kuongeza kiasi kikubwa cha misaada inayoletwa katika eneo Gaza na kusambazwa katika Ukanda huo.

Bi McCain amesema  malori ya WFP "Yanasubiri kwenye kivuko cha Rafah, yakiwa yamesheheni chakula kilichopangwa kwa ajili ya familia katika makazi ya wakimbizi na nyumba kote Gaza, na unga wa ngano kwa ajili ya mikate ili kuanza kazi".

Ripoti za hivi punde za kibinadamu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa unga wa ngano haupatikani tena katika masoko ya kaskazini mwa Gaza na kwamba hakuna maduka ya mikate yanayofanya kazi kutokana na ukosefu wa mafuta, maji, unga na uharibifu wa miundombinu.

Watoto wakihahamishwa kutoka hospitali ya Al-Shifa huko Kaskazini mwa Gaza kuelekea eneo la Kusini mwa ukanda huo wa Gaza huko Mashariki ya Kati kutokana na mapigano  yanayoendelea hivi sasa kati ya Israel na wapiganaji wa kipalestina wa Hamas
© UNICEF/Eyad El Baba
Watoto wakihahamishwa kutoka hospitali ya Al-Shifa huko Kaskazini mwa Gaza kuelekea eneo la Kusini mwa ukanda huo wa Gaza huko Mashariki ya Kati kutokana na mapigano yanayoendelea hivi sasa kati ya Israel na wapiganaji wa kipalestina wa Hamas

Matumaini ya maisha

Tangu uwasilishaji mdogo wa misaada kupitia kivuko cha Rafah na Misri kuanza tena tarehe 21 Oktoba, zaidi ya malori 73 ya msaada wa chakula wa WFP yamefika Gaza, lakini msaada huo hautoshelezi kabisa.

Bi. McCain ameonyesha matumaini kwamba mafuta zaidi yataingizwa ndani ya eneo hilo "ili malori yetu yaweze kubeba vifaa vinavyohitajika sana na kwamba mkate utapatikana tena kama njia ya kuokoa mamia ya maelfu ya Maisha ya watu kila siku".

Takriban lita 75,000 za mafuta ziliingia Gaza kutoka Misri Jumatano kufuatia uamuzi wa Israel wiki iliyopita wa kuruhusu "kuingia kila siku kwa kiasi kidogo cha mafuta kwa ajili ya shughuli muhimu za kibinadamu", kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA.

Mafuta hayo yanasambazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa ajili ya wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, kusaidia usambazaji wa chakula na uendeshaji wa jenereta katika hospitali, vituo vya maji na usafi wa mazingira, makazi na huduma nyingine muhimu kusini mwa Ukanda huo, wakati ufikiaji wa eneo la Gaza kaskazini umekatishwa na operesheni za kijeshi za Israel.

Mkuu wa OCHA Martin Griffiths wiki iliyopita alisema kwamba takriban lita 200,000 za mafuta zinahitajika kwa siku.

Watoto wanatembea katika kambi ya muda kusini mwa Gaza.
WHO
Watoto wanatembea katika kambi ya muda kusini mwa Gaza.

Uhamishaji wa watu hospitali

Uhamisho mpya wa watu 190 waliojeruhiwa, wagonjwa wenzao na wafanyikazi wa huduma za afya kutoka hospitali ya Al-Shifa katika Jiji la Gaza ulikamilika jana Jumatano.

Hatua hiyo ilitangazwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO kama juhudi za pamoja kati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu wakiongozwa na Chama cha Hilali Nyekundu cha Palestina PRCS.

Wakimbizi hao walisafirishwa kwa msafara wa gari la wagonjwa kuelekea Kusini mwa Gaza.

OCHA ilinukuu ripoti za PRCS zikisema kwamba uhamishaji huo "ulidumu kwa karibu saa 20 huku msafara huo ukizuiliwa na kufanyiwa ukaguzi wakati ukipita kwenye kizuizi kinachotenganisha kaskazini na kusini mwa Gaza na kusikitishwa na ukweli kwamba maisha ya wagonjwa yalikuwa hatarini.”

Wagonjwa wanaosafishwa vifo au dialysis waliohamishwa walihamishiwa katika Hospitali ya Abu Youssef An Najjar huko Rafah, Gaza, wakati wagonjwa wengine walisafirishwa hadi hospitali ya Ukanda wa Ulaya huko Khan Younis. 

Takriban wagonjwa 250 na wafanyikazi wanaaminika kuwa katika hospital ya Al-Shifa, ambayo haifanyi kazi tena, imesema OCHA.

Wakati huo huo, jana Jumatano ilishuhudia idadi ndogo zaidi ya watu waliokimbia kutoka kaskazini mwa Gaza na kuvuka kuelekea kusini kwa kutumia upenyo uliofunguliwa na vikosi vya ulinzi vya Israeli kwenye eneo lenye msongamano mkubwa katika Ukanda huo la barabara ya Salah Ad Deen.

Kulingana na ufuatiliaji wa OCHA ni takriban watu 250 waliohamia kusini. Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kupungua huko "kunachangiwa zaidi na matarajio yanayotokana na kusitishwa kwa uhasama kwa minajili ya misaada ya kibinadamu" ambakoo bado hakujatekelezwa.

Hadi sasa, zaidi ya watu milioni 1.7 huko Gaza ni wakimbizi wa ndani.