Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UN arudia wito wake kwa Israel kusitisha mashambulizi Rafah

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika Mkutano wa ngazi za juu wa Muungano wa Nchi za Kiarabu huko Manama-Bahrain.
UN News
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika Mkutano wa ngazi za juu wa Muungano wa Nchi za Kiarabu huko Manama-Bahrain.

Mkuu wa UN arudia wito wake kwa Israel kusitisha mashambulizi Rafah

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amerejea onyo lake dhidi ya shambulio yanayoendelea huko Rafah, kama vile timu za misaada zilivyotoa wito wa dharura wakutaka waweze kupita kwa usalama katika eneo lote la Gaza, ili kufikisha misaada kwani kwa sasa akiba ya misaada ya kuokoa maisha ipo chini.

Katika tukio linalohusiana na hilo, Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ hii leo imesikiliza ombi kutoka taifa la Afrika Kusini ambalo linaiomba mahakama hiyo kuliwekea vikwazo zaidi jeshi la Israel ambalo linafanya mashambulizi ya anga na ardhini huko Ukanda wa Gaza mashambulizi ambayo yamegharibu maelfu ya maisha ya watu.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inasikiliza ombi lililowasilishwa na Afrika Kusini tarehe 10 Mei 2024 katika kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel.
UN Photo
Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inasikiliza ombi lililowasilishwa na Afrika Kusini tarehe 10 Mei 2024 katika kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel.

Afrika Kusini inataka mahakama ya ICJ kuipa amri Israel ya kusitisha operesheni zake za kijeshi katika mji wa Rafah kusini mwa Gaza.

Katika wito wa "kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote" ambao bado wanashikiliwa huko Gaza, Katibu Mkuu Guterrres aliwaambia viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wakati akihutubia katika Mkutano huko Bahrain kwamba hakuna kitu kinachohalalisha "adhabu ya pamoja" ya Wapalestina.

“Shambulio lolote dhidi ya Rafah halikubaliki; litasababisha ongezeko lingine la maumivu na taabu tunapohitaji msaada wa kuokoa maisha,” aliongeza.

Akiongozwa na Philippe Lazzarini, ambaye ni mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA,  Guterres pia aliunga mkono tena shirika hilo la Umoja wa Mataifa na kusema "Linasalia kuwa uti wa mgongo wa operesheni zetu huko Gaza na njia ya kuokoa wakimbizi wa Kipalestina katika kanda na linahitaji usaidizi kamili na ufadhili,” alisisitiza wakati huu ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP likitoa onyo jipya kuhusu njaa inayokuja huko Gaza.

Misafara ya chakula iliyokuwa ikisafiri kuelekea Kaskazini mwa Gaza imeshambulia na mikombora. (Maktaba)
© UNRWA
Misafara ya chakula iliyokuwa ikisafiri kuelekea Kaskazini mwa Gaza imeshambulia na mikombora. (Maktaba)

Kuvuka vizuizi 

“Akiba ya chakula na mafuta itaisha baada ya siku chache,” limeonya WFP katika chapisho lake kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X. "Tangu Mei 6, hatujaweza kufikia na kupokea misaada kutoka katika kivuko cha Kerem Shalom. Hali inazidi kuwa mbaya."

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilionesha tishio la kweli kwamba kuongezeka kwa uhasama huko Gaza kunaweza kusababisha operesheni za misaada "kusimama kabisa" na kusababisha janga la kibinadamu.

Ingawa WFP imetoa vyakula maalum vya lishe kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto chini ya umri wa miaka mitano kote Gaza, shirika hilo limesema kuwa hadi kufikia tarehe 11 Mei ugawaji ulisitishwa huko Rafah "na unaendelea tu katika maeneo ya Khan Younis na Deir El Balah kwa kiwango kidogo”.

Nako Kaskazini mwa Gaza, WFP pia ilionya kwamba viwango vya utapiamlo mkali miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili "vimeongezeka mara mbili kutoka asilimia 15 mwezi Januari hadi asilimia 30 mwezi Machi mwaka huu".

Wasaidizi wa kibinadamu wanaonya kwamba utapiamlo uliokithiri ndio aina hatari zaidi ya utapiamlo, na kuwaacha watoto walioathirika kati ya mara tatu hadi 12 zaidi ya uwezekano wa kufa kuliko mtoto mwenye lishe bora.

Tathmini hiyo ya kutisha inakuja wakati shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) likiripoti jana jioni kwamba watu 600,000 – ambao ni robo ya wakazi wa Gaza - sasa wamefurushwa kwa lazima kutoka Rafah katika wiki iliyopita, huku kukiwa na shughuli zinazoendelea za kijeshi za Israeli na maagizo ya kuwataka wapalestina kuondoka eneo la Rafah.

Watu wengine 100,000 wamekimbia eneo la kaskazini ili kutii amri ya kuhamishwa na jeshi la Israel, huku mapigano makali ya risasi yakiripotiwa kupamba moto.

Takriban watu milioni 1.7 wamekimbia makazi yao huko Gaza, mara kadhaa.
© UNRWA
Takriban watu milioni 1.7 wamekimbia makazi yao huko Gaza, mara kadhaa.

Amri ya kuondoka

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, "kilomita za mraba 285, au takriban asilimia 78 ya Ukanda wa Gaza" sasa wamepewa amri ya kutakiwa kuondoka na jeshi la Israel.

Katika chapisho lake la hivi karibuni, OCHA iliripoti kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu "kutoka angani, ardhini na baharini...katika sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza, na kusababisha vifo zaidi vya raia, kufurushwa, na uharibifu wa nyumba na miundombinu mingine ya raia".

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ilithibitisha ripoti za uvamizi wa ardhini na mapigano makali huko Jabalia kaskazini mwa Gaza, na vile vile huko Deir al Balah katikati mwa Gaza na mashariki mwa Rafah kusini.

"Hadi kufikia Mei 15, kivuko cha Rafah kilikuwa bado kimefungwa. Kivuko cha Kerem Shalom kinafanya kazi, lakini hali ya usalama na vifaa iliyopo inatatiza utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa kiwango kikubwa,” OCHA ilibainisha.

Ikirejelea wasiwasi huo, WFP lilisisitiza kwamba "maeneo mengi ya kuingia Gaza" kwa ajili ya kutoa misaada yanahitajika" ili ku kubadilisha hali ya njaa kwa miezi sita na kuepusha njaa, mtiririko wa kutosha wa chakula, kila siku na kila wiki…Tishio la njaa huko Gaza linaonekana kuwa kubwa zaidi."

Afrika Kusini dhidi ya Israel

Katika juhudi za kusitisha operesheni ya kijeshi ndani na karibu na mji wa kusini mwa eneo hilo, Afrika Kusini iliwasilisha ombi jipya kwa mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa ya Haki ICJ ambayo ilitakiwa kusikilizwa hii leo.

"Hatua za haraka zinahitajika ili kuhakikisha kuwa Wapalestina wanasalia huko Gaza," ombi la Afrika Kusini lilisema, katika madai yake yaliyowasilishwa tarehe 10 Mei, 2024.

"Hali iliyoletwa na shambulio la Israeli dhidi ya Rafah, na hatari kubwa inayoleta kwa vifaa vya usambazaji wa misaada ya kibinadamu na huduma za kimsingi huko Gaza, kwa maisha ya mfumo wa matibabu wa Palestina, na maisha ya Wapalestina huko Gaza kama kikundi, sio tu inazidisha hali iliyopo, bali kunaongeza ukweli mpya ambao unasababisha madhara yasiyoweza kurekebishwa kwa haki za watu wa Palestina huko Gaza.

Kote Rafah ni magofu
© UNRWA
Kote Rafah ni magofu

Rafah ni kimbilio la mwisho

Rafah ni "kimbilio la mwisho" kwa Wananchi wa gaza, ombi la Afrika Kusini liliendelea kueleza, na kuongeza kuwa jiji hilo pia ni "kituo cha mwisho kinachoweza kutumika" kwa makazi na huduma za kimsingi ikiwa ni pamoja na matibabu. Jeshi la Israel kushikilia kivuko cha Rafah na kufungwa kwa muda mfupi na matatizo yanayoendelea ya kufikia kivuko kilicho karibu cha Kerem Shalom kumezuia sehemu kuu za kuingilia kwa ajili ya misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha Gaza, Afrika Kusini ilisisitiza.

"Watu waliosalia na vituo vya matibabu viko katika hatari kubwa, kutokana na ushahidi wa hivi karibuni wa maeneo ya uhamishaji kuchukuliwa kama maeneo ya maangamizi, uharibifu mkubwa na makaburi ya halaiki katika hospitali nyingine za Gaza na matumizi ya Akili mnemba - AI kutambua 'maeneo ya kuua'," nyaraka za mahakama ya ICJ zinaonesha.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki hapo awali ilitoa amri maalum kwa Israeli mwishoni mwa mwezi Januari - inayojulikana kama "hatua za muda" - kuzuia madhara kwa Wagaza, kufuatia madai ya Afrika Kusini kwamba Israel ilikiuka wajibu wake kama mtia saini Mkataba wa Mauaji ya Kimbari. Hakukuwa na wito wa kusitishwa mara moja kwa operesheni kamili ya kijeshi ya Israeli katika Ukanda huo.

Israel ilikanusha vikali madai hayo na imepanga kujibu ombi la hivi karibuni la Afrika Kusini siku ya Ijumaa.