Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi wa madai dhidi ya wafanyakazi wa UNRWA Gaza utakuwa wa ufanisi:Guterres

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu Mashariki ya Kati.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu Mashariki ya Kati.

Uchunguzi wa madai dhidi ya wafanyakazi wa UNRWA Gaza utakuwa wa ufanisi:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ameendelea kusistiza kwamba uchunguzi wa madai dhidi ya wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kuhusika katika mashambulizi ya oktoba 7 mwaka jana Kusini mwa Israel utafanyika kwa kina na kwa ufanisi.

Kupitia taarifa iliyotolewa mjini New York Marekani na msemaji wake mbele ya waandishi wa habari Katibu Mkuu amekutana leo na msaidizi wa Katibu Mkuu na mkuu wa Ofisi ya Huduma za Uangalizi wa Ndani OIOS ili kuhakikisha uchunguzi huo unafanyika kwa uafanisi.

Msekaji huyo amerejea kusisitiza kwamba “Mfanyakazi yeyote anayehusika na vitendo vya kigaidi atawajibishwa ikiwa ni pamoja na kupitia mkondo wa kisheria wa jinai.”

UN iko tayari kutoa ushirikiano

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amekumbusha kuwa “Na kama tulivyosema, Sekretarieti iko tayari kushirikiana na mamlaka yenye uwezo wa kuwashtaki watu binafsi, kwa kuzingatia taratibu za kawaida za Sekretarieti za ushirikiano huo.”

Ameongeza kuwa “Katibu Mkuu pia amekuwa akishirikiana na uongozi wa UNRWA na wafadhili wa UNRWA, pamoja na viongozi wa kanda, kama vile Mfalme Abdullah wa Jordan, ambaye alizungumza naye muda mfupi uliopita, na Rais Sisi wa Misri, ambaye atazungumza naye baadaye mchana huu.”

Pia amesema Katibu Mkuu binafsi amesikitishwa na shutuma dhidi ya wafanyakazi wa UNRWA, lakini ujumbe wake kwa wafadhili, hasa wale waliositisha michango yao ni kuhakikisha angalau kuendelea kwa operesheni za UNRWA, “kwani tuna makumi ya maelfu ya wafanyakazi wa kujitolea wanaofanya kazi kwa muda wote katika eneo hilo. Mahitaji makubwa ya watu waliokata tamaa wanaowahudumia lazima yatimizwe.”

Amehitimisha tarifa hiyo kwa kukumbusha kwamba “Katika wakati huu, mtazamo wa UNRWA na mamilioni ya watu inaowahudumia, sio tu Gaza, lakini pia Jerusalem Mashariki, katika Ukingo wa Magharibi, Jordan, Lebanon na Syria ni makubwa sana.”