Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeni viongozi wanawake kwenye STEM kuvutia wasichana kujiunga na tehama

Wasichana kwenye TEHAMA, Addis Ababa, Ethiopia.
© ITU/M. Jacobson – Gonzalez
Wasichana kwenye TEHAMA, Addis Ababa, Ethiopia.

Ongezeni viongozi wanawake kwenye STEM kuvutia wasichana kujiunga na tehama

Wanawake

Leo ni siku ya kimataifa ya wasichana katika tehama na mwaka huu inasherehekea uongozi ikisisitiza hitaji muhimu la kuwa na mifano thabiti ya wanawake viongozi katika taaluma ya sayansi, teknolojia, uhandishi na hisabati -STEM kwani hali ilivyo sasa kuna wanawake viongozi wachache katika maeneo hayo. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la mawasiliano ITU limesema ingawa wanawake wanajaza asilimia 40 ya kazi za ujuzi wa juu zaidi duniani katika STEM lakini bado ushiriki wao katika nyanja zinazohusiana tehama unaendelea kuwa mdogo. 

ITU imesema wanawake nikama hawako kwenye masuala ya utengenezaji wa programu, uhandisi, utafiti wa teknolojia, ufundishaji na vile vile katika nafasi za juu za kutengeneza sera. Pia wanawake wameonekana kuwa katika muelekeo wa kuacha kazi za sayansi na teknolojia kwa viwango vya juu kuliko wanaume.

Ingawa kuna pengo la kijinsia katika kila sekta ila pengo kubwa la uhaba wa wanawake viongozi limeonekana kuwa katika masuala ya STEM ambapo wanawake wengi hujikuta katika nafasi za chini za uongozi au usaidizi kuliko nafasi za kuwa mameneja huku kukiwa na fursa chache za kupanda vyeo.

Ili kustawi katika STEM, wasichana na wanawake wanaochipukia katika eneo hili wanapaswa kuoneshwa wanawake wanaoshika nafasi za uongozi, kukuza msukumo na kuvunja vikwazo vinavyozuia maendeleo yao. 

Katika kuadhimisha siku hii ya wasichana katika tehama, inayoadhimishwa kimataifa nchini Ufilipo mada zinazojadiliwa zinalenga kushughulikia changamoto hizi, kuhimiza uwezeshaji na maendeleo ya uongozi kwa mustakabali wenye usawa katika STEM.