Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA iko tayari kutekeleza mapendekezo huru ya jopo la uchunguzi

Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina Philippe Lazzarini
UN Photo/Evan Schneider
Kamishina Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina Philippe Lazzarini

UNRWA iko tayari kutekeleza mapendekezo huru ya jopo la uchunguzi

Masuala ya UM

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA), Philippe Lazzarini, leo (23 Apr) aakizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani amerudia kusema anakaribisha mapendekezo ya ripoti iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kuhusu juhudi zake za kuhakikisha kutoegemea upande wowote na kujibu madai ya ukiukaji mkubwa yanapojitokeza.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna aliongoza ripoti hiyo iliyochapishwa Jumatatu Aprili 22, na ikionesha kuwa UNRWA imeweka idadi ya kutosha ya taratibu za kuhakikisha kujitolea kwake kwa kanuni ya kutoegemea upande wowote na kuainisha baadhi ya mapendekezo 50.

Kuhusu Ripoti ya Catherine Colonna, Lazzarini amesema, "umeona katika ripoti hiyo pia na shirika katika hali halisi tayari lina mifumo kadhaa ya kushughulikia masuala ya kutoegemea upande wowote, mbele zaidi kuliko wastani wa mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa au hata Mashirika yasiyo ya kiserikali, NGOs. Lakini kwa sababu ya ugumu wa mazingira tunayofanyia kazi, tunahitaji kuwa waangalifu sana, na tunaweza kufanya zaidi siku zote.”

UNRWA inashambuliwa

Aidha Lazzarini amewaeleza waaandishi wa Habari kwamba mashambulizi dhidi ya UNRWA, "si lazima kwamba yanachochewa kwa sababu ya masuala ya kutoegemea upande wowote, lakini kimsingi yanachochewa na lengo la kuwaondoa Wapalestina katika sheria ya wakimbizi."

Lazzarini amesema hii ni "sababu kwa nini kuna msukumo leo kwa UNRWA kutokuwepo tena Gaza, lakini sio Gaza pekee, pia tuko chini ya shinikizo kadhaa linapokuja suala la Yerusalemu na Ukingo wa Magharibi."

Kamishna Mkuu amebainisha kuwa wafanyakazi 180 wa UNRWA hadi sasa wameuawa huko Gaza tangu tarehe 7 Oktoba.

Amesema, “tulikuwa na majengo zaidi ya 160 ambayo yameharibika au kuharibiwa kabisa, huku watu takribani watu 400 wakiwa wameuawa walipokuwa wakitafuta ulinzi wa Umoja wa Mataifa. Pia tuna ripoti kwamba majengo yetu  yametumiwa kwa madhumuni ya kijeshi, ama na jeshi la Israel, lakini pia Hamas au makundi mengine ya kisiasa au makundi yenye silaha chini."

"Tunaendelea kusikia pia kwamba UNRWA inaendeleza hali ya ukimbizi, ambayo ni upuuzi. Kimsingi, ni kana kwamba ungesema kwamba jibu la kibinadamu katika eneo la migogoro linaendeleza mzozo huo. Ukweli ni kwamba hali ya ukimbizi inadumishwa kwa sababu ya kutokuwepo kwa suluhu ya kisiasa.”