Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashariki ya Kati bado hali si shwari, UNHCR yapaza sauti

Kundi la wanaume likipanda vifusi vya jengo lililobomolewa huko ukanda wa Gaza, Mashariki ya  Kati
© UNRWA/Mohammed Hinnawi
Kundi la wanaume likipanda vifusi vya jengo lililobomolewa huko ukanda wa Gaza, Mashariki ya Kati

Mashariki ya Kati bado hali si shwari, UNHCR yapaza sauti

Amani na Usalama

Mapigano huko Mashariki ya Kati yakiingia siku ya tatu kati ya Israel na wapalestina, huko Geneva, hii leo wajumbe wa mkutano wa 54 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za binadamu walisimama kwa dakika moja kuwakumbuka mamia ya watu waliopoteza maisha katika mapigano hayo yaliyoanza baada ya wanamgambo wa Hamas kurusha makombora kuelekea upande wa Israel. 

Takwimu kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA zinasema hadi sasa watu 370 wakiwemo watoto 20 wameuawa huku zaidi ya 2,200 wamejeruhiwa upande Palestina ihali kwa Israel waliouawa ni takribani 650.

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi amenukuliwa hii leo huko Geneva, Uswisi akisema shirika hilo linakabiliwa na moja ya nyakati ngumu zaidi katika historia yake ya miaka 70.

Bwana Grandi amesema picha za kutisha na kusikitisha za mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Hamas dhidi ya raia wa Israel zimegubika skrini za televisheni kwa saa 48.

Mkuu huyo wa UNHCR amesema “tunashuhudia vita nyingine Mashariki ya Kati, vita ambayo bila shaka itasababisha machungu zaidi kwa raia, pande zote za Israel na Palestina, na kuhatarisha kuleta ukosefu mkubwa wa utulivu kwenye ukanda huo ambao tayari umegubikwa na mvutano.”

Bwana Grandi amesema iwapo hatua hazitachukuliwa haraka kudhibiti, kuna hatari mzozo huo ukasambaa na kudumaza amani duniani.

Jana Jumapili, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana kwa faragha kujadili mapigano hayo Mashariki ya Kati huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa taarifa Jumamosi akilaani mashambulizi hayo ya Hamas dhidi ya Israel huku akitaka diplomasia itumike kumaliza mzozo huo