Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya idadi ya waliochanjwa, chanjo ya malaria nchini Kenya imeleta tija gani: WHO

Watoto nchini Kenya ambao ndio waathirika wakubwa wa maambukizo ya malaria.
GAVI
Watoto nchini Kenya ambao ndio waathirika wakubwa wa maambukizo ya malaria.

Zaidi ya idadi ya waliochanjwa, chanjo ya malaria nchini Kenya imeleta tija gani: WHO

Afya

Walezi, viongozi wa afya na wahudumu wa afya wa jamii wanaojitolea wanatafakari juu ya utekelezaji wa chanjo ya malaria na jinsi nyenzo hiyo mpya inavyowafikia watoto walio hatarini kwa kuzuia malaria kuokoa maisha.

Ziwa Victoria barani Afrika ni ziwa la pili kwa ukubwa duniani la maji baridi na ziwa kubwa zaidi la kitropiki.

Mfumo wa mazingira katika ukanda wa ziwa hilo unasaidia viumbe mbalimbali ikiwemo ndege wa ajabu, viumbe wa majini na wanyama.

Kwa bahati mbaya, mfumo huo wa ikolojia pia ni mahali pazuri pa kuzaliana kwa mbu wanaobeba vijidud vya malaria.

Wataalamu wa malaria wanataja maeneo karibu na ufuo wa ziwa hilo kama eneo la ziwa la Kenya lililoghubikwa na malaria.

Watu wengi huko wamepata maambukizi ya malaria, na wengi wamepata hasara ya kupoteza wapendwa waona ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na watoto, waathirika wa kawaida wa malaria na walio hatarini.

Chanjo dhidi ya malaria katika kituo cha afya.
GAVI
Chanjo dhidi ya malaria katika kituo cha afya.

Waathirika wa malaria

"Nilipokuwa nikikua, niliteseka sana kutokana na mashambulizi kadhaa ya ugonjwa wa malaria, na nimeona watoto wakiugua na kupata ulemavu wa kudumu," anasema Vivienne, mama wa watoto 5 kutoka soko la Chemelil, kijiji cha mashambani nje ya mji wa Kisumu.

Ameongeza kuwa "Watoto wangu 3 wakubwa wanakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya malaria. Hilo linapotokea, wanapoteza hamu ya kula, wanaugua homa, kuhara, na kutapika, na kuwa dhaifu sana.”

Uzoefu huu wa maisha na malaria ndio sababu Vivienne na akina mama wengine kote katika sehemu hii ya Kenya walikuwa na shauku kuhusu kuwasili kwa chanjo ya kwanza ya malaria duniani, RTS,S/AS01 (au RTS,S) mwaka wa 2019.

Mwaka huo, chanjo hiyo ilipatikana katika nchini  Kenya, pamoja na Ghana na Malawi, katika utangulizi wa majaribio kupitia mpango wa kitaifa wa chanjo, chini ya Mpango wa Utekelezaji wa Chanjo ya Malaria (MVIP) unaoratibiwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO.

Madhumuni ya majaribio yalikuwa kutathmini matumizi ya chanjo hiyo kwa afya ya umma, ikiwa ni pamoja na kama walezi wangewaleta watoto wao kwenye kliniki kwa ajili ya vipimo na kupata dozi 4 na athari za chanjo katika kupunguza magonjwa ya utotoni na vifo kutokana na malaria katika matumizi ya kawaida ya mara kwa mara.

Takriban miaka 4 tangu kuanza kwa chanjo hiyo, zaidi ya watoto milioni 1.4 wamepokea chanjo hiyo katika nchi 3 za majaribio, ambapo watoto 400,000 nchini Kenya wamepata angalau dozi yao ya kwanza.

Ufuatiliaji wa chanjo kwa watoto nchini Kenya.
WHO Kenya
Ufuatiliaji wa chanjo kwa watoto nchini Kenya.

Tija za utekelezaji wa chanjo ya malaria

"Chochote tulichokuwa tukitumia hapo awali, tulifikia mahali ambapo mzigo wa malaria uliongezeka, na tulihitaji zana mpya ya ziada," anaeleza Dkt. Gregory Ganda, mtendaji mkuu wa afya wa kaunti ya Kisumu.

Zaidi ya miaka 3 na kuendelea, chanjo hiyo imekuwa nyenzo muhimu na ya ziada ya kuokoa maisha sambamba na mbinu zingine za kukabiliana na malaria, kama vile matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa, unyunyiziaji wa dawa ndani ya nyumba, matibabu ya kinga kwa wajawazito, na dawa bora za malaria.

Tangu kuanmza kwa chanjo hiyo katika baadhi ya maeneo ya Kenya, kulazwa hospitalini kwa watoto chini ya miaka 5 kutokana na malaria kali kumepungua kwa kiasi kikubwa, na vifo vya watoto vimepungua.

"Katika kipindi cha miaka 3 iliyopita, tumeshuhudia upungufu mkubwa wa watoto wanaolazwa kutokana na malaria. Ni hisia nzuri kama daktari unapofikiria kufunga wodi kwa sababu ya ukosefu wa wagonjwa." ameongeza Dkt. Ganda.

Mbu aina ya anopheles waambukizao malaria wakiwa katika maabara ya taasisi ya KEMRI/CDC nje ya mji wa Kisumu nchini Kenya
Sven Torfinn/WHO 2016
Mbu aina ya anopheles waambukizao malaria wakiwa katika maabara ya taasisi ya KEMRI/CDC nje ya mji wa Kisumu nchini Kenya

Kutana na watoto wa kizazi cha chanjo ya malaria

Vivienne alisikia kwa mara ya kwanza kuhusu chanjo ya malaria kutoka kwa Rose Akinyi, mfanyakazi wa kujitolea wa afya ya jamii aliyefika nyumbani kwake muda mfupi baada ya kujifungua mtoto wake wa 4, Isaac.

Nchini Kenya wahudumu wa kujitolea wa afya ya jamii hutumika kama viungo muhimu kati ya walezi na mfumo wa huduma za afya.

Mbali na kuangalia afya ya Vivienne na Isaac, Rose alimkumbusha kuhusu chanjo mbalimbali zinazotolewa mara kwa mara nchini Kenya.

Kwa sababu Vivienne anaishi katika mojawapo ya kaunti ndogo 26 zilizoshiriki katika utangulizi wa majaribio ya chanjo, ambayo ni pamoja na chanjo ya malaria.

Isaac sasa amepokea dozi zote 4 za chanjo ya malaria, huku kaka yake mdogo, Moses, mwenye umri wa miezi 13, amepata dozi 3 za kwanza.

“Isaac na Moses wameteseka kidogo sana kutokana na malaria kuliko watoto wangu wengine. Watoto wana nguvu zaidi, na walipopata malaria, haikuwa kali sana,” ameongeza Vivienne.

Katika Homa Bay kaunti jirani, bintiye Margaret Atieno, Stella, hivi majuzi alipokea kipimo cha 3 cha chanjo hiyo.

Alieleza jinsi alivyotamani watoto wake wakubwa wangefaidika na kinga hiyo iliyoongezwa.

"Kuwa na chanjo ni muhimu kwa sababu inamlinda mtoto wangu," anasema. "Natamani hata ungekuwa na mtoto mwingine kwa watoto wakubwa ili waweze kulindwa kama vile Stella anavyolindwa."

Kwa ujumla, uamuzi ni mkubwa chanjo inaokoa maisha ya watoto, walezi wanataka chanjo hii kwa watoto wao, na watoto zaidi walio katika hatari wanafikiwa na kinga hii ya ziada ya malaria.

"Chanjo ya malaria imekuwa ya mabadiliko na mafanikio. Tumeona vifo vikipungua kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 1 na chini ya umri wa miaka 5. Watu hawakufikiri tungeweza kupata chanjo ya malaria, na sasa kila mtu ana furaha,” anasema Dkt. Gordon Okomo, mkurugenzi wa afya wa Kaunti ya Homa Bay.

Hivi karibuni Kenya ilipanua wigo wa utoaji wa chanjo hiyo kwa jamii zaidi katika maeneo ya majaribio, zaidi ya mara mbili ya upatikanaji wa chanjo ya malaria na Wizara ya afya imedhamiria kupanua zaidi wigo wa chanjo hiyo.

Kadiri mchakato wa kimataifa wa kutokomeza malaria unavyoongezeka, nchi nyingi zaidi zimezindua mipango yao ya kutokomeza malaria.
© WHO/Nurbolot Usenbaev
Kadiri mchakato wa kimataifa wa kutokomeza malaria unavyoongezeka, nchi nyingi zaidi zimezindua mipango yao ya kutokomeza malaria.

Kutumia fursa mpya

Ziara za utoaji chanjo ya malaria pia zinaunda fursa mpya kwa wahudumu wa afya kuwaona watoto ambao pengine wasingekwenda kwenye vituo vya afya au hospital na kuwapima kwa ajili ya chanjo nyingine zozote ambazo hazikufanyika.

“Chanjo ya malaria imekuwa fursa ya kutusaidia kufuata wateja na kuboresha utowaji wa chanjo nyingine,” anasema Maureen Atieno, muuguzi msimamizi wa kliniki ya afya ya uzazi na mtoto, katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Homa Bay.

Ameongeza kuwa "Unapofuatilia chanjo ya malaria tunaweza kutambua watu ambao wamekosa chanjo nyingine, ikiwa ni pamoja na za surua na rubella."

Kuangalia mbele

Mmbali ya Kenya, mahitaji ya chanjo ya malaria ni makubwa mno. Angalau nchi 28 barani Afrika zinapanga kutuma maombi ya msaada wa muungano wa chanjo duniani Gavi kupeleka chanjo hiyo.

Usambazaji wa chanjo wa awali ni mdogo na utatolewa kulingana na mfumo unaoweka kipaumbele cha dozi za awali kwa watoto wanaoishi katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Kadiri usambazaji unavyoongezeka ili kukidhi mahitaji, chanjo itawafikia watoto wengi zaidi, ndani na katika nchi zenye ugonjwa huo.

Kuongezeka kwa usambazaji ili kupata manufaa kamili ya chanjo ni kipaumbele kwa WHO, Gavi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na washirika wengine wa chanjo.