Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi nchi yafungua dimba Afrika kutumia chanjo mpya ya majaribio dhidi ya Malaria:WHO

Mtoto akichanjwa
PATH
Mtoto akichanjwa

Malawi nchi yafungua dimba Afrika kutumia chanjo mpya ya majaribio dhidi ya Malaria:WHO

Afya

Malawi inakuwa nchi ya kwanza kati ya nchi tatu za Afrika kuanza kutumia chanjo mpya ya majaribio dhidi ya malaria, imesema taarifa ya shirika la afya duniani WHO iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi.

WHO imesema imeukaribisha uzinduzi wa chanjo hiyo ya kwanza katika programu ya majaribio duniani. Chanjo hiyo inayofahamika kama RTS,S itakuwepo kwa ajili ya watoto wa umri wa miezi mitano hadi miaka miwili nchini Malawi, Ghana na Kenya zitafuatia katika wiki chache zijazo.

WHO inasema malaria inasalia kuwa moja ya magonjwa yanayoongoza kwa kusababisha vifo ulimwenguni na kila dakika mbili ugonjwa huo unasababisha kifo kwa mtoto mmoja duniani. Vifo vingi zaidi vinatokeaa barani Afrika ambako zaidi ya watoto 250,000 wanakufa kutokana na ugonjwa huo kila mwaka. Watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wako hatarini zaidi. Duniani kote malaria inaua watu 435, 000kila mwaka, wengi wao wakiwa watoto. 

 

Mlinda amani wanayehudumu nchini Sudan Kusini akihudumia mwanamke mjamzito anayeugua malaria.Watoa huduma wakati mwingi ni walengwa wa mashamubulio
UNMISS
Mlinda amani wanayehudumu nchini Sudan Kusini akihudumia mwanamke mjamzito anayeugua malaria.Watoa huduma wakati mwingi ni walengwa wa mashamubulio

Mkurugenzi mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, “tumeshuhudia mafanikio makubwa kuanzia kwenye vyandarua na hatua nyingine za kudhibiti Malaria katika kipindi cha miaka 15 lakini maendeleo yamerejea nyuma katika baadhi ya maeneo. Tunahitaji masuluhisho mapya kurejesha vita ya dhidi ya Malaria kwenye mstari, na chanjo hii inatupa matumaini ya kufikia huko. Chanjo ya Malaria ina uwezo wa kuokoa maelfu ya maisha ya watoto.”

Imewachukua watalaamu miongo mitatu kuijaribu chanjo hiyo ya RTS,S ambayo WHO inaitaja kuwa ya kwanza hadi sasa ikiwa ya pekee ambayo imeonesha kuwa inaweza kupunguza visa vya malaria kwa watoto. Katika majaribio ya maabara, chanjo hiyo imeonesha kuweza kukinga takribani visa vinne kati ya kumi vya malaria ikiwemo visa vitatu kati ya kumi vya malaria Kali inayotishia maisha.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt Matshidiko Moeti amesema, “malaria ni tishio la mara zote katika jamii za kiafrika ambako chanjo hii itatolewa. Watoto maskini wanaathirika zaidi na wanakabiliwa na kifo. Tunafahamu uwezo wa chanjo kuzuia magonjwa na kuwafikia watoto wakiwemo wale ambao wanaweza wasiwe na nafasi ya kuvifikia vituo vya afya.”

Chanjo hii ya malaria inalenga kuwafikia takribani watoto 360,000 kwa mwaka katika nchi tatu.