Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajasiriamali wanawake kwenye mizozo wanahitaji usaidizi wa kimkakati na si misaada

Picha ya pamoja ya washiriki wa Mkutano wa 5 wa Umoja wa Mataifa kuhusu uwekezaji kwa wajasiriamali (WEIF) huko Manama, Bahrain.
UN News/Abdelmonem Makki
Picha ya pamoja ya washiriki wa Mkutano wa 5 wa Umoja wa Mataifa kuhusu uwekezaji kwa wajasiriamali (WEIF) huko Manama, Bahrain.

Wajasiriamali wanawake kwenye mizozo wanahitaji usaidizi wa kimkakati na si misaada

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Suala la kuwekeza kwa wanawake wajasiriamali kwenye maeneo yenye mizozo duniani limepatiwa uzito hii leo mwishoni mwa mkutano wa 5 wa Umoja wa Mataifa kuhusu uwekezaji kwa wajasiriamali, WEIF 2024 huko Manama, mji mkuu wa Bahrain, jukwaa lililoratibiwa na Umoja wa Mataifa na wadau wake.

Wanawake kutoka Afghanistan, Algeria, Gaza, Iraq, na Sudan walishiriki kwenye jopo mahsusi na kusema kuwa uwekezaji wa aina hiyo umekuja wakati muafaka kwani utazidi kuzijengea utulivu, matumaini jamii zinazowategemea.
 
Umuhimu wa uwekezaji kwa wanawake wajasiriamali kwenye maeneo ya mizozo umetajwa na UNIDO kuwa ni mafanikio makubwa ya WEIF 2024.
 
Nafikiri mafanikio makubwa zaidi ya WEIF 2024 ni kwamba tumeileta na kuishirikisha jamii ya kimataifa kutambua na kuelewa matatizo, machungu ya wanawake walioko kwenye mizozo na ni kwa jinsi gani tuwasaidie,” amesema Dkt. Hashim Hussein, Mkuu wa ofisi ya shirika hilo ya kusongesha Teknolojia na Uwekezaji, ITPO nchini Bahrain.
 
Amesema si kwa kuwapatia msaada bali kupitia maendeleo ya kiuchumi, kuhakikisha wanaendeleza familia zao na bila shaka na jamii na nchi wanamoishi. Nafikiri haya yatakuwa ndio mafanikio yetu makubwa ya WEIF 2024.
Tahani Abu Daqqa (kwenye skrini,) mfanyabiashara Mpalestina kutoka Gaza.
UN News/Abdelmonem Makki
Tahani Abu Daqqa (kwenye skrini,) mfanyabiashara Mpalestina kutoka Gaza.

Vita huvuruga miradi ya kusaidia jamii Gaza

Tahani Abu Daqqa, mfanyabiashara mwanamke kutoka ukanda wa Gaza amekuweko eneo hilo kwa miezi 7 sasa tangu kuanza kwa vita. Aliondoka ukanda huo wiki tatu zilizopita lakini wakati akitaka kurejea hakuweza Kwani kivuko cha Rafah kilifungwa na hivyo kupata fursa ya kuja Manama kushiriki WEIF.
 
Akiwa mpalestina wa kwanza mwanamke kufungua viwanda ikiwemo cha nguo na biskuti kama njia ya kujenga fursa ya ajira kwa wanawake badala ya kuondoka na kwenda nje ya Gaza, Tahani anasema juhudi zake zimekuwa zinagonga mwamba.
 
Vita inayojirudia tangu mwaka 2007 imekwamisha miradi yake. “Mradi wa mazingira wa mfuko wa Damour unaohusika usafishaji wa majitaka na kupatiwa nishati kupitia sola. Mradi mwingine wa Life for Renewable Energy ambao ulikamilika kwa changamoto nyingi lakini ukikaribia kukamilika, mradi ulishambuliwa na kuharibiwa. 

Kujenga mahema kwa wakimbizi Gaza

Baada ya vita kuanza Oktoba 2023, kila kitu kilibadilika, anasema “na ghafla nilikimbilia eneo karibu na bahari, ningaliweza kupata nyumba ya kuishi lakini wanawake wanawake na watoto walikuwa wanaishi mtaani huku mvua ikiwanyeshea. Hatukuwa na chochote, hakuna benki, hakuna fedha, kila kitu kimekwenda.”
 
Nilikuwa na deni la dola 500,000 lakini nilisahau shida zote nikikumbuka watoto na wanawake wanaoala nje.  Nilianza kununua mbao, na kukusanya jamaa na watu wa kujitolea na kuanza mahema usiku na mchana.
 
Anasema  marafiki zake wa kiyahudi walichangia dola 5,000 aondoke Gaza lakini alitumia fedha hizo kujengea watu mahema.
 
Taani anasema suala la kuwekeza kwa mwanamke mjasiriamali katika eneo la mizozo ni sahihi kwani wanawake ndio watekelezaji.
[Kushoto kwenda kulia] Alaa Hamadto, mama wa Sudan mwenye watoto watatu wa kike, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Solar Food; Tahani Abu Daqqa, mfanyabiashara Mpalestina kutoka Gaza; Malalai Helmandi, Afisa Mkuu Uendeshaji wa shirika la kuzalisha ni…
UN News/Abdelmonem Makki
[Kushoto kwenda kulia] Alaa Hamadto, mama wa Sudan mwenye watoto watatu wa kike, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Solar Food; Tahani Abu Daqqa, mfanyabiashara Mpalestina kutoka Gaza; Malalai Helmandi, Afisa Mkuu Uendeshaji wa shirika la kuzalisha nishati ya jua Helmandi Sola.

Maisha na Ndoto za wasudan ni muhimu

Alaa Hamadto, mama huyu wa watoto watatu kutoka Sudan ni Afisa Mtendaji Mkuu na Muasisi wa kampuni ya Solar Food, kampuni ya teknolojia salama ya kukausha vyakula kwa kutumia nishati ya jua.
 
Vyakula vinavyokaushwa havijaongezwa dawa yoyte na huuzwa jumla na rejareja. Kiwango cha Alaa kilisambaratishwa kutokana na vita inayoendelea Sudan.
 
“Tulikuwa tunauza nje ya nchi bidhaa zetu ikiwemo Uingereza, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu na Qatar. Ofisi yangu ilikuwa ndani ya kiwanda nchini Sudan,” amesema Alaa.
 
Anasema ndoto yake ilikuwa kuleta mabadiliko Chanya kwenye maisha ya watu na hilo lingalifanikiwa kupitia usaidizi kwa wakulima wadogo. Nataka pia kusaidia kusambaza faida za ukaushaji wa vyakula kwa kutumia Nishati ya jua.
 
Kwa bahati mbaya vita ilipoanza Alaa alipoteza kila kitu. “Maisha ya wasudani ni muhimu, vivyo hivyo ndoto zao,” amesema Alaa akiongeza kuwa kila mtu anasema kinachoendelea Sudan ni vita ya kikabila lakini ni vita ya kugombani mali iliyogeuka kuwa ya kikabila.”
 
Baada ya vita Alaa alikimbilia Misri, lakini baada ya muda aliamua kurejea na kusalia Sudan. “ Niliamua kurejea Sudan kuanzisha kiwanda cha kukausha mazao lakini ni vigumu sana kufanya kazi tena Sudan kutokana na ukosefu wa usalama, mfumuko wa bei na uhaba wa vifaa.
 
Hata hivyo licha ya changamoto, watu wa Sudan wameonesha mnepo, “nafikiri tunajenga mnepo. Tunafahamu hakuna mtu atakuja kutuokoa n ani juu yetu kunyanyuka na kuendelea,” ametamatisha Alaa. 
Malalai Helmandi, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa shirika la kuzalisha nishati ya jua la Helmandi Solar nchini Afghanistan, na mumewe Hamid Helmand, Mkuu wa kampuni hiyo.
UN News/Abdelmonem Makki
Malalai Helmandi, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa shirika la kuzalisha nishati ya jua la Helmandi Solar nchini Afghanistan, na mumewe Hamid Helmand, Mkuu wa kampuni hiyo.

Vita Afghanistan imevuruga mfumo wa uthabiti wa mwanamke

Malalai Helmandi, Afisa Operesheni Mkuu wa shirika la kuzalisha nishati ya jua au sola nchini Afghanistan Helmandi Solar na mume wake Hamid Helmand kwa muda wa miaka miwili wamekuwa wakitekeleza miradi ya kuinua wanawake kwenye taifa hilo la Asia.
 
Amesema kwa kipindi cha miaka miwili na nusu kampuni yao inaandaa mabanda ya bustani kwa ajili ya wanawake hao walioathiriwa na vita.
 
Anasema miaka 47 ya vita nchini Afghanistan imedhoofisha jukumu la mama kama mhimili wa nyumba. “Yeye ndio anatumia muda wake mwingi wakati wa makuzi ya mtoto. Na katika utamaduni wa Afghanistani muungano wa familia ni thabiti. Kwa hiyo naona zile familia ambazo mama amewezeshwa, na ana ufahamu, amepatiwa mbinu ya kujipatia kipato, au hata kwa kiwango kidogo yuko kwenye nafasi ya kupitisha maamuzi, hizi ni familia ambazo ninaona hata watoto wao wanakuwa na mtazamo tofauti kuhusu maisha kuliko mtu ambaye hata hafahamu nini kinaendelea kwa hiyo hawezi kumshawishi mtoto wake aende kwenye mwelekeo ambao hautasaidia jamii.”
 
Bwana Helmand anasema ni kwa mantiki hiyo baada ya siku tatu za WEIF 2024 anachorejea nacho nyumbani ni kwamba, “Na sasa kwa juhudi na fikra zetu nadhani tunaweza kurejesha hayo majukumu na kazi kwa wanawake kwani asilimia 80 ya wanawake hao wamepoteza kazi zao kwa sababu ya vita na kwa sababu ya kilichoendelea kwenye eneo hilo.”
 
Mwaka 2018 Iraq ilikuwa kwenye mzozo na kundi la wanamgambo wa ISIS lakini mazingira hayo hayakumzuia Basima Abdulrahman, Muasisi na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya KESK, inayosaka majawabu ya nishati salama kupitia teknolojia na kujikuta anatekeleza kile alichopenda cha kuwa na kampuni endelevu.
Basima Abdulrahman, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KESK.
UN News/Hisae Kawamori
Basima Abdulrahman, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KESK.
 
“Niliamua kujenga biashara endelevu kwa sababu nilikuwa napenda uendelevu na sikujua kuwa nilikuwa ninaenda kuanzisha kampuni ya kulinda mazingira,” amesema Basima akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa akisema hakuogopa mzozo uliokuwa unaendelea kwani mabadiliko ya tabianchi ni kitisho kikubwa kama ilivyo ISIS “hivyo mapambano hayo lazima yaende pamoja na sio yafanyike kwa mpangilio maalum na ndio nikaamua kuwa si mapema bali inaweza kuchelewa.”
 
Anaamini kuwa kwa Iraq kuingia kwenye mpito wa nishati jadidifu sio tu mpango kimkakati au sio tu anasa bali ni hitaji kwa sababu kuna uhaba wau meme kwa asilimia 50 na pengo hilo linazibwa kwa jenereta ambazo zinachafua mazingira na hazizibi pengo na zaidi ya yote ni aghali.
 
Basima ana ujumbe kwa wajasiriiamali wanawake kwenye maeneo ya mizozo au hata kwenye maeneo ambamo mfumo dume umejikita kwamba unaweza kuanzisha biashara kubwa na kuikuza, lakini wakati wowote unaweza kuwa na mnepo na thabiti na kusonga mbele licha ya changamoto moto zozote unazokumbana nazo na kuimarisha biashara yako.
 
Pazia la WEIF2024 likikunjwa hapa Manama, Bahrain hadi mwaka 2026 kusubiri WEIF2024, Dkt. Hashim anajivunia kwamba tumeweza kuhakikisha wajasiriamali wanapaza sauti zao. Tumeweza kuona wajasiriamali ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa wana fursa ya kuzungumza, kuwasaidia. Unajua vijana, sasa tunawasikiliza, zamani wao walikuwa ni wasikilizaji tu.