Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugunduzi na ujasiriamali vyaunganisha wahitimu SUA na soko la mazao Dubai

Revocatus Kimario(kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Ushiriki wa Wanafunzi wahitimu wa SUA, SUGECO akizungumza naAssumpta Massoi.
UN News
Revocatus Kimario(kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Ushiriki wa Wanafunzi wahitimu wa SUA, SUGECO akizungumza naAssumpta Massoi.

Ugunduzi na ujasiriamali vyaunganisha wahitimu SUA na soko la mazao Dubai

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la 5 la Kimataifa kuhusu uwekezaji kwa wajasiriamali likianza huko Manama, Bahrain washirki wameweka bayana ni kwa jinsi gani wanatekeleza wito wa Umoja wa Mataifa wa kuchochea ugunduzi na ujasiriamali kama njia mojawapo ya kufanikisha ukuaji uchumi na hatimaye kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Likiwa limeleta zaidi ya washiriki elfu moja wakiwemo wajasiriamali kutoka Afrika na nchi za kiarabu moja ya mada zilizojadiliwa ni ubia endelevu kati ya nchi za kiarabu na za kiafrika, hoja ambayo tayari imeanza kuzaa matunda kati ya wanafunzi na wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo nchini Tanzania, SUA na wafanyabiashara huko Dubai, Falme za kiarabu.

Revocatus Kimario, Mkurugenzi Mtendaji wa Ushiriki wa Wanafunzi wahitimu wa SUA, SUGECO ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa kando ya mkutano huo kuwa kilimo mara nyingi kimeonekana kuwa kimbilio la mwisho kwa wahitimu nchini Tanzania hasa kwa kuzingatia kuwa kiwango cha kuajiriwa kwenye sekta rasmi kimepungua.

“Kwa kutambua hilo tulianzisha SUGECO na wanafunzi tunakuwa nao tangu wakiwa hawajahitimisha masomo yao. Tunaatamia mawazo yao na ubunifu wao,” amesema Bwana Kimario akigusia hoja hiyo ya kuatamua ambayo shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya viwanda, UNIDO linasema ni muhimu ili kuhakikisha ubunifu au hoja za vijana hazifii njiani.

Alipoulizwa wana ugunduzi wa aina gani? Bwana Kimario anasema, “tumebahatika kuwa na vijana waliobahatika kuwa na fursa ya elimu. Na vijana wanajaribu kufanya mambo mengi kwa njia tofauti tofauti .Mfano namna ya kutumia teknolojia teknolojia ya jua au zilizowazunguka kuzalisha bidhaa. Ukija pale kwenye kituo chetu cha SUGECO utaona sasa hivi tumekuja na mfumo wa uzalishaji wa mazao kwa kutumia maji, lakini maji hayo tunayasukuma kwa nishati ya sola au jua na kisha yanakwenda kwenye hifadhi na baadaye tena yanarejea shambani. Hii ni sehemu ya moja ya ugunduzi kwani tumebadilisha mfumo ambao watu walikuwa wamezoea. Na tumesaidia watu wengi kutumia maji machache lakini kuzalisha bidhaa nyingi.”

Kupitia SUGECO, kinachofanyika ni kubadilisha fikra za wanafunzi waanze kuona kilimo kama fursa rasmi na sio fursa mbadala na wanafundisha pia kuongeza thamani kwenye bidhaa na ubunifu. “Mfano sisi sasa hivi tunatumia viazi lishe kutengenezea mikate badala ya kutegemea tu unga wa ngano,” amesema Bwana Kimario.

SUGECO pia inasadia SUA kuongeza thamani kwenye tafiti zinazofanywa na wataalamu wa SUA, “ziko tafiti nyingi zinazofanywa na wataalamu wetu, lakini sasa ni kwa vipi tutatumia tafiti hizo kuzigeuza kuwa biashara hiyo ni moja ya maeneo tunayomulika. Kwa hiyo tunauganisha kati ya wanazuoni wanaofanya hizo tafiti na vijana wanaotaka kutumia tafiti zinazofanyika kufanyia biashara.”

Alipoulizwa UNIDO imewasaidia namna gani, Bwana Kimario amesema imewawezesha kusafiri hadi Manama na kuweza kuwasilisha fursa za kilimo na bidhaa zilizoko Tanzania hasa mazao ya bustani mfano tikitimaji ambalo wamepata fursa ya soko Dubai. “Tumepata soko Dubai. Wao walikuwa wanahangaika kuwa wakitoa zao hilo Brazil wanatumia hadi siku 45 kufika Dubai. Lakini wakitoa Tanzania ni kati ya siku 18 hadi 21, sasa kwetu hapa ni fursa. Nan dio nimekuja hapa kuwasilisha fursa hiyo.”

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa SUGECO amesema wakulima latembee kifua mbele kwani kilimo ndio bidhaa inayouzika zaidi duniani. “Tatizo ni kwamba wakulima bado hawajajua thamani yao, kwani bila mkulima hakuna uhai.”