Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu walioondolewa Rafah wafikia 360,000 huku UN ikitoa ombi la dola bil 2.8 kusaidia Gaza na Ukingo wa Magharibi

Wananchi wa Kipalestina katika ukanda wa Gaza wanakimbia tena huku wanajeshi wa Israel wakizidisha mashambulizi ya mabomu Rafah.
© UNRWA
Wananchi wa Kipalestina katika ukanda wa Gaza wanakimbia tena huku wanajeshi wa Israel wakizidisha mashambulizi ya mabomu Rafah.

Watu walioondolewa Rafah wafikia 360,000 huku UN ikitoa ombi la dola bil 2.8 kusaidia Gaza na Ukingo wa Magharibi

Msaada wa Kibinadamu

Takriban watu 360,000 wamekimbia eneo la Rafah katika wiki iliyopita huku kukiwa na mashambulizi yanayoendelea ya wanajeshi wa Israel ambayo yamelemaza uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu na inaaminika yamemuua mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X UNRWA wameandika kuwa "Takriban watu 360,000 wamekimbia Rafah tangu amri ya kwanza ya kuhamishwa wiki moja iliyopita," wakirejelea vipeperushi vilivyosambazwa na jeshi la Israeli kuamuru wale walioko mashariki mwa Rafah kuondoka kwenye makazi yao.

Katika tahadhari nyingine, UNRWA ilionya kuhusu " vikwazo wa kibinadamu zimezuia" kufikia eneo lote la Ukanda wa Gaza ambalo sasa ni "suala la maisha au kifo" kwa Wagaza ambao tayari wanakabiliwa na "mashambulio ya mabomu na ukosefu wa uhakika wa upatikanaji wa chakula".

Haya yanajiri wiki moja tangu jeshi la Israel lisonge mbele na mashambulizi yake ya kijeshi huko Rafah, kutwaa udhibiti wa upande wa Gaza wa kivuko cha mpaka cha Rafah na kivuko cha Kerem Shalom.

"Tunahitaji mara moja na kwa haraka kupita kwa usalama kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu na wafanyakazi," shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilisisitiza, huku kukiwa na ripoti mpya za mapigano zaidi na mashambulizi ya makombora katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa eneo hilo.

"Mashambulio ya mabomu na maagizo mengine ya kuwahamisha yamesababisha uhamaji na hofu zaidi kwa maelfu ya familia" kaskazini, UNRWA ilisema. “Hakuna pa kwenda. HAKUNA usalama bila kusitishwa kwa mapigano."

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia liliripoti hii leo kuwa mfanyakazi mwingine aliuawa huko Gaza, na kufanya jumla ya wafanyakazi waliouawa katika vita hivyo kufikia 188.

Mtu huyo - afisa mkuu wa miradi mwenye umri wa miaka 53 - aliaminika kufa katika shambulio la Israeli katika mji wa kati wa Deir Al Balah, baada ya kuondoka Rafah. "Ameacha mke na watoto wanne," shirika hilo lilisema.

 

OCHA na ombi la fedha

Katika tukio jingine linalohusiana na hilo, Umoja wa Mataifa umetoa ombi la dola bilioni 2.8 kwa ajili ya kusaidia zaidi ya watu milioni tatu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi katika kipindi cha miezi minane ijayo.

“Kwa miezi kadhaa, wanawake na watoto wameuawa kwa kasi inayozidi vita vyovyote katika karne hii. Na wale ambao wameepuka kifo na majeraha sasa wana hatari ya kupoteza maisha kwa sababu ya ukosefu wa chakula, maji safi na salama, dawa na huduma za afya," amesema Joyce Msuya, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Naibu Mratibu wa Misaada ya Dharura OCHA.

Akizungumza akiwa nchini Kuwait, Bi. Msuya alieleza jinsi kila siku, "wengi wa wanawake hujifungua katika mazingira ya kutisha, mara nyingi bila ganzi au msaada wa matibabu, huku mabomu yakilipuka karibu nao".

"Akina mama hutazama watoto wao wakifia mikononi mwao kwa sababu hawana maziwa ya kutosha kuwaweka hai. Na watoto wanakufa kwa sababu hawana chakula au maji ya kutosha.”

Yapo mengi yanayoweza kufanya

Baada ya zaidi ya miezi saba ya vita, takriban watu 35,000 wameuawa, kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza. Wengine 70,000 zaidi wamejeruhiwa au kutoweka, na wengine wengi wamenaswa chini ya vifusi.

Kuendelea kutolewa kwa ufadhili kunahitajika haraka ili kuwasaidia wale wanaotegemea misaada ya kibinadamu kuendelea kuishi, afisa huyo mkuu wa OCHA alisema, akisisitiza kwamba hata bila ya kusitishwa mapigano, "bado kuna mengi tunaweza kufanya kutokana na mazingira yanayofaa".

Bi. Msuya amebainisha kuwa "Tuko katika mazungumzo ya kila siku na pande zinazhohusika. Tunaratibu mwitikio wa kibinadamu…Tumewatoa watu kutoka kwenye vifusi na kurejesha miili ya wafanyakazi wa misaada, ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya kazi katika shirika lisilo la kiserikali la World Central Kitchen na Médecins Sans Frontières ambao waliuawa wakiwahudumia wenye uhitaji.

Maoni ya afisa huyo wa OCHA yalikuja wakati ofisi ya uratibu wa misaada iliripoti ubomoaji mpya wa majengo ya Wapalestina katika Kambi ya Al'Arrub katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Hebron.

Takwimu za hivi karibuni kutoka kwenye tovuti ya mtandaoni ya OCHA zinaonesha kuwa miundombinu 435 imeharibiwa au kuharibiwa kote Ukingo wa Magharibi mwaka huu, na kusababisha watu 824 kuyahama makazi yao.