Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Msaada kwa mateka waliookolewa huku Tedros anaonya juu ya bahari ya uhitaji

Mpalestina aliyejeruhiwa akitibiwa katika Nasser Medical Complex katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza. (Maktaba)
© WHO
Mpalestina aliyejeruhiwa akitibiwa katika Nasser Medical Complex katika mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza. (Maktaba)

Gaza: Msaada kwa mateka waliookolewa huku Tedros anaonya juu ya bahari ya uhitaji

Msaada wa Kibinadamu

Huku leo kukiwa na ripoti kwamba mateka wawili wameokolewa wakati wa uvamizi wa kikosi maalum cha Israel katika mji wa Rafah, mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO ameonya kwamba mgogoro wa kibinadamu unaoendelea Gaza bado haujakabiliwa na wala kufikia hatua yoyote ya msaada unaotosheleza. 

Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema "Hadi sasa, tumewasilisha tani 447 za vifaa vya matibabu kwa Gaza, lakini ni tone tu katika bahari ya mahitaji, ambayo yanaendelea kuongezeka kila siku." 

Hospitali katika mgogoro mkubwa

Ameongeza kuwa ni hospitali 15 tu kati ya 36 ambazo bado "zinafanya kazi kwa kiasi au kidogo" katika eneo hilo, huku kukiwa na ripoti mpya za kuendelea kwa mashambulizi makali ya jeshi la Israel kusini mwa Gaza ambayo yaliambatana na ujumbe wa uokoaji wa mateka wawili wa Kiisraeli kutoka ghorofa ya pili ya jengo huko Rafah.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO ameendelea kusema kuwa "Wafanyakazi wa afya wanafanya kila wawezalo katika hali isiyowezekana," huku akielezea wasiwasi unaoenea kati ya jumuiya ya kimataifa kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Rafah, "ambapo wakazi wengi wa Gaza wamekimbilia kutoka kwenye uharibifu mkubwa kuelekea kaskazini ." .

Maombi mapya

Tedros amesema hayo katika hotuba yake kwa Mkutano wa Kilele wa Serikali za Dunia huko Dubai na kuongeza kuwa "WHO inaendelea kutoa wito wa kupatikana kwa usalama kwa wafanyikazi wa kibinadamu na vifaa, tunaendelea kutoa wito kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas kuachiliwa na tunaendelea kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano," 

Katika tukio linalohusiana na hilo mwishoni mwa juma, shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, liliripoti kwamba shehena ya chakula kwa ajili ya watu milioni 1.1 imeendelea kukwama kwenye bandari ya Israel kutokana na vikwazo vya hivi karibuni vilivyowekwa na mamlaka ya Israel.

"Takriban makontena 1,049 ya mchele, unga, mbaazi, sukari na mafuta ya kupikia yamekwama huku familia huko Gaza zikikabiliwa na njaa na kutokula," limeandika shirika hilo kwenye ukurasa wake wa X zamani Twitter.

Mateso Rafah

Takriban watu milioni 1.5 sasa wamejificha Rafah, karibu na mpaka wa Misri. Hii ni mara sita ya idadi ya watu waliokuwepo kabla ya vita, limeanainisha shirika la UNWRA katika taarifa yake ya hivi karibuni kuhusu vita hivyo, ambayo ilichochewa na mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas ambayo yalisababisha takriban raia 1,200 wa Israel na kigeni kuuawa na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka tarehe 7 Oktoba mwaka jana.

Pamoja na kuongezeka kwa mashambulizi ya anga huko Rafah, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limeripoti kwamba mapigano makali yameendelea katika na karibu na mji wa Khan Younis kaskazini zaidi, uharibifu wa makao makubwa ya UNWRA kusini mwa eneo hilo, na kituo cha mafunzo cha Khan Younis, ambacho kimewasukuma maelfu ya Wapalestina zaidi kuelekea Rafah.

UNRWA "haitaweza kuendesha operesheni ipasavyo au kwa usalama kutoka kwenye mji unaoshambuliwa na jeshi la Israel," imesema, taarifa ya shirika hilo ikimnukuu Thomas White, Mkurugenzi wa Masuala ya UNRWA huko Gaza.

Ikiangazia hitaji kubwa la kufikishwa zaidi kwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda huo, shirika hilo la Umoja wa Mataifa limebainisha kuwa kivuko cha Kerem Shalom kutoka Israel kilikuwa kimefungwa tangu Jumatano Februari 7 kwa sababu waandamanaji walikuwa wameendelea kukizuia.

"Ugavi muhimu wa kukabiliana na uhaba wa chakula unaendelea kuzuiwa kutokana na kukosekana kwa vibali vya mamlaka ya Israel kuhamisha unga kutoka bandari ya Israel ya Ashdod hadi Ukanda wa Gaza," imebainisha pia ripoti ya UNWRA.