Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gaza: Huko Rafah hofu yatanda, wagonjwa wahofia kusaka huduma

Watu wakichota maji ya kunywa huko Rafah kusini mwa Gaza
© UNRWA
Watu wakichota maji ya kunywa huko Rafah kusini mwa Gaza

Gaza: Huko Rafah hofu yatanda, wagonjwa wahofia kusaka huduma

Afya

Hofu kubwa ikiendelea kutanda huko Rafah, kusini mwa Gaza wakati huu ikiripotiwa kuwa Israel inataka kuelekeza operesheni zake za kijeshi kwenye eneo hilo, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni ,WHO linasema hospitali tayari zimezidiwa uwezo kwani Umoja wa Mataifa umekuwa unasema operesheni hiyo ya kijeshi itasababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi ambao watahitaji huduma za afya.

Kiongozi wa timu ya WHO huko Gaza Dkt. Ahmed Dahir, ameiambia Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa kuwa kwa sasa huko Rafah, kuna hospitali tatu tu ambazo zinafanya kazi ikiwemo ile ya wazazi ya Emirati na kwamba kwa kipindi cha wiki nzima iliyopita, WHO imekuwa inahakikisha zimejiandaa vya kutosha na zimepatiwa vifaa vya matibabu.

Tweet URL

Dkt. Dahir anasema hospitali tayari zimefurika wagonjwa na kutokana na kinachoendelea hivi karibuni, imekuwa vigumu hospitali hizo kufikiwa. Ametoa mfano wa hospitali ya Al-Najjar inayotoa huduma ya kusafisha figo kwa wagonjwa zaidi ya 100.

“Kwa bahati mbaya, hospitali hii ni miongoni mwa hospitali zilizoko kwenye eneo ambalo serikali ya Israeli iliagiza watu waondoke na hivyo wagonjwa wanahofia kusaka huduma,” amesema Daktari huyo wa WHO, Gaza, akiongeza kuwa “tunasikia pia kwamba wagonjwa wengi waliolazwa kwenye hospitali hiyo wanaanza kuondoka.”

Amesisitiza kuwa WHO kila mara imekuwa ikitaka hospitali zilindwe dhidi ya mashambulizi.

“Tumeweka bayana mfumo wa kuwezesha wagonjwa wanaohamishwa waweze kupitia, sasa kama hospitali haziwezi kufikiwa ni nini mbadala?” amehoji Dkt. Dahir, akisema ndio maana wamekuwa wanasaidia ukarabati wa hospitali ya Nasser huko Khan Younis.

Alipoulizwa kuhusu hali ya wajawazito na watoto wachanga waliozaliwa, Dkt. Dahiri amesema hospitali ya wazazi ya Emirati ni moja ya hospitali pekee ya huduma hizo Gaza, ikisaidia kuzalisha watoto zaidi ya 100 kila mwezi.

“Tumekuwa tukihakikisha kuwa hospitali hiyo ina vifaa vyote. Na iwapo tunashindwa kuifikia, basi tunaweza kuwaelekeza wajawazito kwenda mathalani hospitali ya mashinani ya Al Mawasi, na vile vile hospital ya Nasser.”

Mafuta yanaisha

Wakati huo huo, nishati ya mafuta ambayo ni muhimu kwa operesheni za kibinadamu Gaza inaweza kuisha “kesho” na baadhi ya akiba ya chakula inaweza kutosha hadi mwisho wa wiki, amesema Afisa mwandamizi wa misaada ya kiutu kutoka Umoja wa Mataifa huko Mashariki ya Kati.

Andrea de Domenico, ambaye ni mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA kwenye eneo la Palestina linalokaliwa, oPt, amesema kufungwa kwa kivuko cha Rafah kupitia Misri kumekwamisha upatikanaji wa nishati hiyo na kuathiri kuingia kwa misaada ya kibinadamu na mienendo ya watumishi wa kusambaza misaada hiyo.

Akizungumza kutoka Yerusalemu, Bwana de Domenico amesema ukosefu wa mafuta ni hofu kubwa sana kwani wasaidizi wa kiutu wana lita 30,000 tu za dizeli kwa siku ilhali kiwango kinachotakiwa ni lita 200,000 kwa siku.

Kipauembele kinapatiwa sekta ya afya, maji na mawasiliano huku nishati nyingine ikitengwa kwa dharura kufanikisha mienendo ya wafanyakazi. “Hii ina maana kimsingi hatutakuwa na mafuta kesho,” amesema.

“Israeli imetuhakikishia kuwa inafanya kazi kutuletea nishati zaidi na wanatumai kesho tutaweza kupata,” ameongeza afisa huyo wa OCHA akisema tutaona itakavyokuwa na kwamba changamoto itakuwa usambazaji iwapo Rafah itakuwa katikati ya operesheni ya kijeshi.