Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taka ngumu Kakuma zageuka lulu, wakimbizi vipato vyaongezeka- UNHCR

Raphael Bassemi(kulia), mkimbizi kutoka DRC akiwa na wenzake kambini Kakuma Kenya anakusanya taka ngumu za plastiki na kugeuza vifaa vya kuuza katika biashara yake.
© UNHCR/Charity Nzomo

Tabianchi na mazingira

Katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma iliyoko kaskazini magharibi mwa Kenya, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC amegeuza taka ngumu kuwa lulu na hivyo sio tu kuweka usafi kwenye makazi ya kambini, bali pia kuinua kipato chake na cha jamii inayomzunguka.

Ninapoona plastiki naona fursa za ajira! Ni kauli hiyo ya Raphael Bassemi, mkimbizi kutoka DRC akiwa hapa kambini Kakuma akizungumza huku wanawake na wanaume waliovalia maovaroli na glovu na barakoa wakiokota taka. 

Raphael Bassemi, Mkimbizi kutoka DRC akionesha baadhi ya vifaa anavyotengeneza kutoka kwa taka ngumu za plastiki.
© UNHCR/Charity Nzomo
Raphael Bassemi, Mkimbizi kutoka DRC akionesha baadhi ya vifaa anavyotengeneza kutoka kwa taka ngumu za plastiki.

Anasema anafurahi anapoona jamii inashiriki na zaidi ya yote wanawake wasiokuwa na ajira sasa wameajiriwa, "Nilipoanza nilijikita tu kwenye plastiki, lakini ilibainika kuwa kuna takangumu nyingi za kudhibitiwa. Sasa  ninajishughulisha na aina zote za taka.”

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linaonesha taka mbalimbali zikiwemo mifupa ya mafuvu ya ng’ombe, vyuma, seng’eng’e na kadhalika. Sasa amesharejeleza tani zipatazo 100 za takangumu.

"Tunatengeneza rula kwa ajili  ya wanafunzi, vibanio vya kuanikia nguo, sahani za kulia chakula na vikombe vya chai na kahawa. »

Vijana wajasiriamali wakimbizi wakikusanya taka za plastiki ngumu kwa ajili ya kutengeneza vyombo kama vile sahani na vikombe kwa ajili ya kuuza ili kujipatia kipato kambini Kakuma.
© UNHCR/Charity Nzomo
Vijana wajasiriamali wakimbizi wakikusanya taka za plastiki ngumu kwa ajili ya kutengeneza vyombo kama vile sahani na vikombe kwa ajili ya kuuza ili kujipatia kipato kambini Kakuma.

Raphael na wenzake wakiwa kwenye kiwanda hiki alichoanzisha wanapata ugeni ukiongozwa na Dominique Hyde kutoka UNCHR. Baada ya ziara, Bi. Hyde anasema, "Kilichotuvutia ni jinsi wanaweka mawazo yao kwenye hii biashara ili istawi, na pia kushirikisha jamii ipate ajira na hatimaye kipato walipie elimu na umeme. Kama sisi sote tunahitaji kazi, wao wanahitaji kazi, na wao wameanzisha hii ajira wenyewe. »

Sasa Raphael anasema jamii ina furaha naye ana furaha na zaidi  ya yote.

"Ninapoona wanawake  ninaofanya nao kazi wana furaha, nami nina furaha na ninatamani kuchukua hatua zaidi."