Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ataka Israel na Hamas wamalize vita Gaza

Katibu Mkuu António Guterres akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu hali ya Gaza.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu António Guterres akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu hali ya Gaza.

Guterres ataka Israel na Hamas wamalize vita Gaza

Amani na Usalama

Hali huko Gaza ikizidi kuwa mbaya kila uchao, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa viongozi wa Israel na Hamas wanaoshiriki mazungumzo ya kina hivi sasa, wafikie makubaliano ya kusitisha mapigano.

“Kwa ajili ya wananchi wa Gaza, kwa ajili ya mateka na familia zao nchini Israel na kwa ajili ya ukanda wa Mashariki ya Kati na dunia nzima, ninaishawishi serikali ya Israel na viongozi wa Hamas, wafikie makubaliano sasan,” amesema Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani. 

Bwana Guterres ameelezea wasiwasi wake kuwa bila makubaliano, “vita na madhara yake yote kwa Gaza na Ukanda mzima itazidi kuwa mbaya.”

“Wajumbe wote wa Baraza la Usalama, na serikali nyingi, zimeelezea dhahiri kupinga kabisa operesheni hizo. Natoa wito kwa wale wote wenye ushawishi kwa Israel wafanye lolote liwezekanalo kwa uwezo wao kuzuia,” amesema Katibu Mkuu.

Zuia kusambaa kwa mapigano Rafah

Takribani miezi saba imepita tangu mashambulio ya kikatili ya Hamas dhidi  ya Israel na kuibua chuki zinazoendelea hivi sasa.

Wiki za hivi karibuni zimeshuhudia mashambulizi kwenye eneo la Rafah kusini mwa Gaza, ambako zaidi ya watu milioni 1.2 hivi sasa wamesaka hifadhi, bila chakula, huduma za afya an huduma nyingine muhimu huku wakiwa hakuna pahala pa kwenda.

Bwana Guterres amesema iwapo operesheni za kijeshi zitafanyika huko Rafah, “itaibua mwendelezo wa mapigano, na kuua maelfu ya raia na kulazimu mamia ya maelfu ya watu kukimbia.”

Halikadhalika, itakuwa na madhara makubwa kwa wapalestina huko Gaza, na pia machungu kwenye eneo linalokaliwa na Israel la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan, na halikadhalika ukanda mzima.

Mifumo ya afya imeporomoka

Bwana Guterres pia amezugumzia ni kwa vipi vita inasambaratisha mfumo wa afya kwenye eneo hilo lililozingirwa, ambako theluthi mbili ya hospital na vituo vya afya havifanyi kazi, ilihali idadi kubwa ya zilizosalia zimeharibiwa kwa kiasi kikubwa.

“Baadhi ya hospitali zinafanana na makaburi,” amesema Katibu Mkuu akipazia sauti ripoti kuhusu kubainika kwa makaburi ya watu wengi kwenye maeneo kadhaa ikiwemo hospitali za Al-Shifa na Nasser.

Watu wakiwa wamekusanyika nje ya Hospitali ya Al Shifa Gaza ambako kumekutikana makaburi ya halaiki
WHO
Watu wakiwa wamekusanyika nje ya Hospitali ya Al Shifa Gaza ambako kumekutikana makaburi ya halaiki

Makaburi ya halaiki na uwajibikaji

Miili ya watu zaidi ya 390 imeripotiwa kufukuliwa kwenye hospitali ya Nasser pekee, na “kuna simulizi zinazokinzana ya makaburi kadhaa ya halaiki na kwamba baadhi ya watu waliozikwa, waliuawa kinyume cha sheria.”

KatibuMkuu amesema ni muhimu kwa jopo huru la kuchunguza uhalifu kisayansi likaruhusiwa kuingia bila vikwazo maeneo hayo ili kubaini mazingira ambamo kwayo wapalestina mamia ya wapalestina wamepoteza maisha yao na walizikwa au walihamishiwa kwa mazishi.

“Familia za waliokufa au waliopotea wana haki ya kufahamu nini kilitokea, na dunia ina haki ya uwajibikaji kwa ukiukwaji wowote wa sheria ya kimataifa ambao unaweza kuwa ulitokea,” amesema Guterrres.

Epusha njaa inayosababishwa na binadamu

Kwa upande wa kaskazini mwa Gaza, ambako watu wengi walio hatarini tayari wanakufa kwa njaa na magonjwa, Guterres amesihi jamii ya kimataifa “ifanye kwa kadri iwezekanavyo kuepusha njaa inayoweza kuepushwa, njaa ambayo amesema inasababishwa na binadamu.”

Ijapokuwa maendeleo yamepatikana, hatua zaidi zinahitajika, ikiwemo ahadi ya kufungua vivuko viwili vya kuvushia misaada kati ya Israel na kaskazini mwa Gaza, ili msaada iweze kuingizwa kutoka Bandari ya Ashdod na Jordan.

Ukosefu wa usalama ndio kikwazo kikubwa cha kusambaza misaada Gaza, na amesisitiza kuwa misafara yenye shehena za misaada ya kiutu, wafanyakazi na wananchi “hawapaswi kulengwa.”

“Tunakaribishwa usambazaji wa misaada kwa njia ya anga na bahari, lakini hakuna mbadala wa kutumia njia za barabarani,” amesema Katibu Mkuu, kabla ya kutoa wito kwa mara nyingine tena kwa Israel kuruhusu ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa njia salama na bila vikwazo vyovyote huko Gaza, ikiwemo kwa UNRWA.

Pongezi kwa UNRWA

Katibu Mkuu alitamatisha hotuba yake kwa kuangazia UNRWA, ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, akisema “hakuna shirika liwezalo kuchukua nafanye na na kazi yake muhimu inayofanya” likisaidia mamilioni ya wapalestina huko Gaza, Ukingo wa Magharibi, Jordan, Syria na Lebanon.

“Uwepo wa UNRWA kwenye ukanda huo wote ni chanzo cha matumaini na utulivu. Huduma yake ya elimu, afya na nyinginezo zinatoa hisia ya kuweko kwa hali ya kawaida, usalama na utulivu kwa familia na jamii zinazohaha,” amesema Katibu Mkuu.

Shirika hilo limeomba dola bilioni 1.2  kuweza kushughulikia janga la kibinadamu huko Gaza na vile vile kukidhi mahitaji huko Ukingo wa Magharibi ambako ghasia zinazidi kuongezeka.

Kwa kiasi kikubwa, inategemea wahisahi na takribani nchi 16 zimesitisha michango yao mapema mwaka huu kufuatia madai ya Israeli ya kwamba watumishi 12 wa shirika hilo walihusika kwenye mashambulio ya tarehe 7 Oktoba mwaka 2023. Umoja wa Mataifa uliteua chombo huru kikiwa na jukumu la kutathmini juhudi za shirika hilo zinazingatia kanuni za kiutu za kutoegemea upande wowote.

Jopo hilo, likiongozwa na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Catherine Colonna hivi karibuni lilichapisha ripoti yake ambayo ilibaini kuwa “kanuni kadhaa na mifumo pamoja na taratibu zilizoko UNRWA ni ambazo zimeainishwa vema zaidi katika mfumo wa Umoja wa Mataifa.”

Bwana Guterres amesema mpango wa mkakati unaandaliwa ili kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo, na ametoa wito wa ushirikiano kutoka kwa wahisani, nchi ambamo UNRWA inafanya kazi pamoja na wafanyakazi.

Imarisha usaidizi

Wakati huo huo, nchi nyingi zilizokuwa zimesitisha michango yao kwa UNRWA, zimeanza tena kuchangia, na Katibu Mkuu amesema “tuna matumaini kuwa nchi nyingine nazo zitarejea.” Halikadhalika, nchi nyingi zaidi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimechangia UNRWA kwa mara ya kwanza ilihali wahisani binafsi nao hawakuwa nyuma.

Hata hivyo pengo la fedha bado lipo, hivyo amesihi nchi wanachama na wahisani waoneshe ukarimu kwa kutoa ahadi kubwa ili kazi ya shirika hilo iweze kuendelea.

“Huu ni wakati wetu wa kusisitizia matumaini yetu ya michango na jawabu la mataifa mawili kuweko kwa pamoja – hiyo ndio njia endelevu ya kuelekea kwenye amani na usalama kwa Israeli, wapalestina na ukanda mzima,” amesema Guterres.