Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika iliongoza kwa kupatiwa wagonjwa wa COVID-19 viuavijasumu (Antibiotics)- WHO

Harakati za wahudumu wa afya kupatiwa watu chanjo dhidi ya COVID-19 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC (MAKTABA)
© UNICEF/Gwenn Dubourthoumieu
Harakati za wahudumu wa afya kupatiwa watu chanjo dhidi ya COVID-19 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC (MAKTABA)

Afrika iliongoza kwa kupatiwa wagonjwa wa COVID-19 viuavijasumu (Antibiotics)- WHO

Afya

Ushahidi mpya uliotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO unaonesha kuwa wakati wa janga la COVID-19 kulikuweko na matumizi yasiyo ya lazima na ya kupita kiasi ya viuavijasum au antibiotics ambayo huenda yamesababisha kusambaa kwa usugu wa viuavijiumbe maradhi au Antimicrobials.

Taarifa iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na WHO inasema ingawa ni asilimia 8 tu ya wagonjwa waliolazwa kwa ajili ya COVID-19 ndio walikuwa na maambukizi yatokanayo na bakteria au vimelea na hivyo kuhitaji viuavijasumu, takwimu zinaonesha kuwa wagonjwa watatu kati ya wanne sawa na asilimia 75 ya wagonjwa walitibiwa kwa viujavijasumu pengine tu ingaliweza kuwasaidia hata kama haikuwa inahitajika.

Wagonjwa wasio mahututi Afrika walipatiwa viuavijasumu

Matumizi ya viuavijasumu yalikuwa ni kuanzia asilimia 33 kwa wagonjwa ukanda wa Pasifiki Magharibi hadi asilimia 83 ukanda wa Mediteranea Mashariki na Afrika.

Kati ya mwaka 2020 hadi 2022 kitendo cha daktari kuandikia dawa aina ya viuavijasumu kwa wagonjwa kilipungua huko Ulaya na Amerika, ilhali kiliongeza katika nchi za Afrika.

Kwa wastani kiwango kikubwa cha matumizi ya dawa hizo miongoni mwa wagonjwa wa COVID-19 waliokuwa mahututi kilifikia asilimia 81.

Ingawa hivyo kulikuwa na utofauti mkubwa wa utoaji wa dawa hizo kwa wagonjwa ambao hawakuwa mahututi lakini ukanda wa Afrika uliongoza kwa kupatiwa wagonjwa wa kiwango hicho kwa asilimia 79.

Matumizi holela ya viuavijasumu huweza kusababisha usugu wa dawa

“Pindi mgonjwa anapohitaji viuavijasumu, manufaa yake yanazidi hatari zitokanazo na matumizi ya dawa hizo au hatari za kuleta usugu hapo baadaye,” ameesma Daktari Silvia Bertagnolio, Mkuu wa kitengo cha Ufuatiliaji, Ushahidi na uimarishaji wa Maabara WHO.

Amesema “hata hivyo pindi viuavijasumu vinapotumika pale isipo lazima, hazina faida yoyote zaidi ya kuongeza hatari na matumzi yake yanaweza kusababisha kuibuka au kusambaa kwa usugu wa dawa hizo kwa vijiumbe maradhi, au microbes.”

Daktari Bertagnolio  amesema takwimu hizi mpya zinataka sasa kuimarisha matumizi sahihi ya viuavijasumu na kupunguza madhara yasiyo ya lazima kwa wagonjwa na jamii.

Kwa ujumla matumizi ya viuavijasumu hayakuimarisha tiba ya wagonjwa wa COVID-19. Badala yake, inaweza kuwa iliongeza hatari kwa watu ambao hawakuwa na maambukizi ya bakteria au vimelea ikilinganishwa na wale ambao hawakupatiwa dawa hizo wakati wanaugua COVID-19.

Utafiti huu kuchangia kwenye mapendekezo yajayo

Uchambuzi zaidi utafanyika wa takwimu hizi mpya ili ziweze kujumuishwa kwenye mapendekezo yajayo ya matumizi ya viujavijasumu kwa wagonjwa wa COVID-19, kama sehemu ya mwongozo wa tiba dhidi ya ugonjwa huo. Mkutano utafanyika Hispania mwezi ujao.

Na baadaye mwezi Septemba mwaka huu, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na kikao cha viongozi kukubaliana hatua za kupunguza usugu wa viuavijiumbe maradhi kwa ajili ya afya ya binadamu, Wanyama, na sekta ya kilimo pamoja na mazingira, halikadhalika kusongesha uongozi na ufadhili wa fedha ili kupunguza usugu wa dawa hizo au AMR.