Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Upatikanaji sawa na matumizi sahihi ya viuavijasumu kwa wakimbizi na wahamiaji ni muhimu - WHO

Mwanasayansi anajaribu sampuli inayoshukiwa kuwa na sumu ya bakteria.
CDC
Mwanasayansi anajaribu sampuli inayoshukiwa kuwa na sumu ya bakteria.

Upatikanaji sawa na matumizi sahihi ya viuavijasumu kwa wakimbizi na wahamiaji ni muhimu - WHO

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu milioni 1.27 duniani kote hufa kila mwaka kutokana na usugu wa viuavjiumbe maradhi (Antimicrobial Resistance (AMR), imeeleza taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO. 

Miongo kadhaa ya matumizi mabaya na matumizi kupita kiasi ya viuavijasumu na viuajiumbe maradhi vingine, vimefanya dawa hizi zisiwe na ufanisi katika kutibu magonjwa ya kawaida ya kuambukiza, kuharakisha kuibuka na kuenea kwa usugu.  

Uzoefu wa wakimbizi na wahamiaji katika nchi wanazotoka, safari ya uhamiaji, sera za kuingia na kuujumuishwa, na mazingira ya kuishi na kufanya kazi katika nchi inayowapokea yanaweza kuongeza hatari ya watu hawa kupata magonjwa ya kuambukiza na kutoa changamoto kwa uwezo wao wa kupata dawa za kuzuia magonjwa na kutibu magonjwa ipasavyo.  

Ripoti ya nne ya Mapitio ya Ushahidi wa Kimataifa wa WHO kuhusu Afya na Uhamiaji (GEHM), ikichukua ushahidi juu ya upatikanaji wa viuajijasumu muhimu katika wakimbizi na wahamiaji, inakusanya ushahidi juu ya upatikanaji wa dawa muhimu kwa wakimbizi na wahamiaji na kupata kwamba upatikanaji na matumizi kwa watu hawa ni tofauti na huathiriwa kwa kiasi kikubwa na mifumo ya afya ya nchi mwenyeji. Ingawa kiwango cha ufikiaji wao ulimwenguni hakiko wazi, ripoti hiyo inaangazia vikwazo vya kawaida vya mfumo wa afya kufikia na kutumia dawa za kuua viua vijasumu kotekote: muda mrefu wa kusubiri kuonana na daktari, uwezo mdogo wa huduma za afya, gharama kubwa za afya, maagizo yasiyofaa ya matumizi ya dawa, na ukosefu wa nyenzo zilizotafsiriwa au huduma za tafsiri. 

Vikwazo katika kupata huduma za afya na kupata na kutumia viuavijasumu vinaweza kusababisha matumizi yasiyo ya lazima au yasiyo sahihi, ambayo mara nyingi husababisha matokeo duni ya kiafya kwa watumiaji na maendeleo zaidi ya vimelea sugu vya dawa. 

"Baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa wakimbizi na wahamiaji mara nyingi hukimbilia masoko yasiyo rasmi na kujitibu ili kuondokana na vikwazo vya mfumo wa afya katika nchi inayowapokea," anasema Dkt. Santino Severoni, Mkurugenzi wa Mpango wa Afya na Uhamiaji wa WHO. Anaongeza kusema, "Upatikanaji wa dawa za kuua viuavijasumu zilizo salama, zenye ufanisi, nafuu, za ubora wa juu kwa wote, ikiwa ni pamoja na wakimbizi na wahamiaji, ni muhimu katika kukuza afya ya watu hawa na ni muhimu kushughulikia usugu wa dawa  na kudumisha uwezo wa kutibu maambukizi." 

Ripoti hiyo pia inabainisha sera zisizo za afya na mambo ambayo yanatatiza upatikanaji na matumizi sahihi ya viuavijasumu (antibiotics) kwa wakimbizi na wahamiaji, kama vile uzoefu wa awali usioridhisha wa huduma rasmi, na urahisi wa upatikanaji usio rasmi wa dawa hizo. Zaidi ya hayo, makundi haya yanaweza kukumbana na unyanyapaa, hofu ya kufukuzwa kwa sababu ya hali ya uhamaji, au vizuizi vya lugha, na kushindwa kufikia matunzo kwa sababu ya ukosefu wa muda au usafiri na vikwazo vya kifedha. 

TAGS: WHO, Viuavijiumbe maradhi, viuavijasumu, Usugu wa dawa