Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kufanya kazi kwa mazoea ndio ‘mwiba’ wa ukuaji uchumi Afrika – UNECA

Fundi seremala nchini Eritrea akitumia mashine kukata mambo kuwa samani.
UN Eritrea
Fundi seremala nchini Eritrea akitumia mashine kukata mambo kuwa samani.

Kufanya kazi kwa mazoea ndio ‘mwiba’ wa ukuaji uchumi Afrika – UNECA

Ukuaji wa Kiuchumi

Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi barani Afrika, UNECA imetoa ripoti yake inayoainisha mambo ya kuzingatia ili hatimaye kipindi cha mpito kuelekea matumizi ya nishati salama kiweze kuwa cha haki na endelevu.

Ripoti hiyo Mpito wa Haki na Endelevu (JST) barani Afrika imezingatia ukweli kwamba nchi za Afrika zinaweza kukabiliwa na changamoto za kiuchumi, kijamii na kimazingira iwapo zitaendelea kuendesha shughuli zao kimazoea na hivyo ni lazima kufanya marekebisho ya kimsingi.

Ikiwa imezinduliwa huko Addis Ababa, Ethiopia ambako ndiko makao makuu ya UNECA, ripoti inachambua fursa na sera za Afrika zitakazowezesha kujenga mifumo ya kiuchumi ya haki na endelevu.

“Kwa hilo kufanikiwa, nchi za Afrika zinahitaji mipango kamilifu ya maendeleo na mikakati ambayo kimsingi inapanga upya mifumo ya uzalishaji, ulaji, usimamizi, teknolojia, nguvu kazi na fedha,” imesema taarifa kutoka UNECA.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Katibu Mtendaji wa UNECA, Claver Getete amesema kipindi cha mpito kilicho cha haki na endelevu kinachotoa hakikisho la ukuaji wenye kasi, jumuishi na endelevu, pamoja na ukuaji wa sekta ya viwanda vya uzalishaji wa bidhaa mbali mbali na rafiki kwa mazingira, kitasaidia Afrika kufikia kiwango chache cha ustawi.

Paneli za sola zitumiazo jua zinatoa nishati safi inayojali mazingira kwa Wazambia wengi (kutoka maktaba)
ILO/Marcel Crozet
Paneli za sola zitumiazo jua zinatoa nishati safi inayojali mazingira kwa Wazambia wengi (kutoka maktaba)

Bi. Zuzana Schwidrowski, Mkurugenzi wa Idara ya Uchumi Mkuu na Usimamizi katika UNECA, akiwasilisha ripoti hiyo amesema Afrika ina fursa ya kunufaika na JST ikiongozwa na mahitaji ya waafrika wenyewe.

“Mambo kama vile idadi kubwa ya watu ni vijana, ardhi yenye rutuba, vyanzo vingi vya nishati rafiki kwa mazingira, akiba kubwa ya madini muhimu na kuchelewa kufika kwa teknolojia vinaiweka Afrika kwenye nafasi ya kuweka mpito endelevu kimataifa,” amesema Bi. Schwidrowski. 

Hata hivyo Afrika lazima itafsiri JST kulingana an mahitaji na mazingira  yake.

“Kwa kuzingatia ukubwa wa changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi sambamba na kukua kwa pengo la ukosefu wa usawa na umaskini, hakuna muda wa kupoteza, wakati wa kuchukua hatua ni sasa,” amesema Hanan Morsy, Naibu Katibu Mtendaji UNECA anayehusika na Miradi.