Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo jumuishi na endelevu ya viwanda Afrika ndio muarobaini wa SDG’s:UN

Siku ya Viwanda Afrika 2018
UNIDO/banner
Siku ya Viwanda Afrika 2018

Maendeleo jumuishi na endelevu ya viwanda Afrika ndio muarobaini wa SDG’s:UN

Ukuaji wa Kiuchumi

Maendeleo jumuishi na endelevu ya viwanda ni kichocheo cha kufikia ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030 kwa bara la Afrika, umesema Umoja wa Mataifa.

Katika ujumbe maalumu wa siku ya maendeleo ya viwanda barani Afrika hii leo, ambayo hutoa jukwaa la ushirikiano wa kimataifa na majadiliano ya ajenda ya viwanda Afrika, na kuchagiza kuhusu fursa na changamoto zinazohusiana na ubunifu, shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO limesema, uchagizaji wa kuwa na mfumo wenye tahamni wa kusafirisha na kusambaza bidhaa za viwandani ni chachu ya kuinua maendeleo ya viwanda ambayo yataleta ustawi wa kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa shirika hilo, kaulimbiu ya mwaka huu “kuchagiza tahamani ya kikanda ya usambazaji Afrika:njia ya kusongesha mabadiliko ya kimfumo, ukuaji wa viwanda na uzalishaji wa makampuni ya madawa” inatoa fursa muhimu ya kubaini njia bunifu za kupata suluhu na será za kukuza uzalishaji wa makampuni ya madawa barani Afrika katika muktada wa makubaliano ya biashara huria barani humo (AfCFTA) na muongo wa tatu wa maendeleo kwa ajili ya Afrika (IDDA III).

Image
Hapa ni kiwanda cha viatu katika eneo la mashariki kuliko na viwanda vingi nchini Ethiopia, moja ya nchi iliyoangaziwa katika ripoti.(Picha:UNIDO)

 

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiongeza sauti yake katika umuhimu wa siku hii barani Afrika amesema,  maendeleo ya ushindani na endelevu ya sekta ya viwanda vya madawa Afrika yanaweza kusaidia kuchagiza afya na ustawi bora, sanjari na ukuaji endelevu wa uchumi.

Ameongeza kuwa upatikajani wa madawa yenye ubora kwa gharama nafuu kutapunguza changamoto za kiafya, huku uzalishaji, usafirishaji na usambazaji katika kanda hiyo ukitoa tija ya ajira na kuongeza kipato.

Amesisitiza kuwa Kukabiliana na mahitaji ya bara la Afrika kunahitaji mikakati ya ushirika, hususan na sekta binafsi, kuchagiza usafirishaji na usambazaji wa kikanda, kuhakikisha uwekezaji unaohitajika na kuboresha fursa ya ujuzi na teknolojia.”

Kwani amesema mafanikio yatakayopatikana yatasaidia kutoa ajira, kupunguza umasikini, njaa, pengo la usawa, kuwezesha wanawake, kupanua wigo wa fursa kwa vijana, huku yakiboresha afya, kulinda amazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Siku ya maendeleo ya viwanda barani Afrika (AID) mwaka huu inaadhimishwa kimataifa kwenye makao makuu ya UNIDO mjini Vienna , Austria kwa msaada wa tume ya Umoja wa Mataifa ya uchumi barani Afrika UNECA, tume ya Muungano wa Afrika AUC na ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.