Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama saidieni wanawake wa Sudan kupambana na ukatili katika mizozo

Wanawake wakiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani Sudan. (Maktaba)
© UNOCHA/Ala Kheir
Wanawake wakiwa katika kambi ya wakimbizi wa ndani Sudan. (Maktaba)

Baraza la usalama saidieni wanawake wa Sudan kupambana na ukatili katika mizozo

Haki za binadamu

Wakati wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijiandaa na mjadala wa wazi hapo wiki ijayo kuhusu ukatili wa kijinsia katika maeneo yenye migogoro, wameombwa kutuma ujumbe usio na shaka chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu kuwa raia wa nchini Sudan lazima walindwe na kamwe wasitendewe vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ambavyo vinajumuisha uhalifu wa kivita. 

Taarifa ya pamoja iliyotolewa hii leo jijini New York Marekani na viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa Pramila Patten ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili wa Kingono kwenye mizozo, na Joyce Msuya ambaye ni Naibu Mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa OCHA, imeeleza kuwa ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuanza kwa mzozo nchini Sudan wameomba ushirikiano zaidi wa kimataifa katika kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana nchini humo.

“Matendo haya ya kinyama, ambayo yanafanana na mambo ya kutisha yaliyoshuhudiwa huko Darfur miongo miwili iliyopita, lazima yachochee hatua za haraka.” Wameeleza viongozi hao. 

Ripoti za unyanyasaji wa kijinsia zinaonesha athari zisizo sawa za vita kwa wanawake na wasichana ikiwemo uwepo wa madai ya ubakaji, ndoa za kulazimishwa, utumwa wa ngono, na usafirishaji haramu wa wanawake na wasichana hasa katika maeneo ya Khartoum, Darfur na Kordofan. 

Viongozi hao wa ngazi za juu ya wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa mamilioni ya raia wako hatarini hasa wanapokimbia maeneo yenye migogoro kutafuta hifadhi ndani na nje ya nchi ya Sudan. 

Wamesema kuwa ukubwa halisi wa mgogoro bado haujajulikana na kumekuwa na viwango vidogo vya kuripoti matukio ya kikatili kwa kuogopa unyanyapaa na kutokuwa na imani na taasisi za kitaifa.

“Bila ya kuongeza utashi wa kisiasa na ufadhili wa kifedha kusaidia wale walio mstari wa mbele hasa mashirika yanayoongozwa na wanawake katika kutoa huduma za kuokoa maisha msaada utaendelea kupungua.” Imesema taarifa hiyo ambayo imeeleza kinachotakiwa ni “Ufadhili kamili wa mpango wa mahitaji na majawabu ya kibinadamu kwa nchi ya Sudan ambayo mpaka sasa imepata ufadhili wa asilimia 10 pekee.”

Ukipatikana ufadhili huo utasaidia wale walionusurika na kuunga mkono hazina kubwa ya wadau mbalimbali wa Umoja wa Mataifa katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia yanayohusiana na migogoro.