Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN yapokea ripoti za raia kuuawa na wanawake kubakwa nchini Sudan

Wakimbizi kutoka Sudan wakisubiri kupokea vifaa muhimu vya msaada kakati wa usambazaji huko Koufroun, kijiji cha Chad karibu na mpaka wa Sudan.
© UNICEF/Donaig Le Du
Wakimbizi kutoka Sudan wakisubiri kupokea vifaa muhimu vya msaada kakati wa usambazaji huko Koufroun, kijiji cha Chad karibu na mpaka wa Sudan.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN yapokea ripoti za raia kuuawa na wanawake kubakwa nchini Sudan

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binaadamu, OHCHR imeeleza kusikitishwa na athari mbaya kwa za mapigano kwa raia zinazoendelea nchini Sudan ambapo mpaka hizi sasa wamepokea taarifa za kuuawa kwa raia ikiwemo watoto na wajawazito, ubakaji huku waandishi wa habari wakiwa katika hali mbaya kutokana na matamshi ya chuki hususani mitandaoni.

 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini Geneva Uswisi msemaji wa Ofisi hiyo ya Haki za Binadamu Jeremy Laurence amesema.

“Kwa wiki hii pekee limetokea shambulio katika soko la mifugo lenye shughuli nyingi katika mji mkuu Khartoum lilisababisha vifo vya raia wanane, miongoni mwao takriban watatu wanatoka familia moja. Mashambulizi ya anga kwenye soko la Al-Muwaliyyah tarehe 7 Juni yalidaiwa kutekelezwa na Jeshi la Sudan.”

Watoto, wajawazito na wakimbizi wauawa

Jeremy pia alizungumzia tukio la mtoto kuuawa akiwa nyumbani kwao

“Tulipokea taarifa za mauaji ya raia wengine wanne mjini Khartoum tarehe 5 mwezi huu wa Juni, siku moja kabla yani tarehe 4 Juni angalau raia watatu, wote wa familia moja, akiwemo mwanamke mjamzito, waliripotiwa kuuawa. Siku hiyo hiyo, yalifanyika mashambulizi ya angani karibu na Uwanja wa michezo kusini mwa Khartoum ambayo yalipiga kituo cha wakimbizi, ambapo huko inaripotiwa yakiripotiwa kuwauakwa takriban wakimbizi 10.

Watoto wasiopungua 71 wamefariki katika kituo cha kulelea watoto yatima mjini Khartoum tangu mapigano yaanze kutokana na ukosefu wa misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya matibabu.

Waandishi wa habari

Kuhusu ripoti za unyanyasaji wa kingono msemaji wa OHCHR amesema.

“Tangu mapigano yalipoanza, Ofisi yetu imepokea ripoti za kuaminika za matukio 12 ya unyanyasaji wa kingono yanayohusiana na mzozo huo, dhidi ya angalau wanawake 37, ingawa idadi inaweza kuwa kubwa zaidi. Katika angalau matukio matatu, waathirika walikuwa wasichana wadogo. Katika kisa kimoja, wanawake 18 hadi 20 waliripotiwa kubakwa.”

Shirika hilo pia limeeleza kumekuwa na ripoti zinazotia wasiwasi za watu kutoweka na wengine kuwekwa vizuizini kiholela.

Waandishi wa habari nao wapo katika hatari kubwa huku kukiwa na ongezeko la matamshi ya chuki mtandaoni na taarifa za upotoshaji.

“Ofisi yetu imefahamu kuhusu orodha inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwashutumu wanahabari fulani kuwa wafuasi wa RSF. Tumeona maoni kwenye Facebook yakitaka kuuawa kwa wanahabari kwenye orodha hiyo,” ameeleza msemaji huyo wa OHCHR

Shirika la Umoja wa Mataifa la Haki za binadamu limesisitiza wito wake kwa pande zote mbili kwenye mapigano kuhakikisha ulinzi wa raia na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu. 

Wameeleza ni lazima pia wahakikishe ukiukaji wote unachunguzwa kikamilifu na kwa uhuru na wale waliohusika wanawajibishwa.