Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

M23 wanaendelea kutekeleza ukatili Kivu Kaskazini: Türk

Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
MONUSCO/Sylvain Liechti
Wapiganaji wa M23 wakielekea Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

M23 wanaendelea kutekeleza ukatili Kivu Kaskazini: Türk

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amehitimisha ziara yake rasmi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC mjini Kinshasa jana Alhamisi 18 Aprili. 

Katika siku yake ya mwisho ya ziara kwenye mji mkuu wa DRC Kinshasa, alikutana na Rais Félix Tshisekedi na wajumbe wakuu wa Serikali.

Hii ilikuwa ni ziara yake ya kwanza katika nchini DRC kama Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, ingawa amekuwa hapo mara kadhaa awali. 

Akiwa nchini humo alipata fursa ya kusafiri hadi mikoa ya mashariki mwa nchi, ambako alitembelea kambi mbili za wakimbizi wa ndani au IDPs huko Bunia na Goma na kukutana na waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia.

Türk akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mwishoni mwa ziara  yake, amesema "Jimboni Kivu Kaskazini, kundi lenye silaha la wapiganaji wa M23 linaendelea kuzusha ugaidi, kuua na kuwateka nyara watu wengine wakimbizi wa ndani, na pia mara kwa mara kulenga watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na viongozi wa kijamii na watoto wanaandikishwa kwa nguvu katika safu zao za kijeshi."

Wanawake waliokimbia makazi yao wakisubiri kupokea msaada wa pesa taslim katika Kivu Kaskazini, DR Congo.
© UNHCR/Blaise Sanyila
Wanawake waliokimbia makazi yao wakisubiri kupokea msaada wa pesa taslim katika Kivu Kaskazini, DR Congo.

Watu 500,00 wamefurushwa kwenye maeneo yanayodhibitiwa na M23

Tangu Oktoba mwaka jana, Kamishina mkuu amesema watu 500,000 wamefurushwa kutoka maeneo yanayodhibitiwa na M23, na hivyo kufanya jumla ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo la Kivu Kaskazini hadi kufikia karibu watu milioni 2.7.

"Huko Ituri, pamoja na mapigano miongoni mwa jamii, pia kumekuwa na mapigano kati ya CODECO na makundi ya waasi ya Zaire, kundi lenye silaha la ADF (Allied Democratic Forces) liliongeza mashambulizi yake dhidi ya raia, na kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu".

Hadi sasa, kuna takriban watu milioni 1.8 waliokimbia makazi katika jimbo hilo. Vikosi vya usalama wa taifa na wanamgambo, kama wazalendo, pia wanafanya ukiukaji wa haki za binadamu ambao lazima uzuiwe.

Volker Türk Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika mahojiano na UN News
UN Photo/Mark Garten
Volker Türk Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika mahojiano na UN News

Ziara Bunia, Ituri na Goma

Wakati wa zara yake, Kamishna Mkuu alitembelea kambi za wakimbizi wa ndani huko Bunia, Mkoa wa Ituri, na Goma, Mkoa wa Kivu Kaskazini. 

Ingawa migogoro inayotokea katika majimbo haya mawili inatofautiana, matokeo yake ni sawa.

"Watu katika maeneo yote mawili wakimbizi walinielezea jinsi walivyokimbia mapigano na sasa wanahitaji msaada. Pia wameonyesha hamu yao kubwa ya kutaka kurudi nyumbani. Mfano mtetezi mmoja wa haki za binadamu aliniambia kuwa vita vimetuibia kila kitu, ikiwa ni pamoja na maisha yetu ya baadaye".

Kumekuwa na ongezeko kubwa la waathiriwa wa ukatili wa kijinsia, katika maeneo ambayo mapigano yanafanyika, lakini pia katika kambi za wakimbizi wa ndani. 

"Katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo huko Goma, wale niliozungumza nao walinielezea jinsi wanawake walivyoshambuliwa walipokuwa wakitafuta kuni ili kuandaa chakula, na jinsi baadhi ya wanawake na wasichana walivyolazimishwa kujiuza ili kujikimu," amesema kamishina mkuu.

Familia ikiwa kwenye makazi yao huko jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia shambulio kubwa kwenye kambi ya wakambizi
© UNHCR/Hélène Caux
Familia ikiwa kwenye makazi yao huko jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia shambulio kubwa kwenye kambi ya wakambizi

Serikali lazima itemize wajibu wake Mashariki mwa DRC

Mkuu huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa ni muhimu kwamba Serikali iweze kutekeleza kikamilifu jukumu lake mashariki mwa DRC, kutekeleza masuala ya usalama lakini pia kutoa huduma muhimu kama vile elimu na afya. 

Ameongeza kuwa serikali lazima pia itoe suluhu fmuhimu, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa haki kupitia mfumo wa haki na ufanisi wa mahakama.

"Nchi hizo ambazo zinaunga mkono au kuwa na ushawishi kwa makundi yenye silaha lazima zichukue jukumu lao kuhakikisha mapigano yanakoma. Huko Kivu Kaskazini, jukumu lolote la Rwanda katika kuunga mkono M23 lazima likomeshwe, na suluhu lazima ipatikane kwa haraka. Vile vile kwa nchi yoyote ambayo inaunga mkono makundi yenye silaha nchini DRC,” 

Mojawapo ya sababu kuu za migogoro hii amesema ni unyonyaji wa maliasili za DRC ambao unafanya umaskini kuongezeka badala ya kuwanufaisha wakazi wa eneo hilo. 

Amesema serikali, pamoja na mamlaka za kikanda na kimataifa, zina wajibu hapa. Sekta binafsi pia ina majukumu muhimu, ikiwa ni pamoja na biashara zinazochimba rasilimali, kama vile coltan, ambazo ni za thamani sana kwa ulimwengu.

"Sote tunatumia simu za rununu ambazo zinawezekana, kwa kiasi kikubwa, kutokana na rasilimali za DRC. Dunia haiwezi kuendelea kula kwa gharama ya watu wa Congo. Kila mtu anapaswa kujiuliza jukumu lake liko wapi,” amesema bwana.